Tusipookoa Kigoma, Kagera, Mungu atatuhukumu
Manyerere Jackton
HIVI karibuni niliandika makala iliyokuwa na kichwa kisemacho: Kagera, Kigoma si Tanzania tena!
Wengi waliowasiliana nami, walisema hawakujua chochote kilichokuwa kikiendelea katika ukanda wa magharibi mwa nchi yetu, hadi waliposoma makala hiyo. Walinishukuru kwa kuwafumbua macho.
Majibu haya yalinisaidia kujua mambo kadhaa muhimu. Mosi, ili tatizo lifahamike kwa wengi, si lazima liwe kubwa. Kwa kutotambua matatizo yanayowakabili Watanzania wenzetu katika mikoa ya magharibi, hii haina maana kwamba tatizo la ujambazi, utekaji, uporaji na mauji katika ukanda huo, ni dogo.
Ni kubwa, lakini kwa kuwa semina zote zinafanywa Arusha, Dar es Salaam, Bagamoyo, Mwanza, Dodoma, Zanzibar (Unguja) na Morogoro; hakuna anayeyajua haya.
Laiti kama siku moja semina hizi zingepelekwa Kibondo, Ngara, Kasulu, Biharamulo, Karagwe au Muleba; kisha basi la wanaojiita wanaharakati likatekwa, leo ujambazi ungekuwa kwenye vitabu vya hadithi.
Pili, maneno ya wanasiasa wetu yamewaingia sana Watanzania. Maneno kama Tanzania ni kisiwa cha amani, Tanzania hakuna mapigano, Watanzania wanapendana; yote haya na mengine, yamewafanya Watanzania wengi waamini kuwa nchi hii ni tulivu. Tanzania ina wavumilivu tu.
Majuzi tu, Jeshi la Polisi liliposema limedhibiti ujambazi kwa asilimia zaidi ya 50, wananchi wengi walipiga makofi. Wakashangilia. Wakatamani IGP Mwema ajitokeze-wambebe-wampe ofa kutokana na kazi kubwa na nzuri.
Waliokuwa wa kwanza kuondoka kwenye baa na sehemu nyingine za starehe, wakawa na sababu ya kuwafanya wakeshe! Wawahi kwenda wapi, ilhali nchi imeshatulia?
Wanasiasa wakadakia. Unaona Serikali ya Ari mpya, Kasi mpya, na Nguvu mpya? Ujambazi kwisha! CCM oyeeee!
Hata wale tunaowajua wazi kwamba wanaikwamisha Serikali ya Awamu ya Nne, wakawa wa kwanza kutamba. Kwa wanasiasa, na Watanzania wengi, Tanzania maana yake ni Dar es Salaam! Ujambazi ukipungua Dar es Salaam, basi Tanzania yote iko shwari!
Ujambazi, uporaji na mauaji yanayotokea Kigoma na Kagera, si ujambazi! Na kama ni ujambazi, basi ni mdogo sana! Tunajidanganya.
Kwa bahati mbaya, sherehe na mbwembwe hizi ni vitu vinavyoonekana upande mmoja tu wa nchi. Kiongozi anayetaka kutoa tambo hizo, ahakikishe anatumia majukwaa yote, isipokuwa majukwaa yaliyopo Kibondo, Kasulu, Kigoma, Karagwe, Ngara, Biharamulo, Muleba, Kahama na kwingineko.
Kusema kwamba ujambazi umepungua kwa asilimia zaidi ya 50 nchini, maana yake ni kwamba hiyo asilimia 50 iliyobaki, ipo Kagera, Kigoma na maeneo jirani. Huu ni ukweli usiopingika.
Ndugu zangu Watanzania wanaoishi nje ya Kagera, Kigoma, Rukwa na sehemu za mikoa ya Mwanza na Shinyanga, watambue kuwa nchi yetu si salama kama tunavyojilazimisha kuamini.
Mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo ina matukio machache ya ujambazi, wananchi wajue kuwa ndugu zao wa Kigoma, Kagera na sehemu za mikoa jirani, hali ni mbaya. Wanataabika. Wanaporwa. Wanajeruhiwa. Wanauawa, na wengine juzi ndiyo wamesikika wake wakibakwa mbele ya waume zao! Fikiria wanaume sita wamefungwa kamba, wanashuhudia wake zao wakibakwa! Unyama gani kuuzidi huu?
