Mithali 6:1-11
Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa rafiki yako, Ikiwa wewe na mgeni mmepeana mikono, Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,
Sasa, mwanangu, fanya hivi ukajiokoe,
Kwa kuwa umejitia mkononi mwa jirani yako; Nenda ukanyenyekee, na kumsihi jirani yako. Usiache macho yako kupata usingizi, Wala kope za macho yako kusinzia. Ujiponye kama paa na mkono wa mwindaji, Na kama ndege katika mkono wa mtega mitego.
Ewe mvivu, mwendee chungu, Zitafakari njia zake ukapate hekima. Kwa maana yeye hana kiongozi, Wala msimamizi, wala mkuu, Lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
Ewe mvivu, utalala hadi lini? Utaondoka lini katika usingizi wako?
Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.