Mchezo mchafu watikisa TANROADS
Vigogo wapoka mradi wa mkandarasi
na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Barabara nchini (TANROADS), inadaiwa kupata hasara ya mabilioni ya shilingi baada ya kupoka mradi wa ujenzi wa barabara ya Dodoma - Manyoni uliokuwa ukitekelezwa na Kampuni ya ujenzi ya Konoike.
Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata, zinaeleza kuwa kupokwa kwa mradi huo kutoka kwa Kampuni ya Konoike kumeisababishia TANROADS kulipa sh bilioni 30.1, kinyume cha utaratibu.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya TANROADS, vimeeleza kuwa uamuzi wa uongozi wa juu wa TANROADS wa kuuondoa mradi huo kwa Kampuni ya Konoike una kila dalili za shaka, kwa sababu ukaguzi wa ujenzi wa barabara hiyo unaonyesha kuwa mkandarasi alikuwa akitekeleza kazi yake sawasawa.
Mmoja wa viongozi wa juu wa TANROADS, aliliambia gazeti hili kuwa uamuzi huo ulichukuliwa na bosi bila kushirikisha bodi zinazohusika na kuikabidhi kampuni nyingine ya ujenzi ambayo gharama zake za ujenzi kwa kilometa ni za juu kuliko za Konoike.
Sote tunashangaa jinsi mkubwa alivyochukua uamuzi huu, tulisikia tu kuwa mradi huo umepokwa kutoka kwa Konoike na kupewa mkandarasi mwingine. Maamuzi yalichukuliwa bila kufuata taratibu na hatujui Konoike walikosea nini, kwa sababu walikuwa wanatekeleza ujenzi kwa mujibu wa mkataba wao.
Cha kushangaza zaidi ni taarifa tulizopata kuwa mkandarasi mpya analipwa sh bilioni 1.4 kwa kila kilomita anayojenga, wakati Konoike alikuwa analipwa sh milioni 820.5 kwa kila kilomita, kilisema chanzo hicho cha habari.
Habari zaidi zilizopatikana zinaeleza kuwa wakati Konoike wakipokwa mradi huo, walikuwa wamekwisha kujenga kilomita 110 kati ya kilomita 127 zilizomo katika mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo.
Zinaeleza zaidi kuwa kampuni mpya iliyopewa mradi huo imelipwa sh bilioni 30.1 badala ya sh bilioni 13.9, jambo linalodaiwa kuzua maswali ya kuwapo dalili za rushwa katika ubadilishaji wa mkandarasi wa ujenzi huo.
Unajua, hawa Konoike wana kiburi, wanalingia ubora wa kazi zao, sasa wakubwa walitaka wawape chochote, wakakataa, ndiyo yakatokea haya. Lakini swali kubwa tunalojiuliza, hizi sh bilioni 16.8 zilizozidi katika malipo zimekwenda wapi? alihoji mmoja wa watoa habari hizi ambaye jina lake tunalihifadhi.
Barabara hiyo ya Dodoma Manyoni, yenye urefu wa kilomita 127, ilianza kujengwa na Kampuni ya Konoike Machi 14, 2007 kwa gharama ya sh bilioni 63.8.
Desemba 16, 2008, TANROADS ilisitisha mkataba na Konoike wa kujenga barabara hiyo na kuteua kampuni nyingine ambayo zabuni inadaiwa kutowekwa wazi.
Akipoulizwa kuhusu madai hayo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Ephraem Mrema, alikiri kulifahamu jambo hilo na kueleza kuwa anaweza kuliongelea kwa kina akiwa katika hali nzuri. Unajua sipo katika hali nzuri, suala hili kweli lipo, lakini si kubwa kiasi hicho, linaweza kurekebishwa tu. Ni makosa madogo madogo ambayo sijui hata kwenu yamefikishwa na nani. Hapa nilipo siwezi kusema lolote. Lakini naandaa majibu, nitayatoa kwa waandishi wa habari, alisema. Aliongeza kuwa suala hilo litapatiwa ufumbuzi na ofisi yake, kwa sababu ina uwezo wa kubatilisha chochote kilicho chini ya uwezo wake kama kilifanyika kimakosa.