The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Kazi\ajira ni sehemu muhimu ya maisha ya watu. Ina maana kubwa zaidi ya malipo anayopata mtu. Inamaanisha kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi binafsi kuhusu jinsi anavyotaka kuishi maisha yake.
Hata hivyo, wapo ambao wanakabiliwa na ukosefu wa kazi/ajira za kuwawezesha kiuchumi hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa thamani ya maisha yao.
Duniani kote, idadi ya watu wasio na ajira imefikia kiwango cha juu sana, haswa miongoni mwa vijana. Kwa kuwa vijana wanajumuisha idadi kubwa na inayoongezeka ya idadi ya watu duniani wenye umri wa kufanya kazi, matarajio yao ya ajira huathiri ukuaji wa uchumi wa siku zijazo, katika nchi zao na kimataifa.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), idadi ya vijana ambao kwa sasa hawako katika ajira, elimu au mafunzo (Not in Employment, Education or Training - NEET) inaongezeka, na vijana wa kike wana uwezekano zaidi ya mara mbili ya wenzao wa kiume kuathirika. ILO pia ilikadiria kuwa vijana walio katika kundi la NEET wangefikia milioni 273 mwaka 2021 kutoka milioni 267 mwaka 2019.
Hivi sasa kuna takribani vijana bilioni 1.3 duniani kote, kati yao milioni 267 wameainishwa kama NEET. Milioni 181 ya NEETs ni vijana wa kike.
Ripoti ya ILO pia inaonesha kuwa wale wanaomaliza elimu ya juu wana uwezekano mdogo wa nafasi zao za kazi kuchukuliwa na mitambo. Hata hivyo, wanakabiliwa na masuala mengine kwa sababu kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya vijana wenye shahada kumepita mahitaji ya wahitimu wanaohitajika katika soko la ajira, jambo ambalo linadidimiza mishahara.
Hali ya Afrika
Vijana barani Afrika wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na uchumi unaokua lakini usioweza kutengeneza ajira za kutosha.
Kijana mmoja kati ya watano hawakuwa kwenye ajira, elimu au mafunzo (NEET) mwaka wa 2019; hali hii ya ukosefu wa ajira imekuwa ikiongezeka kwa kasi tangu 2012 ikiakisi mwelekeo wa kiwango cha kimataifa.
Ripoti ya Hali ya Ajira kwa Vijana barani Afrika inasema kiwango cha NEET kilitarajiwa kuongezeka kidogo kwa asilimia 0.3 hadi 20.8 mwaka wa 2021. Vijana wa kike wamekuwa waathirika zaidi wa hali ya NEET na pengo la kijinsia la karibu asilimia 10 tangu 2018.
Hata hivyo, kipengele kimoja cha kufurahisha ni kwamba wakati kiwango cha NEET kwa wanaume vijana kimekuwa kikiongezeka tangu 2012, kile cha wasichana kilipungua kati ya 2012 na 2018.
Upotevu wa nguvukazi
Ukosefu wa ajira kwa vijana ni uharibifu wa nguvukazi ya dunia. Vijana wa leo ndio wanapaswa kuwa watu wa kuendeleza uchumi. Ndio wanapaswa kuwa nyuma ya maendeleo yoyote katika taaluma za sanaa na teknolojia. Hao ndio wabunifu, madaktari, na wawekezaji.
Kiasi kikubwa cha uwezo wa binadamu hupotea kwa sababu ya ukosefu wa ajira, na kila siku, vijana wanadumaa katika ujuzi wao, wanazidi kukosa matumaini na kukosa kujiamini.
Sheria za kazi katika maeneo mengi duniani zinaelezwa kuwa hazina mifumo elekezi kwa waajiri/waajiriwa kutoa fursa kwa vijana.
Watu wasio na uzoefu wana wakati mgumu kuonesha kwanini wanapaswa kuajiriwa badala ya mtaalamu aliye na uzoefu. Lakini, kipaji cha vijana kinaweza kukosa uzoefu, lakini kikaleta ustadi na mbinu mpya kwa taasisi au kampuni.
Tufanye nini?
Serikali, kwa mfano, zinapaswa kuandaa mipango kazi ya kitaifa inayolenga ajira kwa vijana. Ni muhimu kuanzishwa kwa programu za biashara na miradi inayoajiri na kutoa mafunzo kwa vijana. Wanapaswa pia kuhamasisha taasisi za elimu na waendeshaji binafsi kufanya hivyo.
Waajiri wanaweza kubuni nafasi za kazi za ngazi ya awali, kutekeleza mafunzo kutoka shule hadi kazini na programu za mafunzo ya kazini, na pia kusaidia wajasiriamali wachanga kupata ushauri.
Lakini pia, taasisi za elimu zinaweza kujumuisha ujasiriamali katika mitaala na kufanya kazi na waajiri ili kuhakikisha wanawapa wanafunzi mafunzo yanayofaa. ILO inaeleza kuwa ujuzi fulani hauwezi kueleweka kikamilifu hadi ujifunze kupitia mafunzo ya kazi au uzoefu wa mafunzo.
Hatuwezi kuwa tayari kupoteza vipaji hivi au uwekezaji huu katika elimu ikiwa tunataka kukabiliana na changamoto zinazoletwa na teknolojia, mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa usawa na idadi ya watu.
Tunahitaji mifumo jumuishi ya sera na mifumo sikivu ya mafunzo, iliyoundwa kwa kutumia mazungumzo kati ya serikali, wafanyakazi na waajiri.