Wizara ya Biashara ya China hivi karibuni imelaani vikali uchunguzi unaofanywa na Tume ya Umoja wa Ulaya kuhusu uchunguzi wa kampuni zinazotengeneza magari ya umeme, ambapo Umoja wa Ulaya unataka kiasi kikubwa cha taarifa zinazohusiana na siri za kibiashara za viwanda hivyo. Wizara hiyo imerejea ahadi yake ya kuchukua hatua zote zinazotakiwa kulinda haki na maslahi ya kampuni za China.
Watengenezaji wa magari nchini China wametaka hatua kali za kujibu kitendo hicho cha Tume ya Umoja wa Ulaya zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na kuongeza kwa muda kiwango cha ushuru kwa magari yanayoagizwa kutoka nje yenye injini kubwa, huku viwanda husika vya ndani vikiomba ama kupanga kuomba uchunguzi ufanyike kwa baadhi ya bidhaa zinazoto9ka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, ikiwemo maziwa. Pia, maofisa wa China wameahidi kuchukua hatua zote zinazotakiwa kutetea haki na maslahi ya wafanyabiashara wa China.
Wakati huohuo, utafiti uliofanywa hivi karibuni umeonyesha kuwa, imani ya wafanyabiashara wa China kwa soko la Umoja wa Ulaya imepungua kwa kasi kufuatia uchunguzi wa Umoja huo dhidi ya magari ya umeme ya China na pia ushuru mkubwa unaotozwa kwa magari hayo. Hatua hiyo ya Umoja wa Ulaya imedhoofisa sana ushirikiano kati ya China na Umoja wa Ulaya, na itatoa pigo kubwa kwa uchumi wa Umoja wa Ulaya ambao unakabiliwa na changamoto nyingi.
Akijibu swali kuhusu mkutano wa ndani kati ya watengenezaji magari wakubwa wa China na Umoja wa Ulaya, ambapo kampuni husika zilisema Umoja huo unadai siri za ndani za kibiashara, Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China He Yadong amesema, Tume ya Umoja wa Ulaya imetaka kupewa taarifa nyingi kuhusu uzalishani na operesheni, mipango ya maendeleo, mchakato wa kiufundi, mfumo wa bidhaa na taarifa nyingine kutoka kwa kampuni za China zinazotengeneza magari ya umeme na betri. Amesema aina, muundo na wingi wa taarifa zilizokusanywa na Tume hiyo hazikutarajiwa na haziendani na uchunguzi huo unaofanyika. Pia amelaani adhabu ya ushuru iliyotolewa na Tume hiyo kwa madai kwamba kampuni za China hazikutoa ushirikiano, hatua iliyowashangaza na kuwasikitisha wamiliki wa kampuni wa China.
Bw. He amesisitiza kuwa, hatua ya Tume ya Umoja wa Ulaya imekosa msingi wowote wa uhalali na kisheria, inakiuka kanuni za Shirika la Biashara Duniani (WTO), inavuruga ushindani wa usawa na kudhoofisha mageuzi ya kijani duniani na ushirikiao wa wazi.
Juni 18, kampuni kubwa za China na Ulaya zinazotengeneza magari zilifanya mkutano wa ndani, ambapo watengenezaji wa magari wa China na mashirikisho ya sekta hiyo yalipinga uamuzi wa Umoja wa Ulaya dhidi ya magari ya umeme ya China, na kuitaka serikali ya China kuchukua hatua za kujibu, ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha ushuru kwa magari yanayoagizwa yenye injini kubwa.
Cha ajabu ni kwamba, watengenezaji wa magari wa Ulaya waliohudhuria mkutano huo pia walipinga hatua ya Tume ya Umoja wa Ulaya ya kuongeza ushuru wa ziara kwa magari ya umeme yanayotengenezwa nchini China, na kueleza matarajio yao kwamba China na Umoja wa Ulaya zitaanza majadiliano haraka iwezekanavyo ili kuepuka mvutano zaidi wa kibiashara kati ya pande hizo mbili.
Kuhusu kama Wizara ya Biashara ya China itaanza kufanya uchunguzi kwa bidhaa za maziwa zinazotoka katika nchi za Ulaya, Bw. He amesema Wizara hiyo imepokea maombi yaliyotolewa na viwanda husika, ambavyo vina haki ya kuomba kufanyika kwa uchunguzi huo chini ya sheria za China na kanuni za WTO.
Wakati huohuo, utafiti uliochapishwa na Shirikisho la Wafanyabiashara wa China katika Umoja wa Ulaya (CCCEU) umeonyesha kuwa, asilimia 82 ya kampuni zilizofanyiwa uchunguzi zimesema uchunguzi huo wa Umoja wa Ulaya umesababisha kushuka kwa uaminifu kwa uwekezaji barani Ulaya, huku zaidi ya asilimia 70 zikisema kuwa uchunguzi wa Tume ya Umoja wa Ulaya umekuwa na athari hasi kwa mauzi barani Ulaya.