HAYA NDIO TUNAYATAFUTA KWENYE EAF
Arusha yatikisika: Polisi100 wapambana na majambazi
*Risasi zapigwa kwa zaidi ya saa sita
*Wasichana wafichua maficho yao
*Bomu latumika kulipua maficho
Na Mussa Juma, Arusha.
MJI wa Arusha, jana uligeuka uwanja wa mapambano baada ya polisi, wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na vikosi vingine vya ulinzi na usalama, kupambana vikali na watuhumiwa wa ujambazi baada ya kugundua maficho yao.
Mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha, walikusanyika katika eneo la Njiro Kontena, kushuhudia tukio hilo, ambalo wengi wanalifananisha na sinema kutokana na kurushiana risasi kwa saa zaidi ya sita kati ya polisi na watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi.
Hadi jana jioni, saa kadhaa baada ya watuhumiwa hao wa ujambazi kuzidiwa nguvu na kuamua kujisalimisha, mazungumzo ya tukio hilo yalikuwa yametawala mazungumzo ya watu karibu pembe zote za mji wa Arusha.
Watuhumiwa hao, wanadaiwa kuhusika na wizi wa Sh234 milioni mali ya Benki ya National Microfinance (NMB) tawi la Mwanga, Kilimanjaro. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Basilio Matei, watuhumiwa hao ni Samweli Gitau Saitoti (33) anayedaiwa kuwa ni Mkikuyu mkazi wa eneo la Ngong Nairobi, ambaye ni dereva wa matatu na Peter Michael
Kimenya (40) Mkikuyu mkazi wa Thika Nairobi, ambaye ni dereva wa magari makubwa.
Inadaiwa pia kuwa mmoja wa watuhumiwa hao, Samson Chonjo (26), aliyekamatwa katika tukio tofauti jana, ni miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kuhusika na wizi huo.
Watuhumiwa hao waliwapa wakati mgumu polisi tangu saa 8.00 usiku wa kuamkia jana, walipozingira nyumba hiyo hadi saa 5.53 asubuhi, walipoamua kujisalimisha baada ya kurushiana risasi na polisi waliozingira nyumba walimokuwa wamejificha.
Katika tukio hilo, polisi walikamata bunduki mbili aina ya SMG zikiwa na risasi 85, bastola tano zikiwa na magazini nne zenye risasi 30 na majaketi ya kuzuia risasi pamoja na mabomu mbalimbali yaliyokuwa hajalipuliwa. Bado askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wanaendelea na kazi ya kutegua mabomu yaliyokuwa katika nyumba hiyo.
Kamanda Matei alisema majambazi hao walikamatwa na fedha taslimu dola 8,145 za Kimarekani na Sh 978,000 na alimtaja mwingine aliyekamatwa kuwa ni Samson Chonjo (26)
mkazi wa eneo la Ngulelo mjini hapa.
Alisema Chonjo alikamatwa jana asubuhi katika eneo la Ngulelo baada ya polisi kupata taarifa za wasamaria wema. Kamanda Basilio, alisema maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka jijini Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha bado wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao.
"Kama unavyojua leo ndio tumewakamata bado tunawahoji kuhusiana na matukio ya ujambazi na sio la Mwanga pekee," alisema Kamanda Basilio.
Alisema licha ya kuhojiwa kwa matuhumiwa hao, bado Kikosi Maalum ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kinaendelea kutegua mabomu kadhaa yaliyokuwa yametegwa na majambazi hao kutoka Kenya kabla hawajajisalimisha.
Ilielezwa kuwa watuhumiwa hao walitega mabomu kuzunguka nyumba hiyo na walikuwa wakirusha risasi mfululizo kwa kutumia bunduki aina ya SMG na bastola, na wakati mwingine wakirusha mabomu ya kutupa kwa mikono.
Hata hivyo, jitihada za polisi, viongozi wa serikali, maafisa wa Jeshi la Wananchi na maafisa wa Usalama wa Taifa ambao baadhi yao kwa mara ya kwanza jana walikuwa wamebeba silaha nzito, ilisababisha watuhumiwa hao kujisalimisha majira ya saa 5.53 asubuhi.
Mamia ya watu waliojitokeza kushuhudia tukio hilo, walishangazwa na ujasiri watuhumiwa hao kwa kurushiana risasi na polisi zaidi ya 100 kwa muda mrefu, licha ya kuwapo Kikosi Maalum cha Polisi kutoka Dar es Salaam ambao baada ya kufanikiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo, watuhumiwa hao walipanda juu ya dari.
Maficho ya watuhumiwa hao, waliovalia majaketi ya kuzuia risasi, huku wakiwa wametega mabomu ndani ya nyumba hiyo na nje, yalijgundulika kutokana na makachero wa polisi kunasa namba za simu za wasichana ambao walikuwa wana uhusiano nao kimapenzi.
Akizungumza katika eneo la tukio, akiwa amevaa kifaa cha kuzuwia risasi, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kapteni Evance Balama alisema, mara baada ya polisi kuwasiliana na wasichana hao. walitaja eneo walipo na polisi kuamua kuwafuata.
Kapteni Balama alisema baada ya wasichana hao kutambua kuwa wanasakwa na polisi waligoma kutoka katika nyumba hiyo, hadi mama mzazi wa mmoja wa wasichana hao alipotafutwa na kuzungumza na mtoto wake.
Alisema baada ya majadiliano kadhaa baina ya mama huyo na mtoto, baadaye watuhumiwa hao waliruhusu wasichana hao kutoka nje ya nyumba hiyo ya kisasa yenye ghorofa moja.
