Ulaya: Mawaziri wa EU waimarisha maandalizi ya kupambana na virusi vipya
Mawaziri wa Afya wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana Jumatano (13.02.2020) kuimarisha maandalizi na kuweka mpango wa pamoja wa kuvizuia virusi vya corona ambavyo vimezuka nchini China dhidi ya kusambaa zaidi kote Ulaya.
Katika mkutano wa dharura mjini Brussels, maafisa kutoka mataifa 27 wanachama wa umoja huo wamesema wanahitaji kupanga zaidi ili kuepuka uhaba wowote wa madawa au vifaa ya kujikinga wakati wa mripuko huo, ambao Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limesema ni tishio kwa afya ulimwenguni.
Kwa mujibu wa maafisa wa afya wa China, mripuko huo umewaambikiza watu 53,000 kote duniani na kuwauwa zaidi ya 1,300 ambapo asilimia 99 vimetokea China. Watalaamu wanaamini idadi halisi ya visa vya mripuko huo huenda vikawa juu zaidi. [DW]