Dkt. Wilbert Kleruu - Utata wa kifo chake, historia na maisha yake

Dkt. Wilbert Kleruu - Utata wa kifo chake, historia na maisha yake

Ndugu zangu,
Naendelea na mazungumzo yangu na Mzee Omary Nzowa anayeonekana pichani.
18057875_10211131059005109_2033512247540425340_n.jpg
Swali:- Je unafikiri kwanini Dk. Kleruu alipata tabu sana kufanya kazi na watu wa Iringa?
” Mi nadhani Kleruu, kwa jinsi alivyokuwa, angepata tabu kufanya kazi mahali po pote pale. Tatizo ni ile hali ya kutanguliza ubwana na kuwadharau wananchi.
Hakika, wakati ule Mwalimu Julius Nyerere alipata tabu sana na namna ya ku-deal na viongozi kama akina Kleruu. Kumbuka ,Tanzania kama nchi ilikuwa taifa changa sana. Hatukuwa na wasomi wengi. Nilimfahamu Nyerere, hili la Kleruu lilimsumbua sana Mwalimu.
”Nikwambie Maggid, Ujamaa na Kujitegemea kama itikadi na sera za Mwalimu haukuwa tatizo. Tatizo lilikuwa kwa baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya utekelezaji.
Hawa hawakuwa wanasiasa, wakati mwingine walionekana kama Wanyapara. Mwalimu wakati ule hakujua kila kitu kuhusu watu aliowateua kumsaidia.
”Ni kweli Mwalimu alitia saini hukumu ya kunyongwa kwa Mwamwindi. Naamini hakufurahia, bali hali ya wakati ule ilimlazimisha kufanya vile.
”Sisi tuliomfahamu Mwalimu tunajua kuwa hukumu ile ni moja ya maamuzi magumu yaliyomsononesha sana Mwalimu. Unajua wakati ule kuna Wakuu wa Mikoa waliojenga hoja, kuwa kama Mwamwindi kwa tendo lile asingepata adhabu ile, basi utendaji wao wa kazi mikoani ungekuwa mgumu.
Ndiyo, hoja hizo ziliibuka. Kwa kiongozi wa nchi ni mtihani. Siyasemi haya kumtetea Mwalimu bali ni kutambua ukweli kuwa Mwalimu alikuwa ni binadamu kama wewe na mimi.”
Swali: Unasema ulimfahamu Nyerere na kwamba unaamini kwa wakati ule tatizo kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa kwa baadhi ya aliowapa dhamana ya kumsaidia katika utekelezaji. Je, Mwalimu aliwahi kulizungumza jambo hili nawe ukamsikia?
”Huo ndio ukweli. Mimi nimekuwa katika chama (TANU) tangu mwaka 1956. Kadi yangu ya uanachama wa TANU niliikatia Mbeya. Ni Nyerere mwenyewe, kwa mkono wake, pale Mbeya, mwaka 1956 alinijazia kadi yangu ya TANU. Alianza na Kanali Ayoub Simba ikaja ya kwangu.
”Hata leo, ukiangalia namba za kadi ya TANU ya Kanali Ayoub Simba na ya kwangu zinafuatana. Tulikuwa bado vijana sana, na Mwalimu alifanya mwenyewe kazi ya kuhamasisha vijana kuingia TANU. Mwenzangu Ayoub yeye akaja akaingia jeshini , akafikia mpaka cheo cha ukanali, akawa mbunge pia, kule Mafia. Yule ni kada wa siku nyingi.
”Sasa nimepata kumsikia Mwalimu akiongea kuhusu hili la uongozi? Kwa kweli si mara moja. Nimemsikia Mwalimu akitamka, kuwa njia iliyo nzuri sana ya kumsaidia katika uongozi wake ni kwa tulio karibu na watu kumwambia moja kwa moja juu ya mazuri na mabaya wanayofanya wateule wake.
”Kwamba ni hatari wananchi wakianza ama kuchoka kulalamika au kuwaogopa viongozi wao. Unajua Mwalimu hakuishia tu kutumia watu wa Usalama wa Taifa, aliwatumia pia watu wa kawaida kupata taarifa sahihi.
Swali: Turudi kwenye kilichotokea kijijini Mkungugu, siku ya Krismasi, Desemba 25, 1971. Inasemekana kulikuwa na mtikisiko mkubwa hapa Iringa baada ya Dk.Kleruu kupigwa risasi na Mwamwindi. Je, hali ilikuwaje hasa?
” Ni sahihi, hali ilikuwa ngumu. Wengi tuliathirika na mkasa ule, kwa namna moja au nyingine. Unajua ilifika mahali wakati ule mtu ukigongewa mlango usiku, basi, unavaa kabisa, shati, suruali na viatu, maana huenda ukifungua mlango usirudi tena kitandani kwako!”
Swali: Hivi Iringa ya wakati ule ilionekanaje, unakumbuka?
” Mji huu wa Iringa ulikuwa mdogo sana. Wengi tulikuwa tunajuana. Hebu ngoja nipekue kwenye kabati langu kuona kama nina picha za zamani”.
Mzee Nzowa anainuka kitini. Anakwenda kupekua picha za zamani. Nasubiri kwa shauku.
Mzee Nzowa anapekua kabati lake huku akinismulia kisa cha vijana wa mjini Iringa wakati huo, waliotaka kumwonyesha Julius Nyerere, kuwa RC wake aliyemleta Iringa ana mambo ya hovyo.
Kwa vile RC Kleruu alikuwa pia ni mtu wa moja moto moja baridi, basi, jioni moja vijana wa mjini wakamtafutia RC mtego wa wasichana warembo wa mjini kunywa nae.
Kilichotokea , asubuhi RC hakuonekana Ikulu Ndogo. Katika tafuta tafuta ya RC, akaonekana asubuhi hiyo, chini ya gari lake, eneo la Mshindo, Iringa. Ananisimulia Mzee Omary Nzowa.
Mzee Nzowa ananiambia, jaribio hilo lilikuwa njia ya kumshinikiza Julius Nyerere amuondoe RC Dr Kleruu, mkoani kwao.
Narudi tena kwa Amani Mwamwindi anayenieleza alichoambiwa na baba yake Said Mwamwindi, mara ile Mkulima Said Mwamwindi alipotoka kwenye mkutano kati ya RC Dr Kleruu na wakulima uliofanyika ukumbi wa Welfare, Iringa.
Ni siku chache kabla ya tukio la Desemba 25, 1971.
Itaendelea kesho...
 
