Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea na operasheni kali ya kuzuia vitendo vya kihalifu ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu waliotenda makosa ya kijinai ya siku za nyuma katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
Katika hatua hiyo Polisi wamemkamata GADI DAUDI@ tito Jeshi la mtu mmoja (28) Mkazi wa Ubungo Riverside kwa tuhuma za kumuua JULIUS FREDRICK (22) Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kumpora simu yake ya mkononi .Tukio hilo lilitokea tarehe 16/07/2022 majira ya saa kumi usiku huko eneo la karibu na hosteli za Magufuli Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam baada ya kumvizia, kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili, kupora vitu vyake ikiwemo simu na kumsababishia kifo.
Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam lilifanya upelelezi na ufuatiliaji wa kina na tarehe 27/07/2022 lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo maeneo ya Sinza, Kinondoni, baada ya kumuhoji kwa kina alikiri kumuua mwanafunzi huyo na kumpora vitu vyake na alikiri pia kufanya matukio kama hayo ya unyanganyi kwenye maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, Uchunguzi wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo ni mhalifu sugu ambaye amekuwa akifanya matukio ya kiuhalifu maeneo ya Mlimani city, Mwenge na Kawe, na aliwahi kushtakiwa kwa kesi ya UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA kesi No. 256/2020 na kufungwa miaka 30 kuanzia tarehe 6 Julai 2020, na aliachiwa huru Aprili 2022 kwa sababu za kisheria baada ya kukata rufaa.
Tarehe 1.8.2022 majira ya saa kumi na nusu jioni Mtuhumiwa alikubali kuwapekeleka askari kuwaonesha alipoficha silaha anazotumia katika uhalifu na simu ya marehemu aliyoipora katika vichaka vilivyopo eneo la katikati ya Mlimani city na Hostel za Magufuli.
Baada ya kufika eneo hilo alikurupuka na kuanza kukimbia kuelekea kwenye vichaka vya ndani zaidi. Askari walifyatua risasi tatu hewani kumtahadharisha kusimama lakini alikaidi na hivyo kulazimika kumzuia kwa risasi iliyomjeruhi kwenye paja la mguu wa kushoto, kuanguka chini na kukamatwa kutoka katika jaribio la kutoroka chini ya ulinzi huku akikabiliana na tuhuma nzito za mauaji . Alipelekwa hospitali kwa matibabu. Eneo hilo Polisi imepata panga moja, sime, bisibisi na simu mbili za mkononi.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam liendelea na msako mkali kuwakamata wahalifu wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu na malengo ni kuhakikisha watu wanafanya shughuli zao katika mazingira yaliyo salama , bila hofu na kwa kuzingatia sheria za nchi.