Haya ni mambo ya maharamia kutoka nchi jirani wanaoshirikiana na Watanzania wachache. Hawa ni maharamia waliomwaga damu za watu wasio na hatia, kiasi kwamba sasa wamewageukia Watanzania.
Kinachowaponza Watanzania hawa ni uungwana wao. Kuwakubali wageni wanaotumia kivuli cha ukimbizi. Wakimbizi ndio chanzo kikuu cha yote haya.
IGP Mwema kafanya jambo la maana. Kamteua Kamanda Venance Tossi kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera. Tossi tunamjua, ni mchapakazi, ni aina ya polisi adimu katika nchi yetu. Kilimanjaro ilisifika sana kwa ufedhuli, iligeuka ikawa kama Kagera na Kigoma. Ilisifikia kwa ujambazi na uhalifu wa kila aina.
Miezi michache ya Kamanda Tossi mkoani humo, ilitosha kurejesha amani. Majambazi, wezi na wahalifu wengine, wanamtambua Tossi kama adui yao mkuu.
Sasa amepelekwa Kagera. Hapo IGP Mwema, na wote waliobuni mabadiliko hayo, wanastahili kupongezwa.
Tossi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi, serikali na wananchi, sasa ana kazi kubwa. Dhima aliyopewa kamanda huyu, ni kubwa na ya hatari.
Ndiyo, amepelekwa Kagera. Je, ana vitendea kazi? Ana askari wa kutosha? Ana vifaa maalumu vya usalama kwa askari wanaopambana na majambazi? Anawezeshwa kupata mafuta ya magari kwa saa 24? Je, askari na yeye wametengewa posho kulingana na ugumu na hatari ya mazingira ya kazi hii waliyopewa na taifa?
Tosi huyu bila magari ya kutosha, bila pikipiki, bila askari wa kutosha, bila motisha kwa askari, bila mahema, bila mlo mzuri kwa askari, bila viburudisho kadha wa kadha, atayamudu mabazazi haya kutoka nchi jirani?
Bila vifaa vya kuwawezesha kuingia ndani ya misitu kufanya doria na kuwasaka wauaji hao, Tossi ataweza kuleta mabadiliko? Hawezi.
Je, wenzake aliowakuta katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na sehemu za Shinyanga, wana hayo niliyoyataja hapo juu?
Hii ina maana kwamba bila kumwezesha Tossi na wenzake kwa kila hali, vita dhidi ya majambazi na waporaji katika ukanda huu itakuwa kama Israel na Palestina. Haitakwisha.
Kama nilivyosema katika makala iliyopita, suala la ujambazi katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Rukwa na maeneo ya mikoa jirani, ni tatizo la kitaifa. Hili si jambo la kuwaachia watu wachache.
Kama wakimbizi wanatumia bunduki nzito nzito na mabomu, hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba hii ni vita! Kama ni vita, inabidi vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania navyo viingie kivita.
Hakuna diplomasia kwa wauaji waliojipenyeza ndani ya ardhi yetu, wakaifanya misitu yetu kuwa ngome zao, kisha watu wa aina hiyo, tukawaondoa kwa mapanga au marungu! Wamekuja kivita, sharti washughulikiwe kivita.
Nchi haiwezi kutunza vifaru na magari ya deraya, ilhali kuna sehemu ya Tanzania imetwaliwa. Si busara kuwalea makamanda na wapiganaji, wakaota vilibatumbo, ilhali kuna kazi ya kufanya huko Kigoma na Kagera.
Viongozi wenye uchungu na Watanzania wenzao wanaotaabishwa magharibi mwa nchi, hawawezi kuafiki suala la ukosefu wa fedha kama sababu ya kuwaruhusu majambazi kuanzisha jamhuri ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kuna pesa nyingi zinatumiwa vibaya. Kuna ufujaji wa ajabu. Wananchi wanaachwa wafe, huku wengine wakitumia mabilioni katika semina na makongamano yasiyoisha. Kama ni fedha za wafadhili, wafadhili gani hawa wanaofadhili milo na vinywaji kwenye semina, wakakataa kuwafadhili maskini wanaouawa au kuishi kwa taabu katika jamhuri yao?
Nchi hii kuna meli kubwa ambayo jina lake limefichwa! Meli hii imebeba watu wengi, maarufu kwa ubunifu. Meli hii inaitwa mv Ulaji!
