Adai bila ridhaa ya wananchi ni uhaini
*Adai Kibaki, Obote walilikataa miaka ya 60
*Asema ni mfumo wenye gharama kubwa
Na Hassan Abbas
HUWEZI kulizungumzia vyema suala la shirikisho ambalo linagusa muungano wa mataifa mbalimbali bila kuwa manju katika sheria za kimataifa na ufahamu mpana wa siasa na historia za nchi husika, hivyo ndivyo ilivyobainika Jijini juzi.
Mmoja wa watu muhimu ambao wanaweza kulizungumzia
kwa ufasaha suala la shirikisho linalotolewa maoni sasa la nchi za Kenya, Tanzania na Uganda (na baadaye Rwanda
na Burundi) ni Profesa Palamagamba John Kabudi.
Huyu ni Mkuu wa Idara ya Sheria za Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye juzi aliamua kuvunja ukimya kuhusu mwenendo wa shirikisho hilo.
Alisisitiza kuwa iwapo Shirikisho la Afrika Mashariki ambalo mchakato wake unaendelea hivi sasa litafikiwa bila ridhaa ya wananchi, huo utakuwa sawa na uhaini kwa sheria za Tanzania.
Msomi huyo aliyebobea katika maeneo anuai ya sheria za kimataifa, anasema pia kwamba kitendo cha sasa wananchi kutakiwa wajadili shirikisho ni makosa makubwa kwani wananchi walitakiwa kwanza waamue nchi zao ziungane kwa muundo gani kati ya mifumo mbalimbali ya muungano inayojulikana duniani ndipo mambo mengine yafuatie.
Alisema kuna aina mbali mbali za muungano ambazo taifa moja linaweza kuufanya na jingine na akazitaja baadhi ya aina hizo kuwa ni Union, Federation, Confederation na Community. Akasema wananchi wa Afrika Mashariki wangeamua kwanza juu ya aina hizo.
Profesa Kabudi aliyekuwa akichangia mada kwenye kipindi cha This Week In Perspective kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TvT), akizungumzia uhalali wa kuundwa shirikisho hilo alisema chini ya sheria za kimataifa, maamuzi hayo mazito hayawezi kufanywa na marais tu.
" Kanuni zinasema bayana kwamba ni wazo ambalo lazima lifikishwe kwa wananchi waamue kupitia kura ya maoni muundo na hata taratibu zake," alisema mtaalam huyo.
Akaongeza katika hilo akisema kwa sasa tayari makosa yamefanywa kwa wananchi kutoshirikishwa na badala yake viongozi ndio wameshaamua jumuiya hiyo iwe ya shirikisho.
" Kabla hata ya kuamua muungano huo uwe wa shirikisho au la, hilo ni moja ya maswali ambayo wananchi walitakiwa kuyaamua kwanza. Ni kosa kuamua halafu ndipo unakwenda kuwauliza wananchi kama wanakubali," alisema Profesa Kabudi.
Akizungumzia kanuni za Tanzania kujiunga katika shirikisho hilo, mtaalam huyo ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi wa sheria wa UDSM, amesema chini ya mkataba wa Vienna, Tanzania haiwezi kuingizwa katika shirikisho bila pia maamuzi ya wananchi kupitishwa na Bunge.
" Itatakiwa theluthi mbili ya wabunge wa Bunge la Muungano na lile la Zanzibar wapitishe uamuzi huo ndipo uwe umekidhi matakwa ya kisheria.
" Kuiingiza Tanzania katika shirikisho bila ridhaa hiyo ya wananchi na mabunge yao itakuwa sawa na uhaini," alisisitiza.
Akijibu swali la kama Tanzania iko tayari kuingia katika shirikisho hilo alisema hilo kwa sasa haliwezekani na si jambo la busara.
" Kama ningetakiwa kutoa maoni yangu ya kitaalamu kuhusu hilo, ningesema bila kinyongo kwamba labda baada ya miaka 25 hivi ndipo tutakuwa tayari," alisema.
Akifafanua zaidi na kujibu hoja juu ya iwapo wananchi wa Tanzania ambao wengi wanaonekana kuwa na hofu dhidi ya shirikisho hilo kama wana mantiki, Profesa alisema hofu waliyonayo Watanzania inaeleweka.
" Lazima wawe na hofu na hofu yao iko wazi, Tanzania haiko tayari kuingia katika shirikisho kwa sababu nyingi. Shirikisho lazima liangalie mambo mengi.
" Tanzania inasifika kwa amani na utulivu ambao umeipa taswira kubwa hata kwenye Umoja wa Mataifa. Utawahakikishia nini Watanzania unapoungana na watu kama Rwanda na Burundi (zenye mapigano ya kikabila)?" alihoji.
Akasema pia kiuchumi nchi hizi hazilingani na ndio maana hata kabla ya kuundwa Jumuiya ya kwanza ya Afrika Mashariki mwaka 1967, suala la shirikisho lilishindikana huku Kenya na Uganda ndizo zilizokataa baada ya kujiona hazikuwa tayari.