Tunahitaji watu wengi wenye moyo wa Mzee Mwamwindi maana hawa wakuu wa mikoa wajinga wajinga wameongezeka sana....
 
KIFO CHA MKUU WA MKOA WA IRINGA.

Na: Noel Shao.

Ilikuwa siku ya sikuku ya Noel au Christmas mnamo mwaka 1971. Mkuu mpya wa Mkoa wa IRINGA aliye hamishiwa hapo akitokea Mtwara Dr. Wilbert Kleruu, msomi wa shahada ya uzamivu wa uchumi wa kijamaa katika kilimo.

Kipindi hicho Kulikuwa na kampeni ya kutaifisha mashamba ya wakulima wakubwa na kuyafanya mashamba ya kijiji. Na Dr Kleruu alipelekwa Iringa ili akatekeleze kaz hiyo kwani kipindi hicho iringa ilikuwa na wafanya biashara wakubwa walio miliki mashamba makubwa ya kilimo hasa maeneo ya Isimani.

Katika Eneo hilo la Isimani Kulikuwa na mkulima mmoja aliye kuwa ana miliki Takribani hekari 400 za mashamba na mfanyabiashara aliye kuwa ana miliki majumba iringa mjini - Said Mwamwindi.
Kwa wakati, ule ilishauriwa angalau kila mtu awe na shamba lisilo zidi hekari 4. Jambo ambalo lilileta mvutano Mkubwa kati ya wakulima wakubwa na Serikali.