Miongoni mwa abiria wake ni Idara ya Takwimu. Idara hii imepanga kutumia sh bilioni 3.6 kufanya tathmini ya mapato na matumizi ya kaya 896! Haya ni maajabu.
Unakwenda Kibondo, Kasulu, Ngara, Biharamulo, Muleba, Karagwe, Kahama, kuuliza mapato na matumizi ya kaya? Wana muda wa kufanya kazi wananchi hawa? Watafanya kazi vipi ndani ya wimbi kubwa la ujambazi? Wafanyabiashara wa huku watasafiri vipi, ilhali hawawezi kwenda sokoni bila mitutu ya polisi, na hata wakiwa na polisi, wanatekwa na kuuawa?
Hayo mapato na matumizi kwa kazi ipi? Je, kwa nini fedha hizo zisitumike kununua vitendea kazi na kutoa motisha kwa polisi na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wanaoshinda na kukesha wakiwa wameweka roho mikononi?
Pesa hizo kwa nini zisitumike kununua japo baiskeli kuwasaidia polisi wanaohangaika kwenye mapori ya Kyamisi, Biharamulo, Benako, Lugufu na kwingineko? Pesa hizo kwa nini zisitumiwe kuhakikisha magari ya polisi yanakuwa na mafuta muda wote wa kazi?
Tuna raha gani ya kutumia sh bilioni 3.6, kufanya kazi ambayo ilifanywa katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002? Haya ya mapato na matumizi, mbona yalikuwa kwenye dondoo za sensa hiyo? Nani hataamini kuwa huu ni mpango wa ulaji uliobuniwa kwa makusudi kabisa? Je, viongozi wa aina hii, wana uchungu kweli na Watanzania wenzao wanaotaabika? Mv Ulaji itazuiwa lini kusafiri?
Nimetoa mfano huu kuonyesha kuwa si kweli kwamba nchi yetu haina uwezo wa kumaliza tatizo la ujambazi magharibi mwa nchi yetu. Uwezo huo upo. Tena ni mkubwa kuliko mahitaji.
Wakati kina Tossi, Kanali Mfuru, Kanali Simbakalia, Luteni Kanali Mzurikwao na wengine wakipewa dhima ya kuwashughulikia majambazi, tunapaswa kujiuliza maswali kadhaa.
Nini maana halisi ya neno mkimbizi? Je, kwa tafsiri hiyo, Tanzania ina wakimbizi? Tujiulize.
Kamusi:
Mkimbizi: 1. Mtu akimbiliaye nchi nyingine kutokana na vitendo vya kidhalimu au vita. 2. Mtu mwenye tabia ya kukimbia mahali anapotakiwa awepo.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la II (Oxford).
Wanyarwanda walipoingia nchini mwaka 1994 kutokana na mauaji ya kimbari, walistahili kuitwa wakimbizi, kwa sababu wanakidhi maana ya kwanza iliyotolewa kwenye tafsiri ya neno mkimbizi.
Kadhalika, Burundi nao wakati wakipigana na kuchinjana wenyewe kwa wenyewe kama kuku, walistahili kupokewa, kuhudumiwa na kutunzwa kama wakimbizi.
Je, baada ya Rwanda kuwa nchi inayoendeshwa kidemokrasia, baada ya Burundi kuwa na kiongozi aliyechaguliwa na Warundi wenyewe, bado kuna sababu ya watu wa mataifa hayo kuishi kama wakimbizi katika ardhi ya Tanzania?
Hawa waliopo Kigoma, Kagera na kwingineko magharibi mwa nchi yetu, si wakimbizi. Wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hao ni wakimbizi, lakini siku si nyingi, nao tutawaomba warejee kwao.
Warundi na Wanyarwanda ni watu wenye tabia ya kukimbia mahali wanapotakiwa wawepo.
Hawa wako kwenye tafsiri ya pili ya neno mkimbizi. Wanastahili kwenda kwao ili Watanzania wapumue. Wamemaliza wanyama na misitu, sasa wameingilia maisha ya raia wetu. Watatumaliza hawa.
Wamebweteka. Wanaponda maisha. Wapo walionunua magari. Wapo wenye daladala, lakini ni wakimbizi wanaoishi makambini. Wapo wanaishi kama wafalme walioandikwa kwenye vitabu vitakatifu.
Tujiulize, ukwasi wote huu wanautoa wapi katika ardhi isiyokuwa yao? Wana biashara gani? Je, si kweli kwamba hawa ndio wafadhili wa ujambazi na uhalifu mwingine?