Msichoelewa ni kuwa tunategemea CDM wata behave tofauti na CCM. Ndio maana tunasikitika tunapoona wanafanya yale yale ambayo wanawashutumu CCM. Na kibaya zaidi ni pale ambapo badala ya kusikitikia tukio, wao wanasema mbona CCM wanafanya haya haya!
Amandla...
Kwa nini mnakuwa watu mnaopenda uwongo? Ni wapi CHADEMA imesema kuwa ni halali kupigwa kwa sababu na CCM wanafanya hivyo hivyo?
Mimi nilihudhuria kikao cha ndani cha Njombe. Ukisikia yanayosemwa mitandaoni kuhusiana na kilichotokea kwenye kikao, zaidi ya 50% ni uwongo.
Kikao kile cha ndani, hakikuwa cha siri, na Heche alisema wazi kuwa hata wanachama wa kawaida wanaruhusiwa kuhudhuria ili washuhudie viongozi wao wanayoyajadili. Kwa sababu kikao kilikuwa open, sioni shida hata kutamka yale yaliyotamkwa na kutokea mle ndani:
Baada ya Heche na Dr. Slaa na Mwakajoka kuelezea dhima ya NO REFORM NO ELECTION, Heche alisema kuwa anataka kusikia maoni na hata maswali kutoka kwa wote waliohudhuria. Akawaomba wanaotaka kuongea wanyoshe mikono, alipooona ni wengi, aliomba waorodheshwe majina, na akasema wazi kuwa kila anayetaka kuongea apewe nafasi. Yeye yupo tayari kuwasikiliza hata kama itakuwa ni mpaka asubuhi. Waliojiorodhesha walikuwa 37.
Heche akawaambia wajumbe kuwa kwa idadi hiyo, kila mmoja akiongea kwa dakika 3, itachukua daki 111. Kama kila mmoja ataongea kwa dakika 2, itachukua daki 74. Akawauliza wajumbe wanataka kila mmoja aongee kwa dakika ngapi, akawataka wanaotaka dakika 3, wanyoshe mikono, wakanyosha watatu tu. Wengine wote wakasema dakika 2.
Utaratibu wa kuongea ulifuata mpangilio wa uandikishaji majina. Lakini ulibadilika ghafla baada ya Sigrada kuonesha kuwa anataka kuongea. Kwa sababu ya heshima ya nafasi yake akapewa nafasi ya kuongea, tena bila ya kuzingatia zile dakika 2 ambazo wajumbe wengine walikuwa wanapewa.
Sigrada, kwa mara ya kwanza alikatisha mpangilio wa kuongea, baada ya kiongozi wa jimbo la Makambako kudai kuwa viongozi wa kitaifa na hususani Sigrada, wanawadharau viongozi wa majimbo, akadai kuwa Sigrada aliandika barua kwa OCD kuwataarifu polisi kuwa anafanya mkutano wa hadhara Makambako, bila ya wao kupewa taarifa. Taarifa waliyopewa ni kuambiwa tu waende kwenye mkutano. Malalamiko hayo ndiyo yaliyomwinua Sigrada na kukatisha mpangilio wa kuongea. Heche aliivumilia hali hiyo, akamwachia Sigrada aongee. Aliongea mengi sana, lakini kikubwa alidai kuwa viongozi hao wa Makambako na mkoa wanamhujumu. Baada ya pale, viongozi wa mkoa, BAWACHA mkoa, viongozi wa Makambako na viongozi wa kanda, walihojiwa na Heche. Jambo ambalo halikuwa la kawaida ni kwamba, Sigrada alipokuwa anaongea, wote walikaa kimya, lakini hao viongozi wengine wakihojiwa, wanapotoa maelezo Sigrada alikuwa hawezi kutulia, aliinuka na kuwakatiza wenzake. Tena anasimama na kuongea kwa kunesanesa.
Heche mara kadhaa alimsihi atulie, Sigrada alisema hawezi kutulia kwa sababu wanasema uwongo. Alipoambiwa akae chini, aligoma. Heche akamwambia kuwa kama hawezi kutulia ni aheri atoke nje, Sigrada akasema kuwa itakuwa afadhali. Heche akamwambia, haya toka nje, Sigrada akatoka nje, huku anaenda anaongea. Alitoka mwenyewe, hakuguswa na yeyote.