Sasa, siku hiyo ya Christmas Dr. Kleruu alikwenda Isimani akiwa katika utekelezaji wa sera ya kutaifisha mashamba. Moja kwa moja alikwenda hadi shambani kwa Mwamwindi, na kumkuta analima.

Mkuu wa Mkoa akamuuliza mbona unalima shamba lako mwenyewe na si la kijiji? Mwamwindi akajibu, sioni tatizo hakuna mtu shambani, Leo ni jumapli tena ni sikuku

Maneno Yale yalimuudhi Dr Kleruu, ambaye alikuwa akisifika kwa ukali, kutekeleza sera za serikali, na maneno makali au kutukana watu hadharani pale wanapo fanya makosa.

Dr. Kleruu baada ya kuudhika inasemekana alimtukana Mwamwindi tusi lililo mlenga mama yake ambaye tayari alikuwa amesha kufariki siku nyingi.

Mwamwindi alihoji inakuwaje ana mtukania mama yake, huku akimuonyesha kaburi alimo zikwa.

Ilisadikiwa, Mkuu wa Mkoa aliendelea kuja juu, huku akisema kaburi ndio nini? Huku akilipiga mateke kaburi la Mama yake Mwamwindi.

Na ifahamike kwa kabila la wahehe makaburini yana heshima yake, Kwani ndipo nyakati nyingine hutumika katika Sala, matambiko na mila kadha,.

Kitendo kile kilimgadhabisha Mwamwindi, na kuanza kukimbia kuelekea nyumbani. Mkuu wa Mkoa akadhani Mwamwindi ana mkimbia, akaamua kumfuata hadi nyumbani.

Alipo fika nyumbani, tayari Mwamwindi alisha ingia ndani na kuchukua bunduki yake, Dr. Kleruu baada ya kuona hali ile mara moja alianza kumuomba msamaha, Lakini hasira zilimuwaka Mwamwindi kama moto wa nyika, hakuwa na msamaha, alimfyetulia risasi Dr Kleruu na kumuua

Baada ya kumuua, Mwamwindi aliuchukua mwili ya Mkuu w mkoa na kuuweka ndani y gari (seat ya nyuma) alilo kuja nalo Mkuu huyo wa Mkoa, gari aina ya Peugeot.

Baada ya hapo alichukua kofia ya Dr Kleruu na kuivaa, kisha akiingia ndani ya gari na kuanza safari ya kuelekea iringa mjini. Tena akipita njia isiyo ruhusiwa kwani barabara ilikuwa 'one way'

Alipo karibia mjini, Askari walishangaa ni nani anaye pita njia isiyo ruhusiwa, ila mara waligundua ilikuwa gari y RC wa iringa, hivyo walidhani amepata dharura.

Gari ilipo wasilini kituoni, polisi walijiandaa kupiga salute, mara alishuka Mwamwindi akiwa na bunduki yake na kuelekea ndani (counter). Askari walipigwa na butwaa.

Alipo fika aliwaambia "nendeni mkachukue Nguruwe wenu ndani y gari," na Kisha akakabidhi bunduki yake.

Lilikuwa tukio la kuajabisha, na kushangaza na lililo fanyika kwa haraka sana.

Baada ya taarifa kuenea, msako wa polisi ulianza mara moja. Msiba wa Dr. Kleruu ulikuwa pigo kwa wakulima wadogo,walio sikitika kwa kifo hicho.

Ila katika msako huo, polisi waliwakamata baadhi ya watu walio kuwa wakinywa bia kwa furaha, shangwe na nderemo baada ya kusikia Dr Kleruu ameuawa. Kwani wanadai alikuwa na dharau,.

Kesi ya Mwamwindi alipelekwa haraka sana,. Na ndani ya miezi kadhaa, June 1972, Mwamwindi alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, ikiwa ni moja ya hukumu chache za kunyongwa zilizo wahi kuidhinishwa. Huo ndio ukawa mwisho wa tajiri na mkulima mkubwa, Saidi Mwamwindi.

