Jana Lissu alisema Mwendazake amekufa lakini waliokua wakimsaidia kutesa na kuumiza watu hawajafa. Bado wapo. Wanaweza kuwa wameficha makucha tu kwa muda lakini wakishamsoma mama, watarudi tu.
Na hiki ndicho kilichotokea. Polisi wenye silaha wamezingira ukumbi wa Hekima Garden, Mikocheni kuzuia hafla ya chakula cha jioni iliyoandiwa na Baraza la wanawake la Chadema (BAWACHA).
Iko hivi, Bawacha wameandaa hafla ya kuwakutanisha wanawake wa Chadema kubadilishana mawazo na kuzungumza mambo yao kama akina mama.
Wakaandika barua kwa Mkurugenzi kumpa taarifa. Lakini Mkurugenzi akasema wapeleke maombi yao kwa DC. Wakapeleka barua kwa DC Gondwe. Katika hali ya kushangaza Gondwe eti nae akaagiza barua ipelekwe kwa RC. Yani danadana zisizo na ulazima wowote. Yani akina mama kukaa na kula kuku zao hadi RC atoe ruhusa?
Anyway, barua ikapelekwa kwa RC lakini Makalla akaingia mitini. Hataki kujibu. Baada ya kusumbuliwa sana akaagiza waende kwa RPC Kinondoni. RPC kaagiza waende kwa OCD Oysterbay. OCD akaruhusu hafla ifanyike kwa masharti yafuatayo;
1. Pasiwepo na mziki.
2. Pasiwepo na pombe.
3. Hafla ifanyike kwa dakika 30 tu.
4. Askari waingie ukumbini kusikiliza wanachojadili.
5. Wakimaliza kula watawanyike haraka.
Wanawake wa BAWACHA wamegomea masharti hayo, wanataka wawe huru kufanya mambo yao.
#MyTake;
Mama kemea hawa watu watakuharibia sasa hivi. Hawa akina mama ni wanawake wenzako. Wameamua kukaa, kula na kujadili mambo yao. Kwanini wananyanyaswa? Mwendazake aliwabagua watu kwa vyama vyao. Wapinzani wakawa mistreated kama vile magaidi. Wakapigwa, wakateswa na kunyanyaswa bila sababu.
Wewe ulianza vizuri kwa kuliunganisha taifa. Ukaahidi kuganga makovu yetu. Ukasema tusahau yaliyopita na tufute machozi. Lakini badala ya kutufuta machozi, mbona watu wako wameanza kutuletea machozi tena? Tafadhali wakemee. Jana tumefanya kongamano zuri la Katiba, na dunia imekupongeza kwa sababu polisi hawakutusumbua. Lakini leo hawa akina mama wanasumbuliwa? What happened?