Huku nyuma, Heche alisikitika sana, na akasema mbele ya wajumbe kuwa Sigrada amemvunja sana moyo kwa sababu alimheshimu sana. Akasema kuwa hata kabla ya kugombea nafasi aliyo nayo yeye Heche, Sigrada ndiye aliyempigia simu na kumwomba agombee. Baada ya maneno hayo ya Heche, Dr. Slaa alisimama na kusema kuwa watu wote wamehuzunishwa na alichofanya Sigrada, lakini baada ya kutolewa nje, anaomba arudishwe, apewe nafasi nyingine, pengine kwa kutoka nje atakuwa ametafakari. Akatumwa mtu kwenda kumwita. Lakini muda wote alipokuwa nje tulikuwa tunasikia anaongea kwa kelele. Alikuwa anaongea na nani? Alikuwa anaongea nini?, labda waliokuwa nje ndio wanaojua.
Tulichoshangaa, hata baada ya kutumwa mtu kwenda kumwita, Sigrada hakurudi tena ukumbini. Muda aliotolewa ilikuwa majira ya karibia saa saa 4 usiku. Kikao kikaisha majira ya saa 6 usiku. Tunatoka nje, hatukumwona Sigrada, polisi walikuwa bado wapo, mlinzi wa Heche alikuwa bado yupo.
Baada ya pale baadhi wa wajumbe wakasema hawawezi kulala njaa, wakaenda kwenye baa moja ambayo ni kama night club kwa sababu ipo wazi masaa 24. Wakamkuta Sigrada hapo baa. Muda wote, hakukuwa na taarifa yoyote kuwa kuna mtu amepigwa. Nina hakika wengi, ni kama mimi hatukujua kama huko nje kuna mtu yeyote alikuwa amepigwa. Kwa sababu sikuwa huko nje, siwezi kusema kwa uhakika kama Sigrada alipigwa au hakupigwa, na kama alipigwa, siwezi kujua alipigwa na nani. Lakini, logically, kama alipigwa, basi haikuwa kiasi cha kuumizwa sana maana kama angekuwa ameumia sana, sidhani kama angeenda baa badala ya kwenda hospitali.
Lakini pia, polisi walikuwepo pale nje ya ukumbi, muda wote wakati kikao kinaendelea, kama waliona mtu anatendewa jinai, kwa nini hawakuchukua hatua dhidi ya mhalifu? Kama kweli alipigwa na mlinzi wa Heche, mlinzi yule alikuwepo pale mpaka mwisho wa kikao, na aliondoka na Heche saa 6 usiku. Muda huo wote, wa zaidi ya saa 1, kwa nini hao polisi hawakumkamata huyo mlinzi wa Heche wakati polisi na huyo mlinzi, wote walikuwa nje ya ukumbi wa kikao?
Sigrada kama kweli alipigwa, iwe alipigwa sana au kidogo, siyo hoja, swali kubwa ni kwa nini polisi hawakumchukulia hatua huyo mhalifu hapo hapo wakati wa utendaji kosa?
Kumsaidia anayeumwa siyo tatizo, iwe anaumwa kwa sababu ya kipigo au kwa matatizo mengine ya kiafya. Cha kushangaza ni CCM kulifanya tukio hilo kama mileage ya kisiasa dhidi ya CHADEMA. KAMA CCM wangekuwa na dhamira njema wangeweza kutoa mchango wao wakamkabidhi Sigrada au familia yake. Wangeweza kumsaidia kugharamia usafiri kama kuna haja hiyo. Lakini jukumu la kumhudumia mgonjwa lingebakia kuwa la familia na ndugu wa karibu. Lakini CCM wamemgeuza Sigrada kama kitu cha maonesho. Hali hii inatia mashaka makubwa juu ya dhamira ya CCM dhidi ya Sigrada.
Angalizo:
Ukiona mtu alikuwa adui yako, ghafla anabadilika na kujifanya rafiki na mtu wa karibu sana kwako, chukua tahadhari kubwa.
Maombi yangu kwa Mungu: Mungu amwepushe Sigrada na kila dhamira mbaya iliyojificha dhidi yake. Na tunamwomba Mungu awaaibishe waovu wote na mipango yao mibaya, na uovu ule waupangao dhidi ya Sigrada na chama chake. Uovu waupangao dhidi ya Sigrada au chama chake, uwarudie maradufy na kwa namna ya kujutia.
Tunaogopa hata kwenda kumjulia hali Sigrada kwa sababu ya kuhofia kuwa unaweza kwenda, halafu waovu wakaitumia hiyo nafasi kumfanyia uovu kwa kisingizio kuwa uliyeenda kumwona ndiye mhusika.
Mungu wetu ni mkubwa, hata katika hili, waovu wataumbuka.