Makala ya Raia Mwema lina habari ya kufikirisha kidogo:
Mwandishi anauliza " Diamond ana fedha, lakini anauza nini?"
Hata mimi nimejikuta nikiuliza swali hili mara nyingi tu bila majibu. Wengine wanasema anauza matangazo, wengine ana studio nk. Lakini vipi ile biashara yake ya msingi : Muziki?
soma mwenyewe hapa chini:
Diamond ana fedha, lakini anauza nini?
SEP 29, 2016
by MWANDISHI WETUin BURUDANI & MICHEZO
NASEEB ABDUL ‘Diamond Platnumz’ ananivutia sana miongoni mwa wasanii wa muziki wa nyumbani. Ananivutia kumsikiliza na kumtazama kwenye TV.
Akiwa ananengua jukwaani unaweza kujisemea kwanini asiwe ananengua na aachache na kuimba. Akianza kuimba bado utajisemea tena kwanini asiwe anaimba pekee na si kuchanganya vitu viwili kwa wakati mmoja?
Huyu ndiye Diamond ambaye anafanya vitu viwili kwa wakati mmoja na kuvutia wengi. Wapo wanaompenda kwa kuimba na wako wanaompenda kwa kucheza.
Amejivutia mashabiki wengi kwenye maeneo hayo mawili jukwaani. Kazi zake zimemfanya hivi sasa atajwe kama msanii anayetengeneza fedha nyingi zaidi hapa nchini.
Wingi wa fedha hizo zimefanya afungue kampuni ya WCB, inayofanya kazi za kusimamia wasanii mbalimbali.
Lakini mpaka unapoweka umakini wako kusoma andiko hili, fahamu Diamond amewahi kutoa albamu moja tu ya Nenda Kamwambie mwaka 2009.
Hii ni albamu yake ya kwanza na ya mwisho mpaka wakati huu 2016. Ni takribani miaka saba sasa imepita tangu atoe albamu hiyo ambayo haikuwa na idadi kamili ya nakala alizouza.
Inakuwaje Diamond, anayetajwa kuwa msanii mwenye fedha nyingi, awe ametoa albamu moja tu kwa zaidi ya miaka saba?
Ina maana Nenda Kamwambie ndio imemlipa kiasi hiki mpaka sasa aamue asitoe albamu nyingine?
Wanamuziki, bendi na vikundi duniani kote wanaonyesha na kutangaza utajiri wao kupitia mauzo ya kazi zao ambazo zinakuwa albamu.
Hata Ali Kiba, anayekinzana naye kimuziki aliwahi kusema albamu yake ya kwanza ya Cinderella ilivunja rekodi na kuuza ‘double platinum’ kwa kuuza nakala milioni mbili.
Mauzo ya nakala hiyo anadai yalimuingizia shilingi milioni 200. Kiba aliwahi kusema hata ukimya wake kwenye sanaa haukumfanya apumzika bure, bali alikuwa na ‘jembe’ lililofanya akae pembeni kidogo.
Kwenye dunia ya sasa, wasanii wa muziki wanayo nafasi ya kulipwa au kujiingizia pesa kutokana na vyanzo mbalimbali na hiyo yote ni kutokana na muziki wao na ndiyo maana sio kitu kigeni tena kuona msanii analipwa pale nyimbo zake zinapochezwa redioni.
Hii ni sheria inayotumika kwa baadhi ya nchi duniani, japo nyumbani haijaanza kutumika. Inawezekana sheria hii ingekuwepo nyumbani Diamond, angeingiza fedha zaidi.
Swali kubwa ambalo nimekuwa nikijiuliza ni hili; Diamond na wasanii wetu wengine ambao hawajawahi kutoa albamu wanapata wapi fedha za kuendeshea maisha yao ya kifahari wakati mauzo ya albamu zao ni sifuri?
Biashara ya muziki ni sawa na nyingine yoyote iwe ya kuuza barafu, mikate, machungwa au magari. Mfanyabiashara wa magari, hesabu yake hutokana na idadi ya magari anayouza. Vivyo hivyo kwa biashara nyingine.
Hawa wasanii wetu ambao hawauzi muziki, wanapata wapi fedha za kuendeshea maisha yao? Muziki bila kutoa albamu ni biashara gani?
Nafahamu kuna maonyesho mbalimbali ambayo baadhi yao wana