#NB I stand to be corrected.

Noel C S.
 
Hadithi ina mafundisho mengi hasa kwa viongozi wachache wa awamu hii waliojaa kiburi dharau na kujisikia sana. Bashite, na yule wa Arusha! Dunia inazunguka.
 
sina hakika na simulizi yako kwani ipo kama ya kusadikika kiasi fullani.....mkuu huyo wa mkoa alikuwa anatembea peke yake kiasi cha bw. mwamwindi kuweza kuchukua gari yake baada ya kumuua?!!!
 
KIUFUPI DR. KLERUU ALIJITAKIA MWENYEWE KIFO NA HUYO MWAMWINDI KESI YAKE ILIENDESHWA KISIASA KWA 7BU NI WAZ KUWA RC ALIMCHOKOZA HUYO MKULIMA KWA KIWANGO KILICHOPITILIZA.. RC UNAVUNJA PROTOKALI UNAENDA KUGOMBANA NA MKULIMA SHAMBAN UNATEGEMEA KTATOKEA NIN? TENA UNAKWENDA SKU YA SKUKUU, GARI UNAENDESHA MWENYEW, HUTOI TAARIFA,
MIMI NINGEJITETEA KUWA HUYU JAMAA LICHA YA KUNITUKANA ALIANZA KUNISHAMBULIA IKANIBID NIJIHAMI, EBO!
 
Dr. Kleruu. Nilisikia historia yake kwa mara ya kwanza kupitia wimbo wa. Hayati Mbaraka. mwinshehe.
 
sina hakika na simulizi yako kwani ipo kama ya kusadikika kiasi fullani.....mkuu huyo wa mkoa alikuwa anatembea peke yake kiasi cha bw. mwamwindi kuweza kuchukua gari yake baada ya kumuua?!!!

Inawezekana alikuwa anamchukua mmoja wa wake za mwamwindi. Alikwenda peke yake bila walizi kula mzigo akijua mwamwindi alikuwa safari. Ndiyo sababu mwamwindi alikasirika. Isingekuwa rahisi mtu upinge amri ya Nyerere na TANU enzi hizo.
 
Nilikua hata sijazaliwa kipindi cha hii tukio but kwa maelekezo yote huyu Kleruu alipaswa kufa kabisa, inaonekana ni mnyanyasaji wa raia na alivimbiwa na madaraka, alikua na dharau, visa vyote vinaonekana alimuattack Mzee Mwinyi personal ingawa visa haviko wazi sana...huyu Mwinyi hata mm namuona shujaa hakustahili kunyongwa labda kifungo tu but ndo ivo zilidumu zile fikra za mshika chaki...Lukuvi na wenzake wenye tabia za namna hii na ma dc wenye ukleruu wajifunze
 
Mzee Mwamwindi alikuwa mchapa kazi na mkulima mwafrika mzawa,lakini serikali ya ujamaa haikuwa na huruma kwa mtu alieenda kinyume na matakwa ya watu kama Kleruu.
Mwamwindi alinyongwa baada ya Mwl Nyerere kutia sahihi,lakini sera na siasa ya ujamaa zilikufa kabisa.
 

UTATA WA KIFO CHA DK. WILBERT KLERUU

Kwanza kabisa nijitambulishe kuwa wakati anauawa mkuu wa mkoa Iringa nilikua kijiji cha Chamndindi ambacho kilipakana na kijiji cha Mkungugu, eneo la tukio la umauti wa aliye kuwa mkuu wa mkoa Iringa. Vilevile nilimtambua Said Abdala Mwamwindi, hata kama wakati anamua Kleruu nilikuwa na umri wa miaka kumi na tano, bado nina kumbukumbu ya kumwona marakadhaa akipita katika kijiji cha Ikengeza akielekea kijiji cha Manyanambo ambako naamini alikuwa na mashamba.

