MZAHA WA DAMU 01
by CK Allan 0746 266 267
“Baba njoo uone amefumbua macho yake! Ameamka! Baba Njoo!” ilikua ni sauti ya mtoto mdogo wa kike ambaye alikuwa akikimbia kutoka nje
Nilijaribu kukaa lakini sikuweza kabisa, mwili wangu ulikua unauma kila sehemu, kila kiungo nilihisi maumivu makubwa sana, nilijaribu kufungua mdomo lakini sikuweza, na sasa nilijaribu kunyanyua mkono, nilijikuta nikiishiwa nguvu!, mikono yangu yote ilikuwa imefungwa vitu vizito na sikuweza hata kujigeuza,
Wakati nikiendelea kujigeuza ghafla niliona mwanaume mmoja akiingia kwa haraka
“ohh Asante Mungu,nilisema mimi hakufa huyu! Nilisema mimi ataamka!” alisema yule mzee kwa haraka akimkumbatia Yule mtoto wake,
“Zawadi, kimbia haraka kamuite mama mwambie unko amezinduka!” alisema sasa Yule mzee huku Yule binti akitoka mbio, niliendelea kuduwaa sana!
Yule mzee alinisogelea huku akitabasamu na kisha akaniinua na kunigeuza upande wa pili ambapo sasa nilijisikia afadhali kidogo na ndipo nikashuhudia majeraha kadhaa mwilini mwangu, kwa ufupi ni kama mtu aligongwa na gari, ama kupondwa pondwa na mawe
Nilijikuta naishiwa nguvu na kufumba macho yangu kujaribu kukumbuka chochote
Nilijikuta sikumbuki chochote na kadri nilivyojilazimisha kufikiri ndivyo maumivu yalizidi
“ah usijali utapona kabisa kijana wangu, utapona kabisa, utapona kabisa!” alisema Yule mzee huku akifungua chupa moja iliyokuwa mkononi mwake na kuweka kwenye kijiko huku akinilisha mdomoni,
Ndipo sasa nikahisi maajabu mengine mwilini mwangu, ndioo
Ladha!, sikusikia ladha yoyote mdomoni mwangu na hivyo sikuweza kujua ni aina gani ya kitu nalishwa!
“loh!” nimekuwaje?
“imekuwaje?’ nilijiuliza maswali mengi bila majibu
Ni wakati huo huo sasa Yule mzee alitoka nje ya kile chumba na kisha baada ya muda aliingia akiwa na mwanamke pamoja na yule mtoto, nilijaribu kukadiria umri wao ulikuwa kama miaka 55 au 60 hivi,
“oooh jamani, Mungu ni mwema! Ooh jamani, kijana wa watu jamani, jamani, jamani!” Yule mama sasa aliongea akinishika nywele zangu kichwani huku machozi yakimtoka
“ah kwa.. kwa… kwa… ni… ah” nilijaribu kuongea lakini mdomo hakuweza kabisa kunyanyuka
Ni kama taya zangu hazikuwa sawa, ni kama taya ya juu ilirudi chini na ya juu ikarudi chini..
“ooh umesemaje! Umeongea!” Yule mzee alishikwa na mshangao mpaka akaangusha chupa yake huku mke wake nae akisimama kwa mshangao!
“ameongea!, ameongea!” walijikuta wakisema kwa pamoja huku wakikumbatiana kwa furaha!
Sasa nilielewa kumbe kuna tatizo kubwa zaidi ya hata hili nililokuwa nafikiria,
Kwa maana hiyo hata kuongea kwangu kumewashangaza sana kama sio kuwafurahisha!
“sasa pumzika kijana! Utapona tu!” alisema Yule mama huku akitoka
“mimi nabaki na anko, mama!” alisema Yule mtoto huku akisogeza kiti na kukaa pale kitandani
“mama yangu alisema umekufa! Lakini baba akasema hujafa, utaamka, baba yangu ndie aliyekuleta ….’
