Napenda kuwakumbusha Watanzania, Mataifa ya Ulaya na Marekani huwa hayakurupuki kutoa shutuma, ukiona wanatoa tamko ujue wana uhakika. Walieleza juu ya meli za Iran kutumia bendera ya Tanzania, Membe alikurupuka kukanusha kama kawaida yake, baadaye ikadhihirika ni kweli.
Mataifa ya Ulaya yalitishia kusimamisha misaada kutokana na ufisadi wa Richmond, kwanza serikali ilikanusha baadaye ilidhirika kuwa ni kweli kulikuwa na wizi.
Mataifa ya Ulaya yaliwahi kuelezea ufisadi katika manunuzi ya radar, serikali ikatoa maelezo marefu kuonesha hakuna ufisadi, baadaye ikadhihirika ni kweli.
Sasa wametoa tamko kuwa hakuna msaada kutolewa kwa Tanzania mpaka waone taarifa ya CAG kuhusu ufisadi katika akaunti ya Escrow, serikali imekanusha hakuna ufisadi.
Vyombo vya habari vya Ulaya vimeeleza kuhusu kuhusika kwa serikali ya Tanzania, CCM na China katika biashara haramu ya pembe za ndovu, Membe kama kawaida yake amekurupuka kukanusha lakini mambo hayo yote yatakuja kudhihirika kuwa ni kweli kwa 100%.
Taarifa ya Escrow ipo tayari lakini yaliyomo ndani ni balaa maana ni zaidi hata ya wananchi walivyokuwa wakiitegemea.
Hii iliyopo chini ni kama tetesi lakini ni tetesi yenye uhalisia. Endeleeni kufuatilia kashfa hii kubwa inayogusa ofisi kubwa zote za nchi.
______________________________ ______________________________ ____________
Ikiwa ni siku chache tangu Baraza la Usalama la Taifa kukutana na kupitia ripoti ya uchunguzi ya PCCB kuhusu ufisadi wa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwenye akaunti ya Tegeta escrow Benki Kuu, Taarifa za uchunguzi zinaeleza kuwa mkurugenzi wa PCCB Dr. Edward Hosea atamkabidhi Mh. Rais Jakaya Kikwete ripoti hiyo Jumatano ijayo kama ilivyoelekezwa na Baraza la Usalama wa Taifa.
Awali ripoti hiyo ilikuwa akabidhiwe Mh. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lakini taarifa za ndani zinabainisha kuwa uzito wa ripoti hiyo unastahili Mkuu wa nchi mwenyewe kwani kuna maeneo ambayo Waziri Mkuu atastahili kuwajibika.
Ofisi nyingine zilizohusika kwenye ufisadi huu kwa mamlaka yao ni Wizara ya Fedha, Benki Kuu, TANESCO, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TRA, na baadhi ya vigogo Ikulu.
RIpoti hiyo imekwenda mbali zaidi kuonesha baadhi ya majina ya watu maarufu waliojipatia fedha hizo kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, akaunti ya kampuni ya VIP Engineering katika Benki ya Mkombozi iliyopokea hela za escrow imekutwa hela nyingi zimetoka kwenda kwa Wabunge,Mawaziri Majaji, na baadhi ya watu maarufu (hii ni kwa mujibu wa benki statement ya akaunti hiyo yenye kurasa 27 kuanzia tarehe 20 Januari mpaka tarehe 14 Agosti 2014).
Baadhi ya majina ndani ya benki statement hiyo yalitumiwa pesa kupitia akaunti hiyo ni pamoja na Waziri Anna Tibaijuka, Waziri wa zamani William Ngeleja, Mwanasheria Mkuu wa zamani Andrew Chenge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na mmoja wa Majaji wa mahakama kuu ya Tanzania Mujulizi. Katika orodha hiyo kuna Wabunge, wajumbe wa kamati ya Nishati na Madini, wote isipokuwa mmoja tu ambaye ni mtumishi mwandamizi wa zamani wa Serikali. Viongozi wawili wakuu wa vyama vya siasa vya upinzani nchini wameonekana katika orodha hiyo pia.
Juhudi kubwa zinafanywa hivi sasa kuzuia taarifa ya CAG na PCCB isikabidhiwe Bungeni kwani kama itakuwa wazi inaweza kusababisha kuibuka kwa mtikisiko mkubwa.