Aidha nakumbuka kuwa katika msiba wa mama mkwe wa dada yangu ambaye alifariki kwa ajari ya gari aina ya basi hapo tarehe 27 septemba, 1971, Mwamwindi ndiye aliye fanikisha upatikanaji wa maji katika msiba kwa kutumia gari lake. Sina kumbukumbu ya moja kwa moja juu ya udugu kati ya Mwamwindi na mama mkwe wa dada, lakini kunaukweli wa kuwepo undugu.

Ninacho kumbuka katika msiba ule, palitawaliwa mazungumzo yaliyo husu ukali wa mkuu wa mkoa ambaye hata mimi nilishuhudia alipo fika nyumbani petu, alitoa maagizo ya kugawa ngo’mbe na shamba letu ambalo baba yetu alilikuta pori, akapambana na nyoka na wanyama wakali wa kila aina wakati wakusafisha. Bila hofu na kwa kujiamini alipoambiwa shamba lile lilikuwa na ukubwa wa ekari sita, alisema litagawanywa katikati ili kwamba eneo jingine liwe mali ya umma, na ngo’mbe vivyo.

Mazungumzo yaliendelea siku ya arobaini ya msiba ambapo ilidaiwa Mwamwindi alisema maneno makali sana kuhusiana na mkuu wa mkoa, lakini kaka yake aliye ishi kijiji cha ikengeza alimkemea kwa kuhofia uwepo wa wapambe wa mkuu wa mkoa ambao alihisi wangepeleka maneno, hasa wale waliokuwa na nafasi katika halmashauri za vijiji. Mazungumzo yaliyo tawala katika siku ile ya arobaini, ni pamoja na kukebehi imani za dini kama vile kuhoji, padre asipo shiriki kupanda shamba la ujamaa, angetelemka Mungu kupanda?

Wengine walisema tajiri mkubwa wa wakati ule aliyejulikana kwa jina la Abdalah Mwangubi, alipelekwa mchaka mchaka kwenda kulima shamba la ujamaa, akiwa amevaa taulo kiunoni, ikimaanisha alimfuata nyumbani mapema alfajiri na hakumpa hata nafasi ya kuvaa nguo. Wengine walisema alimburuza ardhini shekh wa msikiti wa Nyang’olo, kisa hakwenda kulima shamba la ujamaa, huku wengine wakisema akiulizwa swali asilo lipenda alimtukana muuliza swali kisha kufuta mdomo kwa kitambaa cheupe sana.


Hayo ndiyo yaliyo tawala katika enzi hizo za uongozi wa mjamaa na msomi aliyebobea kwa sayansi ya uchumi wa kilimo yaani Dk. Kleruu. Wenye kukifahamu kisa hiki vizuri ni wale walio kuwepo Ismani wakati ule na wanao fuatilia mambo kwa kina.

Baada ya utangulizi huo, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mjengwa namna alivyoanzicha mjadala huu ambao kwangu mimi ameuleta katika muda mwafaka. Ninasema hivyo kwasababu wale waliokuwa vijana wa wakati huo ndiyo wazee wa leo napengine wengi wao wako mautini, kama ambavyo hata waliokuwa watoto wakati huo, leo wanabisha hodi kwenye lango la uzee.

Jambo la kwanza, nataka niseme, tuwatendee haki marehemu wote wawili kwa kuepuka kukwepa ukweli wa tuklio lile, nikianza na Kleruu; Hakuna ubishi kwamba siasa ya ujamaa na kujitegemea nikinyume cha mfumo wa siasa ya ubepari au aina yoyote ya maisha yanayoweza kuhalalisha ubaguzi wa kipato.

Mlengo huo wa siasa ya ujamaa unaamini kuwa, ubepari ni unyonyaji kwa maana ya mfumo unao ruhusu wachache kujilimbikizia hata kama wasio nacho watavuja jasho bila kujali,pengine maisha yao ni duni tena ya kutabika. Kinyume chake kilipelekea siasa ya ujamaa kuhalalisha unyang’anyi kwa kigezo cha kuziweka njia kuu za uchumi mikononi mwa umma.


