Na bado, ngoja huo "MUUNGANO"uje!!
Kenya yanyakua sifa za Serengeti kwa utalii
Na Ramadhan Semtawa
WAKATI dunia inatambua umaarufu na utajiri wa kitalii wa mbuga ya Serengeti na hivi karibuni kutangaza kama moja ya maajabu mapya ya dunia, Tanzania imeendela kuduwaa bila kuitumia nafasi hiyo kwa kutangaza utalii.
Badala yake majirani zake Kenya, ambako mbuga ya Serengeti inaendelea kwenye mipaka yake kwa jina la Masai Mara, imechangamkia umaarufu huo kwa kutangaza kwa nguvu sehemu yao kwenye tovuti na majarida mbalimbali duniani.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kwamba baada ya Serengeti kutangazwa kwamba ni moja ya maajabu mapya saba duniani ikishika nafasi ya saba, wahamasishaji wa utalii wa Kenya wamechukua nafasi hiyo kuitangaza kwa nguvu Masai Mara, ambayo ni sehemu ya mwendelezo wa mbuga ya Serengeti.
Novemba 17 mwaka huu kwa mara ya kwanza, Serengeti ilitangazwa kuwa ni moja ya maajabu hayo mapya na Kituo cha Televisheni cha ABC kupitia kipindi chake cha Good Morning America Tv Show na katika gazeti la USA Today.
Kwa kuwa Masai Mara ni eneo moja na Serengeti lakini likitengenishwa tu na mpaka wa Tanzania na Kenya, watetezi na wahamasishaji wa utalii wa Kenya, wamechangamkia mafaniko hayo kwa kutangaza kwamba maajabu hayo mapya saba ni Masai Mara.
Mbuga ya Serengeti kwa upande wa Tanzania ina ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 wakati Masai Mara ina ukubwa wa kilometa za mrada 1,510 tu.
Juhudi hizi za Kenya zinaiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuvutia utalii kwa upande wa Masai Mara, lakini Serengeti ikiwa na ukubwa mara 9.7 ya Masai Mara bado haijatangazwa vya kutosha kuweza kufaini nafasi hii mpya ya kuwa maajabu ya dunia.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amethibitisha kutambua kupanda chati kwa Serengeti, lakini pia kutambua kwamba kuna njama za kimataifa za kuitangaza kama Masai Mara.
Alisema Tanzania haiwezi kuingia katika malumbano ya 'kihujuma' bali itaudhihirisha ulimwengu kuhusu Serengeti na vivutio vyake vya utalii.
Kauli kama ya Profesa Maghembe pia ilitolewa na Rais wa Kampuni ya Bradford Group ya Marekani, Mira Berman, ambayo imepewa dhamana ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania. Alisisitiza kwamba Serengeti ndiyo imekuwa maajabu ya saba mapya ya dunia.
Berman alisema mjini New York wiki iliyopita, kwamba takwimu zinaonyesha kwamba baada ya Serengeti kutangazwa kama maajabu ya saba idadi ya watalii wanaosafiri kuelekea Afrika imeongezeka.
Rais huyo alisema kampuni hiyo kwa kushirikiana na kampuni nyingine ambazo ni Miracle Corner of the World na African Travel Association (ATA), zimekubaliana kumeiweka Tanzania katika nafasi nzuri kiutalii.
Hata hivyo, alisema tatizo kubwa linalaoikabili Tanzania ni ukosefu wa miundombinu ya kisasa, ikiwamo mahoteli makubwa na kutaka serikali iongeze bajeti ya utalii.
Wakati Maghembe na Berman wakisema hayo, gazeti hili limebaini mtandao unaonyesha maajabu hayo wa www. new world seven wonders, ukiitaja mbuga iliyoshinda kwamba ni Masai Mara na hakuna eneo ambalo Serengeti imetajwa.
Watangazaji wa vivutio vya utalii wa Kenya, wamechangamka na mafaniko haya mapya ya Serengeti na kwa mujibu wa taarifa za mtandao huo hadi mwishoni mwa wiki hii, zinaitaja Masai Mara kuwa ndiyo imepandishwa hadhi kutokana na kuwa mazingira mazuri ya kuvutia wanyama wa aina tofauti ambao ni twiga, duma, tembo, simba, pundamilia na uwanda mzuri wa makazi ya wanyama.
Ukiacha Serengeti ambayo imeshika nafasi ya saba, jiji la Jerusalem limekuwa la pili kutokana na historia yake ndefu huku majengo ya kifahari ya Potal Palace yaliyopo Tibeti ambayo hufahamika kama majengo ya Malaika kutokana na muundo wake, yakiwa ni ya kwanza.
Maajabu ya tatu ni Polar Ice ambako inapatikana barafu ambayo si ya kawaida, ya nne ni visiwa vya Kaskazini Magharibi vya Hawaii, visiwa vilivyopo Marekani ambayo vimekuwa na viumbe adimu ambavyo ni pamoja na samaki aina tofauti.
Maktaba na ofisi ya mtandao wa Intaneti iliyopo Marekani nayo imechukua nafasi ya sita kati ya maajabu hayo kutokana na kuwa na mfumo na miundombinu ya kutosha ya kupata huduma za mawasiliano ya njia ya kompyuta, vitabu na taarifa mbalimbali za dunia.
Maajabu ya sita ni majengo ya kizamani maarufu kama Mayan Pyramids ambayo nayo yako Marekani na kwamba kura za kuchagua maajabu hayo zilipigwa kwa njia ya kompyuta moja kwa moja na ujumbe mfupi.
Akizungumzia zaidi hilo, Profesa Maghembe alisema hatua ya Tanzania kuanza kupambana na wanaojaribu kuhujumu vivutio vyake vya utalii inaweza kuathiri biashara ya sekta hiyo.
Profesa Maghembe alisema wiki moja iliyopita katika mkutano wa utalii uliofanyika Uingereza ambako alihudhuria, alinadi vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro.
"Tunajua kuna hujuma dhidi yetu, sisi hatuwezi kupamba na wanaoeneza hujuma bali tunaueleza ulimwengu kuhusu vivutio vyetu," alisisitiza Profesa Maghembe.
Meneja Uhusiano wa Bodi ya Utalii, Geofrey Tengeneza, alithibitishia gazeti hili ofisini kwake jijini Dares Salaam wiki iliyopita kwamba Serengeti ndiyo imeshinda kuwa moja ya maajabu mapya kati ya hayo saba na bodi itaendelea kuitangaza mbuga hiyo na vivutio vingine.
Wazungu kutoka Ulaya walipofika Serengeti mwaka 1913 walishangaa uzuri wa wanyama, uoto wa asili na walibatiza eneo hilo kuwa ni Peponi, yaani Paradise.
Katika miaka ya 80 mwishoni Tanzania iliamua kufunga mpaka wa Bologonja ambao unatenganisha Masai Mara na Serengeti kwasababu za kiuchumi.
Uamuzi huo ulitokana na uchunguzi uliothibitisha kwamba watalii walikuwa wakiingia Serengeti wakitokea Masai Mara huku malipo yote ya malazi, chakula na kuangalia wanyama yakifanyika upande wa Kenya.
Hatua hiyo ilisababisha mvutano mkubwa kati ya Kenya na Tanzania.