Kwa kiasi kikubwa, kutoka nje kwa wasichana hao, kuliwasaidia polisi kuwajua maadui, hasa walipoelezwa kuwa tayari wametega mabomu nyumba nzima, hivyo wasipotumia busara wanaweza kuangamia.
"Hawa wametupa msaada mkubwa na bado tunawashikilia, tunaamini watatueleza mengi," alisema afisa mmoja wa polisi akiwa na maafisa usalama katika eneo la tukio.
Jitihada za Polisi wa Kikosi Maalum kutoka Dar es Salaam, wakiongozwa na maafisa mbalimbali akiwamo Kamanda Duani Nyanda, zilifanikisha polisi kuingia ndani ya nyumba hiyo, huku wakiwa na wamevalia majaketi ya kuzuia risasi.
Hata hivyo, polisi hao walishindwa kukabiliana uso kwa uso na watu hao, kutokana na kupewa taarifa kutoka ngazi za juu za jeshi hilo kuwa watuhumiwa wanatakiwa kukamatwa wakiwa hai ili watoe taarifa zitakazosaidia kuvunja mtandao wao wa ujambazi nchini.
"Hapa tulipo kama tukiamua kumimina risasi lazima tutawaua, ila nasi lazima kutakuwa na vifo, lakini kuna maelekezo kuwa tusiwaue," alisema afisa mmoja wa polisi aliyekuwapo eneo la tukio, saa chache kabla ya watuhumiwa kuamua kujisalimisha.
Baada ya jeuri ya watuhumiwa hao kupiga hovyo zaidi ya risasi 15, polisi waliamua kujibu kwa kupiga makombora ya RPG ambayo yalifanikiwa kubomoa sehemu kubwa ya kuta za nyumba hiyo na wakatupa zaidi ya mabomu 20 ya machozi ndani ya nyumba.
Mapambano yalishika kasi zaidi majira ya saa 3.00 na 4.00 asubuhi, lakini watuhumiwa hao waliendelea kukaidi amri ya kujisalimisha huku wakijibu kwa risasi za rashasha.
Hata hivyo, ilipofika majira ya saa 5.00 asubuhi, watuhumiwa hao waliokuwa wakiwasiliana na wasichana wao, waliweza kupiga simu polisi namba 112 na kuomba kujisalimisha kwa masharti kuwa wasiuawe.
Baada ya simu hiyo, maafisa wa polisi wakiongozwa pia na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (RCO), Chilogile, walikubali na kutoa muda wa kujisalimisha.
Kutokana na makubaliano hayo, kwa kutumia kipaza sauti walihesabiwa hadi 10, lakini walikaidi ndipo polisi walipowaonya kuwa, wataishusha nyumba yote kwa mabomu na risasi, hali iliyowafanya kujisalimisha mmoja mmoja, wakiwa wameweka mikono kichwani.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia watu hao wawili, wakiwa chini ya ulinzi wa polisi wakionekana wenye afya nzuri, huku mmoja akiwa mweupe mwenye kipara ambaye polisi kutoka Dar es Salaam walimtambua kuwa alitajwa kuhusika katika uporaji wa Ubungo.
Watuhumiwa hao, waliondolewa kwenye jumba hilo majira ya saa 6.00 mchana wakiwa kwenye gari la polisi namba T118 AEN, huku wakisindikizwa kwa ulinzi mkali.
Awali, mamia ya wananchi wa Arusha walitaka kuzuia kuondolewa kwa watu hao wakitaka kuwaua, lakini polisi walifanikiwa kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi na kuwasambaza kwa kutumia mbwa.
Nyumba hiyo ni mali ya Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Makoye Ngerere, ambaye hivi karibuni alihamishiwa Makao Makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Habari za uchunguzi zimebainisha kuwa wathumiwa hao, walipanga nyumba hiyo kuanzia Jumapili Julai 17 kwa makubaliano ya kulipa kodi ya Sh450,000 kwa mwezi, kwa muda wa miezi sita.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa watuhumiwa hao kuwa, walipata nyumba hiyo kupitia dalali mmoja wa kike (jina linahifadhiwa).
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Korongoni ambacho ndipo tukio hilo lilitokea, Zulfa Mhina alisema kabla ya kuishi katika nyumba hiyo majambazi hao, alipokea watu kadhaa waliokuwa wanatafuta nyumba.
Mhina ambaye nyumba yake inapakana na nyumba walimokuwa majambazi hao, alisema mtu mmoja alifika kwake kutafuta nyumba akidai ana vijana wake wanatoka nje ya nchi.
Hata hivyo, baada ya kuoneshwa nyumba hiyo hakurudi hadi mapema wiki hii alipopata taarifa tayari nyumba hiyo inawapangaji.
Alisema taarifa hizo alipewa na aliyekuwa mlinzi wa nyumba hiyo, hamisi Kironga ambaye aliondolewa mara baada baada ya majambazi hao kupanga nyumba hiyo.
Hadi jana mchana kikosi sa askari toka jeshi la wananchi(JW) cha kuteguwa mabomo na maafisa kadhaa wa serikali akiwepo mbunge wa jimbo la Arusha, Felix Mrema walikuwa katika eneo la tukio wakiendelea na ukaguzi wa mabomo.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Basilio Matei ambaye alifika eneo la tukio mchana alisema kuwa angetoa taarifa majira ya jioni mara baada ya kukusanya taarifa zote muhimu.