Watanzania tusichambue mambo kwa hisia, hasa hili la makonteina ya Makonda. Kwanza kabisa, sheria ni sheria. Je Watanzania tunakumbuka TFF walivyopata shida kupewa msamaha wa kodi kwa ajili ya majani ya uwanja WA TAIFA? Na hayo majani yaliagizwa na serikali kwa jina la taasisi ya serikali. Sasa sembuse Makonda kuagiza vitu kwa jina lake!
Tunapaswa kuelewa kwamba ikiwa Makonda ataruhusiwa kutoa haya makontaina bila msamaha, yanatoka kama mali za Makonda. Atakuwa na uhuru wa kuyapeleka anakotaka, kuzigawia shule au mtu anaetaka, akisimamia huo ugawaji yeye mwenyewe. Hakutakuwa na udhibiti wowote wa serikali juu ya mali ndani ya makontaina hayo ziligawanywaje. Hilo ni suala la Makonda. Serikali haitakuwa na haki ya kuingilia wala kuweka ukaguzi wa aina yeyote, na wala Makonda hatatakiwa kuyahifadhi makontaina kwenye ghala yeyote ya serikali ili yangizwe kwenye leja ya serikali, kwa sababu ni mali za ya Makonda ambaye amekuwa mkarimu wa kusaidia shule.
Sasa upande wa serikali, ambayo haitakiwi kufanya kazi kwa hisia, suala linakuwa kwamba, unajuaje kama Makonda angewakilisha vifaa vyote kwa ajili ya shule, kama vifaa hivyo havina udhibiti wowote wa serikali kwa kuwa vimeagizwa na MAKONDA kama mtu binafsi?
Angalau basi kama Makonda angekuwa ni taasisi ya NGO basi angetakiwa kujieleza aligawaje zile mali, tena kwa kiasi fulani tu. Lakini kama Makonda hawajibiki kujieleza zile bidhaa za Bilioni 2 aligawa vipi, kama akiruhusiwa kuyachukua makontaina bila kulipia kodi. Kumbuka akiruhusiwa kuyataoa bila kodi, akajigawia sehemu ya mali hizo, huwezi kumshitaki popote pale.
Lakini mtasema ana nia nzuri. Sawa hatukatai, lakini ndio hapo tusiamue mambo kwa hisia. Jiulize, hivi kweli Makonda ni mtakatifu kiasi hicho, vitu vya Tshs bilioni 2 vije kwa jina lake, asishawishike angalau kujiwekea pembeni vitu vya bilioni moja wakati hakuna udhibiti wowote wa serikali wa hivyo vitu? Huyu Makonda akiangusha noti ya Tshs 1000 hataiokota kwa kuwa ameridhika kiasi hicho, kiasi alete bidhaa za Bilioni 2 na asiminye hata kidogo?
Ni wazi serikali inajiuliza, Makonda hapo alipo ana hela kiasi gani asishawishke kunufaika binafsi chini ya kivuli cha "vifaa vya shule" ambavyo havina udhibiti wa serikali? Mie sijawahi kuona Mtanzania mwenye uaminifu kiasi hicho, zaidi ya Nyerere na Sokoine!
Ukiwa waziri, unapopewa taarifa, unatumia na akili zako mwenyewe kujua nini cha kufanya. Kama Makonda ana uchungu na shule, basi atafute namna ya kukabidhi vifaa hivyo kwa serikali ili ndio iwe na jukumu la kuvigawa kwa shule kama mali ya serikali iliyoingizwa kwenye leja ya serikali. Bado lengo lake litakuwa limetimia. Na kwa nini hakufanya hivyo tangu mwanzo? Jiulize kwa nini mwanzoni alikataa katakata kuwa sio yake wala hana habari nayo? Kwa nini alitaka yaingie kimya kimya? Na yangeingia kimya kimya, nani angejua kuwa Makonda kaagiza vitu vya bilioni 2 lakini kagawa vitu vya milioni kumi tu kwa shule mbili au tatu? Sidhani tumefikia hatua ya kuaminiana kiasi hicho.