Serikali ya wakati huo iliendeleza ubabe dhidi ya wenye nacho, kufuatia Azimio la Arusha wenye kumiliki mali walipewa majina ya dhihaka kama vile makupe, wanyonyaji na kadhalika. Haikuwa ajabu kwa wageni kuikimbia nchi na kuacha majumba yao yakinyang’anywa na kuandikwa msajili. Ukawa wakati wa dhiki kuu kwa matajiri, walikimbia huku na kule, wengine wakasalimisha mashamba yao bila shuruti.

Hata hivyo, historia inaonesha hakuna tofauti kubwa kati ya siasa ya ujamaa na ile ya kikoministi, jambo ambalo tunaweza kuamini mauaji ya watu katika mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917 na mwendelezo wa mauaji katika utawala wa kikoministi,inajieleza wazi kuwa msingi wa siasa za aina hii ni mauaji. Hata kama hiyo haitoshi, mauaji yaliyo tokea China hayatenganishwi na usimikwaji wa siasa za kikominisi zilizo kumbatiwa na chama cha kikoministi, chini ya mwenyekiti. Mao T-se-tung.

Katika kusema hivyo, marehemu Kleruu alikuwa katika kusimamia ujenzi wa misingi ya ujamaa, yeye akiwa stadi, kazi hiyo aliielewa vema, kwamba, hakukua na salia mtume kwa matajiri katika ujenzi huo. Lakini aliyekuwa rais wa nchi wakati huo mwalimu hayati, Julius Nyerere alisahau au alidhani angekuwa na njia nyingine ya kufikia ujamaa, japo hakutabirika alimanisha nini, mteule wake alipuliza filimbi na kuingia kwenye midani ya vita peke yake.

Kama hayati, Julius Nyerere angelifahamu hilo, Kleruu asinge achwa pekeyake katika kutekeleza zoezi lile. Aidha kungekuwa na uwezekano wa kuwepo nguvu kubwa hata kama haikuwa njia sahihi ya kuwakabili matajiri wa wakati ule, jambo ambalo huenda watu kama Mwamwindi wangekuwa walikwisha kupunguzwa makali ya ubabe walio kuwa nao.

Ninaamini wapo wanyonge waliokuwa chini ya watu wa aina ya Mwamwindi ambao walikiona cha mtemakuni kupitia makali ya ubabe, kiasi cha kuwapa hofu ili wasidai stahiki zao. Fikiria ujasiri wa kinyama aliofanya mkulima Mwamwindi dhidi ya serikali, sembuse kwa kibarua angeambiwa jambo akamsikiliza? (najaribu kuonesha nguvu mbili hasimu)

Askari aliyekuwpo kituoni siku, Mwamwindi akiukabidhi mwili wa aliyekua mkuu wa mkoa wa Iringa, tarehe 25 disemba, 1971 majira ya jioni, katika utafiti wa Mjengwa anaeleza namna mkuu huyo alivyokataa kwenda na ulinzi wa askari siku hiyo. Maelezo yake yanaleta picha inayo karibiana na ukweli kwamba, kama marehem aliwakamia Rashid Juma na Mwamwindi angeondoka na askari.

Ikumbukwe kuwa alikuwa na mkutano wa dharura na wana kijiji cha Ndolela siku moja kabla ya umauti kumfika, ambapo walikubaliana siku ya krismasi waendelee na kilimo. Siku hiyo mkuu huyo wa mkoa alikuwa na kazi moja ya kuazima matrekta katika vijiji vingine ili kukamilisha malengo yaliyo kusudiwa, ndiyo sababu siku ile kulikuwa na matrekta matano na alikufa akiwa amevaa overroll akimanisha kazi.

