Waufukweni
JF-Expert Member
- May 16, 2024
- 5,383
- 18,776
Kwa mujibu wa familia na rafiki wa karibu wa marehemu, aitwaye Pati, Nestory alionekana akiwa na majeraha makubwa kabla ya kifo chake, na alithibitisha kuwa alikuwa ameitwa katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi. Dakika chache baadaye, mlango wa ofisi hiyo ulifungwa kutoka ndani, na baadaye polisi walidai kuwa Nestory alijifungia na kujiua, taarifa ambayo familia imeipinga vikali.
Uchunguzi wa familia katika chumba hicho ulionesha mazingira ya kutatanisha—sakafu ikiwa imelowa damu, pazia zenye madoa ya damu, pamoja na kisu na panga vilivyojaa damu vikiwa karibu na mwili wa marehemu. Hata hivyo, walipouliza polisi juu ya uwepo wa silaha hizo, walijibiwa kwa kejeli: “Sisi sio binadamu? Hatuwezi kutumia hivyo vitu kula matunda?"
Familia ya Majembe sasa inataka hatua kali zichukuliwe. Wameiomba serikali na vyombo husika kuhakikisha uchunguzi huru unafanyika, wakiwataja viongozi mbalimbali wa Jeshi la Polisi na Tume ya Haki za Binadamu kuchukua hatua mara moja.
====================================
FAMILIA YADAI NDUGU YAO KUUAWA MIKONONI MWA POLISI KITUO CHA POLISI TABATA SHULE.
11 Aprili 2025, Familia ya Raphael Majembe imeibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi Kituo cha Tabata Shule kwa madai ya mauaji ya kikatili ya kijana wao Nestory Raphael Majembe, aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi ndani ya chumba cha Mkuu wa Upelelezi wa kituo hicho.
Kwa mujibu wa familia, Nestory, mwenye umri wa miaka 29, alikamatwa usiku wa tarehe 6 Aprili 2025 kwa tuhuma za kuiba simu, na usiku huo alipelekwa mahubusu, huku kesho yake kaka yake na rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Pati walikamatwa na kupigwa vibaya wakidaiwa kuwa marehemu amewataja kuwa wao ndio wana simu, baada ya hapo waliwekwa mahabusu, Pati amesema kuwa huenda marehumu aliwataja wao baada ya kipigo cha muda mrefu huku akilazimishwa kusema simu amempa nani.
Pati ambaye ni rafiki wa marehemu ameongeza kuwa kabla ya kifo chake, alimwona Nestory akiwa amepigwa v kiasi cha kushindwa kutembea akijikongoja akamuuliza anaenda wapi, na marehumu alimjibu kuwa ameitwa ofisi hiyo mpelelezi. Baada ya muda kama wa nusu saa walishangazwa kuambiwa wajaribu kufungua mlango wa chumba alichoingia Nestory ambacho ni chumba cha Mpepelezi huku wakirekodiwa video. Mlango huo ulikuwa umefungwa kwa ndani, jambo lililozua mashaka makubwa.
Aidha, Walipoona mlango haufunguki, polisi wakamwambia mmeona wenyewe kuwa mtuhumiwa kajifungia ndani, baadae walimsulubu kaka wa Marehemu atoke nje aende akachungulie ndani ya chumba alicho Marehemu, na ndipo baada ya kuchungulia aliona kuwa mwili wa mdogo wake umetapakaa damu.
"Haingii akilini mtu aliyekuwa anatambaa, asiyeweza hata kutembea, aweze kujifungia ndani na kujiua," alisema Pati rafiki wa marehemu.
Familia imeeleza kuwa walipoingia chumbani walikuta mazingira ya utata, pazia na sakafu ya ofisi ikiwa imelowa damu, kisu na panga vikiwa na damu karibu na mwili wa marehemu, lakini walikuta alama za kuchomwa na kisu shingoni. Walipouliza kuhusu uwepo wa panga na kisu katika ofisi hiyo, polisi waliwajibu : "sisi sio binadamu? Hatuwezi kutumia hivyo vitu kula matunda na kwanini hamtuamini?"
Ikumbukwe kuwa, Tukio hilo limeripotiwa na familia hiyo mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) leo, ambapo familia ilifika kuomba msaada wa kisheria na jukwaa la kupaza sauti juu ya kifo chenye utata cha ndugu yao.
Aidha LHRC imeahidi kuendelea na ufutiliaji wa karibu wa taarifa hizo na itatoa ripoti mara baada ya kukamilisha hilo.
Chanzo: Haki TV