Tafsiri isiyo rasmi
Hofu imewakumba wazazi na jamaa za vijana watano ambao wameripotiwa kutoweka kwa zaidi ya wiki tatu sasa. Vijana hao watano wanaotajwa kuwa ni wafanyabiashara wa Kariakoo, walitoweka tangu Desemba 26 walipotoka kwenye sherehe za ufukweni Kigamboni.
Baadhi ya ndugu walisema walipata mawasiliano ya mwisho kutoka kwa vijana hao kuwa wamekamatwa na polisi lakini hadi sasa ni kitendawili waliko. "Tumetembelea vituo mbalimbali vya polisi, hospitali na hata vyumba vya kuhifadhia maiti lakini hatujapata fununu bado," alisema Bw Longili Martin, baba wa mmoja wa vijana hao waliotoweka. “Ninapozungumza na wewe, nimekuwa tu kwenye vituo vya Polisi vya Msimbazi na Central kuona kama kuna maendeleo. Kwa bahati mbaya, hakuna. Polisi wanasema tu kwamba wanachunguza,” alisema.
Bw Martin, mkazi wa Gongolamboto alieleza kuwa mara ya mwisho aliwasiliana na mtoto wake Edwin Kunambi mnamo Desemba 23, alipomwalika mtoto huyo kwenye sherehe za Krismasi. Kulingana naye, Edwin alimwambia kwamba hatajiunga na familia hiyo kwa sababu atakuwa na shughuli nyingi na akaahidi kujumuika nao Siku ya Mwaka Mpya. Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Jumamane Muliro, alisema anafahamu kupotea kwa vijana hao na kwa sasa polisi wanaendelea na uchunguzi wa suala hilo. Alikanusha madai kuwa wamewakamata wanaume hao ambao sasa wanawatafuta.
Baadhi ya wanafamilia wametoa taarifa polisi na tunasema si kila mtu aliyepotea anakamatwa na polisi. Sio kila mtu aliyepotea amekufa, mara kadhaa watoto hupotea na hupatikana mahali pengine…. Kwa hiyo mtu anapopotea watu wawe na subira,” alisema. Kwa mujibu wake, alipokuwa RPC wa Shinyanga na Mwanza, karibu kila siku watu walikuwa wakienda migodini, wanakaa huko kwa muda wa miezi sita na kurudi baada ya kushindwa kupata walichotarajia. "Polisi wanapowakamata watu, kwa kawaida tunatangaza ili wanafamilia wafahamu waliko," alisema.
Bi Sylvia Quentin, jamaa wa mmoja wa vijana waliopotea aitwaye Tawfiq Mohamed, alisisitiza kuwa wametembelea kila kituo cha polisi, hospitali na chumba cha kuhifadhia maiti zaidi ya mara mbili, lakini yote yameambulia patupu. "Hatuwezi kuendelea hivi, leo tunapanga kuandamana kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na kuona jinsi gani anaweza kutusaidia," alisema. Bi Tabu Saidi aliiambia The Citizen kuwa mtoto wake Rajab Mdoe alikwenda nyumbani kwake Kinyerezi Desemba 26, akaomba gari ili aende ufukweni wa Kingamboni na marafiki zake kwa tafrija.
“Nakumbuka ilikuwa majira ya saa 2 mchana, alikuja na kuchukua gari. Ilipofika saa sita usiku, niliamua kumpigia simu lakini simu yake iliita bila kupokelewa. Haikunisumbua, kwa sababu nilijua atarudi lakini nilitilia shaka baada ya kutorudi hadi asubuhi,” alisema. Kulingana naye, alijaribu kupiga simu yake asubuhi na kwa bahati mbaya, haikupatikana. Aliongeza kuwa mnamo Desemba 27, marafiki wawili wa mwanawe walikwenda nyumbani kwake, kuarifu kwamba mwanawe alikuwa amekamatwa na polisi walipokuwa wakienda ufukweni.
"Nimeripoti suala hilo katika vituo vya polisi, nimepitia hospitali zote na vyumba vya kuhifadhia maiti lakini hakuna fununu," alisema, akiongeza kuwa hana la kufanya.