Lakini pia kunaukweli kwamba kule ismani kwa wakati ule kulima na kupanda miezi ya kumi na mbili haikuwa vizuri maana mahindi yalitakiwa tarehe 25 yawe yameota, ndivyo wenyeji wenye nia njema walivyo taadharisha. Hivyo basi mkuu wa mkoa katika kuharakisha, alikua miongoni mwa walioendesha matrekta kiasi cha kufanikisha kulima na kupanda ekari stini kwa siku moja.

Tuna kila sababu ya kuamini kuwa kitendo cha Kleruu kumvuruga mkulima Mwamwindi kwa siku ile ilikuwa ajali, jambo ambalo halikupangwa, japo mkuu huyo alimfuata shambani ni baada ya kumuona mkulima huyo akiendelea na kilimo shambani kwake. Nini kilimsibu, inawezekana kitendo cha kumwona kabaila anaendeleza ukabaila na ukupe wake kwa kuwatumikisha watu wanyonge shambani, akiamini ni kwa malipo hafifu, kilimuudhi mjamaa huyu.

Hapo najaribu kufunga milango ya kufikiri kisa hiki kwa namna nyingine kama ambavyo wengi wamekua wakijaribu kuokoteza sababu ya tukio hili. Upande wa Mwamwindi, si jambo jepesi kuambiwa kuanzia sasa robo ya mali zako ni mali ya umma, haijalishi kuwepo faraja ya namna gani bado litakuwa jambo la kuudhi tu.

Mwandishi nilishuhudia shamba kubwa lililokuwa la mkulima mmoja aliyejulikana kwa jina moja Mwatebela, alinyang’anywa likawa shamba la ujamaa la kijiji cha Nyang’olo. Shamba lile lilikuwa kubwa, akivuna mahindi na kukusanya shambani kabla ya kuyaondoa yalikuwa mlima uliokuwa ukionekana umbali mrefu sana.

Ikiwa Mwamwindi naye alinyang’anywa mashamba makubwa aliyogharamia kufyeka, maana mwandishi alishuhudia misitu ilivyo kuwa ya kutisha kule Ismani katika miaka ya 1964. Tuache kulainisha mambo kwa kufikiri tukio hili ni japesi kama wanavyotaka tuamini, lakini Mwamwindi hakuwa mtu wa mambo mepesi kama hayo wanayo taka tuamini.

Mpaka hapo kisa cha tukio lile ni ile hali ya siasa ya ujamaa na kujitegemea kuwa na mlengo wa unyang’anyi kama ilivyoshuhudiwa majumba, shule na mabenk ya watu binafsi na ya taasisi za kidini yakitaifishwa. Unyang’anyi huu ulipata kupigiwa debe na mwana siasa za mageuzi,Karl Marx alisema,“the prolitarians have nothing to lose but their chains”kwa tafsiri isiyo rasimi, anachochea wavuja jasho waungane ili kwamba umoja na uwingi wao wautumie ama kudai usawa au kunyang’anya mali, maana hata ikizuka ghasia wao hakuna walicho miliki ambacho kitaharibiwa, isipo kuwa watapoteza unyonge wao.

Mwisho niwasihi wasomaji wangu, mitazamo yetu isidumae kwa kuwaangalia Mwamwindi na Kleruu kama watu, bali tuone walibeba dhamana ya matabaka mawili hasimu, ambayo nyakati zote huwapoteza watu wasiione. Kwamfano watanzania tuliaminishwa na wanasiasa juu ya ufisadi ulio kithiri katika nchi yetu , ambapo wote tulihamasika kukemea.

Vita hivi ni kati ya tabaka la wenye nacho na la wasio nacho, eneo ambalo Kleruu alisimama upande wa tabaka la wasionacho akitafuta heshima ya utu wa mtu kwa kuwavuruta matajiri bila kujali uwezo wao. Hakuwa mtu wa kujinyenyekeza kwa mabepari na makabaila, akajitoa mhanga kiasi cha kumwaga damu kuliko kuwatumikia wale alioamini kuwa ni wanyonyaji, ambao hata sasa tunawatambua kwa tabia zao kuwalainisha viongozi na wakuu wa idara, ili wazipuuze sheria ambazo ndicho kipimo cha lazima cha usawa.

