SEHEMU YA 10
Mzee Linus alikuwa amejiinamia, kichwani mwake akiwaza mambo mengi, kifo kile cha kijana wake kilimuumiza sana, lakini alimshukuru Mungu kwa kila jambo. Kama aliyekumbuka kitu, akamshika mkono mzee Komba na kumnong’oneza jambo!
SASA ENDELEA…
“Kaka!”
“Niambie,” Mzee Komba alimuitikia rafiki yake, kichwa chake kikiwa na mawazo mengi.
“Hivi nini kitatokea kwa Bap?” aliuliza tena
“Kivipi?” naye akajikuta akiuliza.
“Hii kwake itakuwa ni kesi ya mauaji au kitu gani,?”
“Sidhani, ni traffic case,” alisema mzee Komba.
“Ila itabidi lazima tumwambie Bap, tabia yake ya kuendesha gari kwa kasi si nzuri, atamgonga mtu sehemu wasiyomfahamu, wanaweza kumfanyia kitu kibaya sana,” alisema mzee Linus.
“Kila siku ninamkataza, lakini hasikii. Kuna wakati niliamua hata kumzuia kuendesha gari, lakini nikashindwa, hebu tumuache, tuamini kwamba atabadilika mwenyewe, hasa baada ya tukio hili.”
“Lakini hatujafuatilia Polisi, nini kimemtokea?”
“Amewekwa mahabusu, katika jambo kama hili, hatuna sababu ya kuhangaika hivi sasa, hebu hili tulijadili kesho, mwache alale leo,”
Watu wakaendelea kujaa pale nyumbani kwa mzee Komba, msiba ulikuwa wa ghafla sana. Mama yake Tonny baada ya kuambiwa aliyemgonga na kumuua mwanawe ni Bap, akili yake ikachanganyikiwa. Mambo mengi yalipita kichwani mwake, akajikuta akihusisha tukio hilo na kile kilichotokea mwaka mmoja na nusu uliopita!
“Atakuwa amefanya makusudi?” alijiuliza, lakini sauti asiyoifahamu, ikamtaarifu kuwa ni bahati mbaya, naye kwa moyo mkunjufu kabisa, akainua mikono yake juu akimshukuru Mungu na kumuombea Baptist!
Baada ya kuwasiliana na ndugu zake wa karibu ambao walikuja msibani pale siku ile ile, mzee Komba akawatangazia majirani na waombolezaji wengine kuwa mazishi ya mtoto wake yatafanyika siku tatu baadaye, wakisubiri watu wengine waliokuwa nje ya Dar es Salaam wafike. Hakutaka kwenda kumzika mtoto wake nyumbani kwao Mbinga, alitaka azikwe Dar kwa kuwa ndipo yalipo maisha yake!
Asfat aliwasili Dar es Salaam saa tano na nusu asubuhi, akakodi teksi iliyomtoa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kumfikisha Nakasagwe saa saba mchana. Alipokelewa kwa vilio kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki. Baada ya kuingiza begi lake chumbani kwake, akaingia bafuni na alipomaliza kuoga, akamfuata mama yake na kumuomba waongee kidogo.
Wakatoka nje kabisa ya nyumba, ambako watu walikuwa wametapakaa. Wakatafuta eneo la peke yao, wakakaa chini ya matofali na kuanza kuzungumza. Asfat akamtaka mama yake amueleze ukweli juu ya tukio lile, kwa sababu alimwambia wazi kuwa yeye binafsi, haamini kama ile ilikuwa ni ajali kama ajali zingine.
Mama akamtazama, macho yake yakaanza kujaa machozi, akajifuta kwa khanga aliyokuwa amejifunga na baadaye akamwambia;
“Hata mimi mwanzo nilikuwa na mawazo kama yako, sikuamini mara moja, lakini kadiri nikirejea tukio zima, sioni ni wapi Bap alikusudia. Kama kuna mtu wa kumlaumu, nilaumuni mimi, nisingemfukuza, asingetoka nje.”
Kwa mara nyingine, Asfat akakubali, lakini hakuridhika!
Baada ya kumaliza mazungumzo hayo, akarejea chumbani kwake, akaikumbuka albamu yake ya picha, akaichukua na kuanza kuziangalia picha zake, zikiwemo za zamani enzi za utoto hadi ukubwani.
Akakutana na picha aliyoipenda sana, alikuwa amepiga na marehemu Juddy, wakati flani wa sikukuu ya Krismas, miaka kadhaa iliyopita, aliipenda picha hiyo kwa vile ilimkumbusha mambo ya siku hiyo, ambayo hawezi kusahau.