Habari inayo-trend sana kwenye mitandao ya kijamii hivi sasa ni kauli aliyoitoa Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, kuwa wao wanaendelea kubaki madarakani kutokana na kutumia vyombo vya dola
Katika maelezo yake aliyoyatoa kwenye luninga ya ITV siku chache zilizopita, aleleza kuwa chama cha KANU cha Kenya na UNIP ya Zambia, kuwa waliondolewa madarakani, kutokana na viongozi wake kufanya uzembe wa hali ya juu, kwa kutoweza kutumia vyombo "vyake" vya dola kuendelea kubaki madarakani!
Hivi kwenye nchi yoyote inayoendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, si kwa kutumia kura za wananchi, kupitia sanduku la kura, ndivyo vinavyoendelea kukibakiza chama kilchoko madarakani?
Sasa inakuwaje Katibu Mkuu wa CCM atamke hadharani kuwa chama chake, kinatumia nguvu za vyombo vya dola, kukibakisha madarakani?
Huo ndiyo ninaouita ulevi wa madaraka uliopindukia, alioufanya Katibu Mkuu huyo wa CCM.
Hivi anajua alichotamka ni kinyume cha Katiba yetu ya nchi, ambayo kwenye ibara ya 3(1) inatamka wazi kuwa nchi yetu itakuwa ni ya mfumo wa vyama vingi?
Kumbe mateso yote wanayopitia viongozi wetu wa vyama vya siasa vya upinzani yanatokana na chama cha CCM kutumia madaraka yake vibaya, kwa kuviagiza vyombo vya dola, kuwashughulikia viongozi hao wa upinzani?
Ninachofahamu ni kuwa Katibu huyo Mkuu amefikia kiwango hicho cha ulevi wa madaraka, kwa kuamini kuwa hakuna chombo chochote hapa nchini kinachoweza kumchukulia hatua, za uvunjifu wa waziwazi Katiba yetu ya nchi, kutokana na ubovu wa Katiba yetu ya nchi, ambayo imempa mamlaka ya ki-mungu mtu, Rais wa nchi hii, ambaye pia ndiyo kiongozi wa chama kilichoko madarakani cha CCM, ambaye ndiye "engineer" wa kuvitumia vyombo vya dola, kukandamiza demokrasia hapa nchini
Naamini kabisa, kauli hiyo inatosha kabisa kuifikisha CCM kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya The Hague, ili waweze kujibu mashitaka, ni kwa vipi wao watumie vyombo vya dola, ili waendelee kubaki madarakani.