Ni shujaa aliyeishi kimapinduzi na kutenda kimapinduzi, lakini pia alitamani kuona usawa katika maisha ya watanzania sambamba na mapinduzi ya viwanda. Mboni za macho yake ya kifikra ziliona Tanzania ya kilimo cha viwanda, akianza na ndoto yake ya kilimo cha kutisha, ambacho aliishia kulima na kupanda mbegu ekari stini katika kijiji cha Ndolela.

Nimeshuhudia watoto wakwanza wa marehem hao wakisameana kwa kukumbatiana kama ishara ya umoja, usawa na utulivu, kinyume na kivumbi kilichoshuhudiwa katika mkoa wa Iringa, wakati na baada ya mauaji ya Dk. Kleruu. Kiigizo hiki hakina sura kamili ya tukio lile kutokana na kwamba marehemu wale walibeba dhamana ya mifumo wala sio familia zao kama ambavyo wanatutaka tuamini, labda kwa binasi yao.

Lakini ukweli wa mambo hapatakuwa na usalama, amani, umoja na utulivu wowote chini ya jua mpaka uwiano wa kipato kati ya wamiliki na watenda kazi uwepo. Hatua ambayo inazichomoza sura za marehemu wetu ambao kimsingi bado kila mmoja amelala mauti akiwa na maktaba yake kinzani, ambazo haziwezi kukutanishwa kwa tabasam au machozi ya watoto wao wa kwanza.

Marehem hawa ni watu mhimu kwa uzito mkubwa na kama maono yangeshirikishwa, walipashwa kuwa alama ya taifa, badala ya uhuru na umoja iwe Kleruu dhidi ya Mwamwindi kwa maana ya nchi ni watu na watu ni maisha na maisha ni mgongano wa wenye nacho na wasio nacho. Wimbo wetu wataifa utaje njia za kuyaunganisha matabaka haya mawili ili kwamba lisitokee tabaka moja kuwa laana mbele ya jingine, kama ambavyo tulishuhudia mwenye nacho akitukanwa na asiye, wakati mwenye nacho akiona nihalali kumpiga risasi asiye nacho kuliko kutengeneza uwiano wa vipato.

Nakumbuka wakati nasoma kulikuwa na siku rasimi ya wanafunzi kutembelea eneo lenye kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Iringa Dk. Wilbert Kleruu. Ninacho kumbuka tuliimba nyimbo za kichochezi na sielewi kwanini tulikuwa hatukamatwi, wanafunzi pamoja na walimu na viongozi wa ngazi za tarafa, wilaya na mkoa.

Tuling’ang’ana kumwita Mwamwindi mnyonyaji na mpinga ujamaa huku tukimsifu Kleruu kuwa shujaa na shupavu, hakuna aliye onesha waziwazi kuwa kinyume na kauli hizo maana tulirudi majumbani mwetu tumevimbishwa vichwa eti tumefanya vizuri. Lakini tukiwa tumesahahu kuwa mashamba ya Mwamwindi na wengine wa tabaka la Mwamwindi yalipokonywa na kuwa mali ya umma, hapo nani mpinga ujamaa kati ya wawili hao?

Nihitimishe kwa kusema dawa ya kuweka uwiano huu wa kipato imo mikononi mwa maisha ya kila mtu katika msuguano wake na kazi anayofanya kilasiku, kazi iliyo halali kumtengeneza afya na utu wake. Uwiano wa kipato hauwezi kuimarishwa kwa ukali wa mtu (Kleruu) wala kwa mtutu wa bunduki (Mwamwindi), wala kwa maridhiano (watoto wao) bali kwa mila na tamaduni asili.

Mkakatima luhwago

lmkakatima@gmail.com
 
Back
Top Bottom