JokaKuu, that is the point. Kabla ya mwaka 1992 tulikuwa na chama kimoja CCM na ni wachache tu kama mimi ambao waliweza kujitenga na kukaa kando bila kujiunga na CCM toka iasisiwe mwaka 1977. Wengi wa wanamageuzi wa mwanzo ama walikuwa ni wana CCM hai au ambao walikuwa CCM mfu ikiwa na maana kwamba ni kwa mwili tu na si kwa moyo. Kujiunga na upinzani kulionekana na kuhesabika kwa baadhi ya watu kama uenda wazimu au usaliti. Wanamageuzi wa mwanzo waliogopwa kama ukoma na sehemu kubwa ya jamii.
Kupigania mabadiliko ya utawala kulitafsiriwa na sehemu kubwa ya jamii kama uroho wa madaraka wakati ukweli ni kwamba waroho wa madaraka ni wale walioyahatamia na kuyang'ang'ania. Ingawa upinzani umefanya kazi kubwa kuuelimisha umma lakini Watu kama hao bado tunao na wengi kama si wote ni wanachama wa CCM. Lakini pia wapo wachache ambao hawaungi mkono CCM kwa mambo mengi lakini wanalazimika kubaki humo kulinda maslahi yao.
Ni hawa ambao kitendo cha Lowassa kinaweza angalau kuwatoa hofu na ama kuwapa ujasiri wa kumfuata huko aliko au kumpigia kura kama atasimama kama mgombea Uraisi. Lakini pia tusisahau kwamba na huko upinzani tunao ambao watauona ujio wa Lowassa kama unahatarisha nafasi zao ndani ya UKAWA. Hapa ndipo natofautiana na wengi kwa sababu naamini kama mtu hasukumwi na ubinafsi, atamkaribisha yeyote na chochote kile mradi kinamuongezea nguvu katika mapambano kama tuliyo nayo kama upinzani.
Tukubali tusikubali ujio wa Lowassa kumeiongezea nguvu UKAWA na pia kuteuliwa kwake kama mgombea kumepunguza kwa kwango fulani sintofahamu (tension) iliyoanza kuota mizizi kuhusu yupi ashike usukani kati ya CUF, Chadema na NCCR. Katika hivi vyama vinavyounda UKAWA, wako wanachama ambao haingekuwa rahisi kwao kuafiki haraka haraka wateule wao wa awali kuenguliwa. Ujio wa mtu mpya ambaye anatoka nje ya watarajiwa kunaleta muafaka na kupunguza munkari ambao wangekuwa nao vinginevyo.
Binafsi nilimpenda Dr. Slaa apeperushe bendera hiyo, lakini ninaye rafiki yangu ambaye alimuona Prof. Lipumba kama anafaa zaidi...kwa bahati sote wawili tumeunga mkono pendekezo la Lowassa kuteuliwa. Nakiri uteuzi wa Lowassa yawezekana umewavunja mioyo watu wengine lakini kwa maslahi mapana ya UKAWA naamini jibu sahihi ni hilo kama lengo ni umoja katika kumuondoa mkoloni CCM. Ningefurahi zaidi kama walengwa wawili hao, Dr. Slaa na Prof. Lipumba wangeunga mkono hayo maamuzi na tusonge mbele.