Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinauarifu umma kuwa namba ya simu ya Mrugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Mhe. Brenda Rupia 0789160733, iliyokuwa ikitumika kuchangisha michango kwa ajili ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa chama, imefungiwa na kampuni ya Airtel Tanzania tangu tarehe 19 Januari 2026.
Baada ya kufanya mawasiliano na uongozi wa Airtel, wamegoma kueleza kwanini wameifungia namba hiyo badala yake wamesema wanamtaka muhusika kufika katika ofisi zao popote nchini.
Hatua ya kumtaka mtu kufika kwenye ofisi zao inashangaza kwani kampuni hiyo imekuwa ikihamasisha huduma za kidijitali kwa wateja wake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza msongamano wa watu katika matawi yao.
Chadema inalani vikali kitendo hiki na kuitaka Airtel Tanzania kuacha kujihusisha au kutumiwa na mifumo ya kisiasa kukandamiza demokrasia na kukiuka haki za raia.
Aidha, tunasisitiza umuhimu wa kampuni hiyo kulinda faragha na haki za watumiaji wa huduma zake.
Pili, tunaitaka Airtel Tanzania kufungua mara moja akaunti hiyo ya Airtel Money, kwani kuchangisha michango kwa uwazi kwa madhumuni halali si kosa.
Taifa linafahamu vyema lengo la michango hiyo na hakuna sababu ya msingi ya kuzuia shughuli hiyo ya kidemokrasia.
Chadema itaendelea kupigania haki, uwazi na demokrasia bila woga wala kuyumba.