Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho hakiwezi kuvumilia matukio ya utekaji na uvunjifu wa amani na hakitakubali.
Mbali na hilo, Dk Nchimbi ametaka vyama vya upinzani ikiwemo Chadema kuungana pamoja kukemea, kukataa kufarakanishwa juu ya matukio ya utekaji na amepuuza taarifa za mitandaoni zinazolenga kuwahusisha viongozi wa Chadema na utekaji, mauaji.
Pia, CCM imelaani tukio la kutekwa na kuuawa kwa Mjumbe wa Sekeretarieti ya Chadema, Ali Kibao kikisisitiza hilo halikubaliki.
Kibao alitekwa Septemba 6, 2024 na watu wenye silaha eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa kwenye basi la Tashriff akienda nyumbani kwake mkoani Tanga.
Mwili wake uliokotwa siku iliyofuata eneo la Ununio, Dar es Salaam ukiwa umeharibika na inaelezwa uso wake ulimwagiwa tindikali.
"Mtu yoyote anayehatarisha usalama wa raia, anayeteka raia au kikundi chochote kinachohatarisha usalama kinaharibu taswira ya CCM," amesema.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Ijumaa, Septemba 13, 2024 alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari, ofisi ndogo za CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Katika maelezo yake Dk Nchimbi amesema: "Tumemsikia Mwenyekiti wa Chadema, (Freeman) Mbowe akitoa mwelekeo wa chama chake kuwa kitachukua hatua. Nikiri Mbowe ni rafiki yangu, lakini Mbowe amefikishwa hapo na genge la utekaji?"
Dk Nchimbi amesema amekutana na Mbowe hivi karibuni katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi, Bakari Machumu: "Na Mbowe alinieleza juu ya suala la Kibao, kwa kumtazama Mbowe hahusiki na tukio hili la utekaji."