Ni jioni iliyogubikwa na utulivu, ambao katika maeneo haya ya Kinondoni Makaburini, haujapata kutokea kwa siku nyingi. Kelele za wapiga debe za Posta wa haraka!!!! zilizoeleka kusikika, leo hii hazipo.
Kwa ufupi ni kwamba hata daladala za Posta-M/nyamala au kinyume chake leo hazipiti katika njia hii. Japokuwa sina uhakika kama kuna askari wa Traffic anayezielekeza njia mbadala.
Waombolezaji ni wengi sana wenye nyuso zenye vionjo na hisia tofauti kulingana na jinsi walivyoguswa na msiba huu ambao mahudhurio yake hayajashuhudiwa katika siku za hivi karibuni.
Licha ya wingi wa waombolezaji, ni sauti moja tu inayosikika katika eneo hili.
"Sasa tukio linalofuata ni kuweka mchanga kwenye kaburi la marehemu ambapo wataanza viongozi mashuhuri" Ilisikika sauti ya MC wa mazishi hayo ambayo inaonekana ni ya mtu mkubwa sana kama siyo Kigogo (simaanishi lugha ya kabila fulani).
Licha ya kuwa si mhudhuriaji mzuri wa misiba ambayo haitokei mtaani kwetu Kwa Mnyamani na maeneo ya jirani, lakini kwa msiba huu nimeshawishika kuahirisha safari yangu ya kwenda kwenye ufukwe wa Salender Bridge kuokota Simbi, ili niweze kushuhudia namna misiba ya Watu Maarufu kama huu inavyofanyika.
Najitahidi kupenya taratibu ili japo nipate fursa kushuhudia kinachofanyika pale kaburini lakini nashtuka kukutana na kundi la watu waliyovaa kaunda suti na miwani myeusi waliotanda kama mita Ishirini kutoka lilipo kaburi ambao badala ya kutazama kwenye tukio, wao wameelekea walipo watu.
Wakati, nashangaa na kutafakari nikahisi wote wananiangalia labda kutokana na mavazi niliyovaa, Nikajisemea mwenyewe, "Hata hapa panatosha" kisha nikatulia.
"Sasa ni zamu ya Ndugu jamaa na marafiki wa Marehemu" Ilisikika tena sauti ya yule MC, ambayo kwa sasa ilikuwa ikisika kwa karibu zaidi kutokana na umbali niliyokuwepo.
"Atakayeanza ni Chiefmtz, rafiki wa damu wa marehemu" MC aliendelea.
Watu wote waliokuwa karibu walikuwa wakiangalia huku na kule kwa shauku ya kumuona huyu rafiki wa damu wa marehemu, aliyepewa heshima ya kuweka mchanga.
Kwa utulivu wa kimsibamsiba, akatokea Bwana mmoja akipenya kati ya waombolezaji na kuelekea lilipo kaburi huku akisindikizwa na macho ya waombolezaji. Mmoja wa vijana wenye suti nyeupe, kati ya vijana waliokuwa waliokuwa wakitoa huduma pale, alikuwa ameshikilia Koleo lenye mchanga akimsubiri Chiefmtz achukue mchanga kidogo kama ilivyozoeleka, kwa ajili ya kutupia kaburini.
Kwa utulivu, huku akifuta machozi kwa kitambaa cha mkononi, Bw, yule alichukua lile koleo alilokuwa ameshika yule kijana na kumwaga ule mchanga wote kaburini.
Kama mtu asiyeamini alichokiona akasema kwa sauti kavu na ya kujiamini,
" Babaangu Balali! Hivi ni kweli umekufa aati!! Nimekumwagia beleshi zima la
mchanga ili uamke uturudishie hela zetu za EPA, mbona husikii"
Huku waombolezaji wakiwa wamepigwa butwaa na yaliyokuwa yakijiri, yule Bwana akachota mchanga mwingine, ukiwa mwingi zaidi wenye mabongemabonge na kuumwaga tena kwa nguvu zaidi na kutoa kishindo "Puuuuuuu!!!!!!!! huku akiendelea kusema
"Nakumwagia mchanga mwingine tena, yaani unajifanya umekufa kabla
hujaturudishia hela zetu za EPA"
Ikasikika sauti ya MC, "Mtoeni huyo, atakuwa amechanganyikiwa!!!!!"
Wale vijana wenye suti wakamuondoa kwa haraka ili kupisha wengine.
Kwa niliyoyaona, nikajikuta huku nikiondoka, naguna "He!!! KUMBE NI BALALI YULE ALIYESHIRIKIANA NA WENZAKE KUTUPORA HELA ZETU? Nikajilaumu sana kwa kuacha shughuli zangu. Hata hivyo nikaishia kusema
BWANA AMETWAA!!!!!