Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo amesema atakifanyia marekebisho kikosi chake na kuonya kama mchezaji hatataka kuwa wa kulipwa hatafanya naye kazi. Akizungumza mjini hapa, Maximo alisema mabadiliko atakayofanya ni ya kawaida, ambayo yamelenga kuwaingiza zaidi vijana katika timu hiyo.
Baada ya fainali hizi za CHAN, basi nitafanya marekebisho ya kawaida katika kikosi changu, lengo likiwa ni kuleta damu changa katika timu kwa manufaa ya siku zijazo. Ninachoshukuru kwa sasa ni kuwa tayari ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20 katika klabu za Ligi Kuu zimeanza, ambayo ndiyo naamini itaibua vipaji vipya.
Nimelenga kuwaingiza chipukizi saba katika kikosi, alisema bila kutaja majina. Pia Maximo alisema itakuwa ni vigumu kufanya kazi na mtu ambaye hatataka kucheza kitaalamu na nidhamu nje na ndani ya uwanja. Nitakuwa naye bega kwa bega mchezaji ambaye anaonyesha juhudi kwa kujituma kwa ajili ya nchi na si kuwa mbinafsi, alisema bila kuelezea kiundani kama kuna mchezaji yeyote katika kikosi chake ambaye ana tabia kama hiyo.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Maximo imekuja huku kukiwa na taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo kuwa baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipishana lugha na kocha huyo, hali inayozua hofu kuhusu majaliwa yao katika siku za usoni katika klabu hiyo.
Maximo alipotakiwa kujibu anakionaje kikosi cha Stars kilichocheza bila kuwapo nyota wake kadhaa, Maximo alisema: Mchezaji nyota?, huyo atakuwa mchezaji nyota wa magazeti. Katika kikosi changu wachezaji wote wako sawa. Majina si kitu kuliko timu yenye nidhamu, mchezaji muhimu ni yule mwenye nidhamu ndani na nje ya uwanja na anayetekeleza majukumu yake ipasavyo awapo uwanjani.
Katika mechi ya juzi wachezaji ambao hawakuvaa jezi ni Godfrey Bonny ambaye ni majeruhi aliyeumia kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Senegal na Athuman Idd ambaye tangu awali kocha alisema hatamtumia kwenye mechi za makundi kutokana na kusumbuliwa na nyama za paja na kupanga kumchezesha timu itakapotinga nusu fainali.
Wachezaji wengine ni kipa Farouk Ramadhani, Amir Maftah ambaye hajapangwa hata mechi moja na Haruna Moshi Boban ambaye katika mechi ya kwanza alicheza chini ya kiwango. Pia Maximo alitaka wazo la kuendelea kucheza soka la ridhaa lifutike vichwani mwa wadau na wachezaji na kuwa kinachotakiwa sasa ni kuwazia soka la kulipwa.
Kuna haja ya wachezaji kuwa na mawazo ya wachezaji kucheza soka la ridhaa yafutike kichwani mwao, kama mchezaji anafikiri mbali na kuishia kuja hapa kwa ajili ya kujionyesha, hayo ni mawazo ya kizamani. Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib amewataka wachezaji wa Taifa Stars kuhakikisha wanashinda mechi dhidi ya Zambia kesho na kufuzu nusu fainali.
Khatib, ambaye pia aliwapa changamoto kama hiyo kabla ya mechi dhidi ya Ivory Coast, alisema Stars ina uwezo wa kufika fainali kwa kuishinda Zambia. Alisema kinachotakiwa kufanywa na wachezaji wa Stars ni kujituma uwanjani na kucheza kwa utulivu kama walivyocheza na wenyeji.
Alipoulizwa kama hahofii kuwa nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa kuungana na kupanga matokeo, Khatib alisema: Kinachocheza si lugha bali ni mpira, kinachotakiwa ni ushindi tu." Naye Balozi wa Tanzania kwa nchi 14 za ECOWAS, Msuya Mangachi aliwataka wachezaji kujua kufanya vizuri katika michuano hiyo ni kuipandisha chati nchi kidiplomasia.
Mjue kazi nzuri mnayoifanya hapa inasaidia kupandisha hadhi ya nchi katika masuala ya diplomasia, mkifanya vizuri na kufika fainali basi ujue kuwa mtakuwa mkizungumzwa na kila taifa, alisema Balozi huyo. Alisema wachezaji wanatakiwa kutoridhika na ushindi walioupata dhidi ya Ivory Coast, bali waongeze juhudi katika mechi dhidi ya Zambia ambayo itakuwa ngumu.
Stars inahitaji ushindi ili ifuzu nusu fainali. Wakati huo huo, habari tulizozipata jana usiku wakati tukienda mitamboni ni kuwa wachezaji Haruna Moshi, Athumani Idd Chuji na Amir Maftah wametishiwa kutimuliwa kambini kwa madai ya utovu wa nidhamu. Kulingana na chanzo chetu ndani ya kambi hiyo ni kuwa wachezaji hao wanadaiwa hawana ushirikiano mzuri na wenzao, huku wakionekana kama wamejitenga na kuonekana kwamba wanaweza kupunguza mshikamano katika timu hiyo.
Hata kauli ya Maximo kwamba atabadili kikosi chake ni kutokana na hasira za kuudhiwa na baadhi ya wachezaji, alisema mtoa habari wetu. Alisema katika kikao kilichoitishwa jana kati ya Maximo, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliopo mjini hapa na wachezaji hao zilieleza kuwa tayari uamuzi wa kuwarudisha nyumbani ulifikiwa, lakini busara ikatumika ili mambo yasiharibike zaidi. Source: Gazeti la Habari Leo