" Kwanza kabisa mkataba wa Tanganyika kuwa koloni chini ya udhamini wa UN ulizuia nchi hiyo isiingie katika aina yoyote ya shirikisho. Lakini mwaka 1961 lilipokuja wazo hilo tena Milton Obote (aliyekuwa Waziri Mkuu) wa Uganda akakataa.
" Wazo hilo lilipoibuka tena mwaka 1963, mwanasiasa aitwaye Emilio Stanley Mwai Kibaki (akiwa mbunge wa jimbo ambalo kwa sasa linaitwa Makadara) alilipinga wazo hilo. Huyu nadhani sasa ndiye rais wa Kenya. Sasa kwa nini leo Tanzania inataka kukimbilia suala hilo," alisema akionesha kuwa wenzetu mwanzo walikataa kwa sababu waliona hawakuwa tayari, sasa wamejiandaa.
Akizungumzia shirikisho hilo, Profesa Kabudi alisema makosa mengi yamefanyika ikiwa ni pamoja na wananchi kutoshirikishwa katika mikataba ya awali na ya msingi sana kama ule wa kuunda shirikisho la kiuchumi, soko la pamoja na pia muungano wa sarafu.
" Hakuna kitu kigumu na kitakachowaathiri sana wananchi wa Tanzania kama soko huria, kitu ambacho mara nyingi huchukua miaka kati ya 10 hadi 15 kuundwa. Lakini katika hili watu hawakupewa nafasi kujadili, wameingizwa tu kujadili hatua ya mwisho ya shirikisho," alisema msomi huyo.
Anasema huwezi kuzungumzia shirikisho la kisiasa wakati kitu cha muhimu kama muungano wa kiuchumi na sarafu wananchi hawakuelimishwa.
" Kwanza shirikisho la kisiasa ni gharama sana kuliendesha kwa sababu nchi kama Tanzania itatakiwa kundesha serikali tatu; Kuchangia katika serikali ya Muungano, Zanzibar na ya shirikisho. Maoni yangu shirikisho ni muundo wenye gharama kubwa sana," alisisitiza.
Kilichojitokeza katika mjadala huo pia ni kuhusu ulazima wa kuharakisha kuundwa kwa shirikisho hilo na namna wananchi wanavyopewa fursa ya kujadili faida na hasara za shirikisho.
Katika hilo Profesa Kabudi, ambaye pia amepata kuwa mwandishi wa hotuba za rais katika awamu ya pili ya Alhaji Ally Hassan Mwinyi, anasema hakuna sababu za kuharakisha shirikisho hilo na akasikitika kuona hata namna ya kulijadili shirikisho lenyewe wananchi wanapotoshwa.
" Ukiangalia faida na hasara wanazozijadili baadhi yao utabaini si za shirikisho la kisiasa. Wananchi wengi wanajadili faida na hasara za muungano wa kiuchumi ambao umeshapita.
" Wengi wanaonekana hawakuelimishwa kuhusu shirikisho na hawalielewi ni kitu gani hatimaye wanajikuta wanajadili vitu ambavyo vilishaamuliwa," alisisitiza.
Maoni haya ya msomi huyo ambaye pia ni mahiri katika Sheria za Mazingira, Ndoa, Madhara, Juriprudensia (falsafa za sheria) na Sheria za mambo ya kale, kati ya nyingine nyingi ambazo amebobea, yanazidi kuibua mjadala na kuunga mkono kilio na hofu ya Watanzania wengi.
Mpaka sasa mchakato wa kutoa maoni unaendelea jijini Dar es Salaam chini ya Kamati iliyoundwa na serikali kushughulikia masuala hayo.
Kinachojitokeza ni kwamba pamoja na suala la mataifa kuungana kuwa ni la muhimu katika zama hizi za utandawazi, Watanzania kutoka kada za wasomi au raia wa kawaida, wote wana hofu kuu ya je, ukiangalia vurugu za kisiasa katika nchi tutakazoungana nazo, mifumo yao ya kiuongozi na mipasuko ya kijamii iliyopo, shirikisho kwa sasa litatusaidia au kutuingiza matatizoni?
|
Tatizo kubwa jingine wakati kamati hiyo ikiendelea kukusanya maoni, imebainika, ni wananchi wengi kutofahamu wanachokitolea maoni, kama pia alivyobaini Profesa Kabudi.
Wengi kati ya wanaotoa maoni wamejikuta wakijadili na hata kuzungumzia masuala ambayo hayahusu shirikisho, lakini kwa ujumla, wengi wao, ukisikiliza walichokisema na taarifa za vyombo vya habari vinavyoripoti, utabaini wanasema Tanzania haijawa tayari na wengi wanasema hilo, tena waziwazi. Tunakaribisha makala kuhusu mjadala huu. - Mhariri