Hivi ndivyo Mwananchi inavyosema juu ya upupu wa Mkumbwa wa gazeti la Ujinga wa KilaSiku (Daily News)
Gazeti la serikali lazua jambo
Thursday, 23 September 2010
Exuper Kachenje na Salim Said
MAONI ya mhariri yaliyotolewa kwenye gazeti la jana la serikali dhidi ya mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, yameibua hisia kali baada ya makamu mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kueleza kuwa yanauma, huku wanaharakati wakieleza kuwa ni ya hatari kwa demokrasia na ya uchochezi.
Katika majumuisho ya tahariri hiyo, gazeti hilo, The Daily News lilisema: "Na ukweli ni kwamba Dk Willibrod Slaa hatakuwa rais wa tano wa Tanzania."
Kauli hiyo ya gazeti hilo ambalo ni mdomo wa serikali limeibua hisia tofauti kutoka kwa wanasiasa, wasomi, wanaharakati ambao wamelaani na kutaka sheria ichukue mkondo wake.
Dk Slaa, ambaye anaonekana kuzoa mashabiki kadri siku zinavyokwenda, alisema: "Hii inaonyesha kuwa serikali ina mpango mchafu ndio maana wametumia gazeti la serikali.
"Lakini nguvu ya Dk Slaa itathibitishwa kwa kushinda uchaguzi na kwenda Ikulu. Na kwa maana hiyo siku za mhariri zinahesabika."
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye alisema: "Tunataka uchaguzi huru na wa haki. Vyombo vya umma vinatakiwa kutumika kwa ajili ya umma na si CCM. Tuumesikitishwa na tahariri hiyo.
"Tunachotaka ni mhariri achukuliwe hatua haraka kwa sababu hiyo inaonyesha mkakati wa serikali si mzuri kwa wapinzani."
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana watu mbalimbali walioongea na Mwananchi walisema kitendo hicho cha gazeti la serikali ni cha kujaribu kuliingiza taifa kwenye machafuko.
Makamu mwenyekiti wa Nec, Jaji Omar Makungu alisema kauli kwamba Dk Slaa hataingia Ikulu, inaumiza lakini ni juu ya Chadema na Dk Slaa kuamua kulalamika kama wataona imemwathiri.
Jaji Makungu alisema Nec imesikia kauli hiyo lakini haiwezi kuifanyia kazi mpaka kuwe na mlalamikaji.
"Sijalisoma hilo gazeti hilo lakini kauli hiyo inauma... inatakiwa walioumizwa walalamike. Wakikaa kimya, sisi hatuwezi kuchukua hatua. Kamati ya maadili ipo; Chadema au Dk Slaa akilalamika, tutawaita wanaolalamikiwa," alisema Jaji Makungu.
"Tupo tayari kupokea malalamiko. Tuna kamati ya maadili, wakicomplain (wakilalamika), tutajadili na kutolea uamuzi."
Meneja wa kampeni wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu amelitaka gazeti la Daily News kuutangazia umma wa Watanzania kuwa linamilikiwa na CCM badala ya serikali.
"Ni vyema Daily News ikawatangazia Watanzania kwamba wao ni gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) na sio la umma," alisema Profesa Baregu.
Alisema kwa muda mrefu gazeti hilo limekuwa likijionyesha dhahiri kufanya kazi za CCM badala ya kuutumikia umma.
Hata hivyo Profesa Baregu alisema gazeti hilo halina uwezo wa kuwashawishi Watanzania kwa sababu mzunguko wake ni mdogo sana na umeegemea zaidi kwenye wizara na taasisi za serikali.
Alifafanua kuwa CCM na vyombo vyake vya habari wamekuwa na jazba baada ya kuona mgombea wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amegeuka kuwa mtaji mkubwa wa Watanzania.
"Rais wa serikali ya awamu ya tano ataamuliwa na Watanzania kupitia kura zao na hakuna mtu yeyote wa kuchezea kura hizo," alisema Profesa Baregu.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya alisema aliungana na Baregu kusema kuwa uamuzi wa kuchagua rais, wabunge na madiwani ni wa wananchi na unafanywa kwa njia ya kura zao na si chombo cha habari au waandishi.
"Katika kampeni kila mmoja anatoa ya kwake, lakini uamuzi ni wa wananchi. Si waandishi wanaoamua, gazeti au chombo chochote cha habari," alisema.
"Ni kura za wananchi. Ninavyojua mimi vyombo vya habari vinatakiwa kufuata maadili, viepuke vitu vinavyoweza kuleta mgogoro. Hatupaswi kuchochea migogoro. Tuwe makini."
Alisema kitendo kilichofanywa na gazeti hilo ni cha hatari kwa sababu kinakandamiza demokrasia na kujenga hisia kuwa huenda kitendo kilichofanywa na gazeti kinashabikiwa serikali hivyo kuweza kuchochea vurugu ndani ya nchi.
"Kitendo kilichofanywa na gazeti hilo ni cha hatari kwani kinaweza kuchonganisha serikali na watu wake na wakaweza kufanya vurugu kwa kile wanachoweza kukiona hawatendewi haki," alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Fordia, Bubelwa Kaiza alisema Daily News ni gazeti la serikali kwa maana hiyo, mhariri na wenzake hawawezi kujituma bali wametumwa na chama au serikali iliyo madarakani.
"Kwa maana hiyo si tu kwamba amekiuka maadili ya taaluma ya habari, lakini, yeye na wenzake wote hawafai kuwapo hapo na kwa kashfa hii, wanapaswa kujiuzulu mara moja kwa kusimamia uovu," alisema Bubelwa.
"Kama amekubali (mhariri) kutumika vibaya na maadili ya taaluma yake, ni kwamba amehongwa fedha au ameahidiwa cheo na kwa hiyo ni rushwa na ufisadi mkubwa wa matumizi mabaya rasilimali za umma."
Kaiza aliongeza kusema: "Kwa vyovyote huyo anayesemwa (Dk Slaa) ni bora zaidi kuliko hao wasiosemwa, awe ni rais na waziri mkuu waliopo madarakani au aliyejiuzulu. Hatupendi kuzungumzia masuala ya ndani ya watu, lakini wote tunawajua ‘A' to ‘Z' (mwanzo hadi mwisho)."
Hata hivyo, Kaiza alibainisha kuwa habari hiyo haiwezi kuathiri chochote katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu Daily News ni gazeti la Kiingereza na halina wasomaji wengi ambao ni wapigakura, lakini pia mzunguko wake ni mdogo sana.
"Linasomwa sana na watu wanaotafuta matangazo ya kazi, wageni, wizarani na watanzania wachache wanaopenda kutangaza kupitia gazeti hilo," alisema Kaiza.
"Ni vyema chama na mgombea aliyetajwa kwa kutumia sheria na vyombo vilivyopo akatetea haki yake kwa sababu ni jambo kubwa na la kustua hakutendewa haki."
Meneja kampeni wa CCM, Abdulrahman Kinana jana alikataa kuzungumnzia tuhuma zilizoelekezwa kwa chama hicho akieleza kuwa gazeti hili, halitendi haki kwa CCM.
"Lakini ninyi (Mwananchi) you never have good news for CCM (hamna habari njema kwa CCM) kila siku mkipiga simu ni habari mbaya, mnaandika habari mbaya tu za CCM, nzuri hamzioni," alihoji.
"Mara Mama Salma kafanya hivi, mara Ridhwani kafanya vile, why can't you be carrier of good news? Always you carry bad news? (wakati wote ni mabaya tu, hamwezi kuandika mema ya CCM?
"Tafadhali waulizeni Daily News suala hilo."