“zawadiii muache anko alale kwanza utamuongelesha baadae!” aliita Yule mama na yule mtoto akaondoka zake
Baada ya wiki moja sasa maumivu yalipungua kwa baadhi ya sehemu za mwili na niliweza hata kujigeuza kitandani pasi na kuwa na msaada, ingawa bado mdomo ulikua hauwezi kunyanyuka na sikuweza kutamka maneno yaliyonyooka,
“tutaangalia namna ya kukufungua huu mkono mmoja kwanza wa kulia maana ni kama umeanza kupona hivi” alisema Yule mzee akinyanyua mkono wangu na kweli maumivu yalikua yamepungua kabisa.
Kesho yake Yule mzee alinifungua vile vipande vya miti ambavyo vilikuwa vimewekwa kwe mkono wangu kwa uangalifu mkubwa kisha akatoa kama mafuta Fulani hivi akaweka kwenye mikono yake na kisha akaanza kuuvuta kunyoosha pole pole,
Nilisikia maumivu makali sana , na kuhisi kama mkono unataka kunyofolewa, lakini Yule mzee aliendelea tu huku nikizidi kupiga kelele Yule mama alishindwa kujizuia alitoka nje, Yule mzee aliendelea tu kana kwamba alikua kiziwi, alipaka yale mafuta na kuendelea kuunyoosha na kadri alivyokuwa akiendelea sasa maumivu yalipungua, na hatimaye yakakaacha kabisa
“loh, huyu mzee mchawi nini!”
niliwaza sasa nikimkodolea macho
Aliniachia ule mkono kisha akanitaka kujaribu kukunja vidole
Vidole vvyote vilikua vinajikunja isipokuwa kidole cha mwisho kidogo
Ambacho kiligoma kabisa
“sasa fanya mazoezi, kumbuka unapona haraka, lakini utapona haraka zaidi kama utaendelea kufanya mazoezi” alisema Yule mzee akifunga zile chupa zake akatoka nje.
Hata mimi nilitaka kupona haraka ili nijue hasa kitu gani kilinitokea, kwa uhalisia sikukumbuka chochote, hata jina langu pia! Hakika sikuelewa kitu gani kinatokea katika maisha yangu, je nilipata ajali? Nilivamiwa na majambazi? Au nilikuwa mwanajeshi nimetoka vitani? Nilishambuliwa kwa bomu? Je hapa nipo wapi? Hawa wanaonihudumia ni akina nani?
Nilijiuliza maswali mengi sana yasiyokuwa na majibu nikajikuta machozi yakinitiririka tu, kila nilivyokuwa nawaza ndivyo ambavyo machozi yalikuwa yanatoka hata hivyo jambo moja ambalo nilikua na uhakika nalo ni kuwa hawa watu walikuwa wamejitolea kunisaidia kwa hali zao na mali zao pengine na kila kitu walichokuwa nacho, je nimekuwapo hapo kwa muda gani? Wiki, miezi, miaka? Nilitamani sana kujua
Nilikumbuka mzee alinihakikishia kuwa ningepona kabisa na kurudi katika hali yangunya kawaida sasa nilisubiri kwa hamu siku hiyo, siku ambayo ningesimama kwa miguu yangu siku ambayo nitaongea kwa kinywa changu, siku ambayo nitaongea kila kitu, siku ambayo nitasimulia kila kitu kilichonikuta na kila kitu kuwa hadharani.."
“ooh usiwaze sana kijana wangu, nakuhakikishia umeshapona, kesho tunafungua mkono mwingine na mguu mmoja” alinikatisha Yule mzee katika mawazo yangu
Nilitingisha kichwa tu kukubaliana nae huku moyoni mwangu nikitoa shukrani za dhati kwa mzee huyu.
Kesho yake asubuhi na mapema mzee alinifungua mkono wa kushoto pamoja na mguu wa kulia, na sasa mikono yangu ilikuwa huru na niliweza kuikutanisha tena pamoja kwa mara kwanza , pamoja na maumivu makali niliyosikia lakini niliona ni bora kuwa katika hali ile kuliko kurudishiwa ile mizigo ya miti, na hivyo nilijikaza kweli kweli, wakati mwingine nilijifanya kutabasamu wakati mzee alipokuwa akinihudumia lakini ningeugulia maumivu makali wakati mzee akiwa ametoka, hata hivyo ilikua afadhali nilikua naweza kuona mguu wangu, pamoja na mikono yangu ikiwa huru, nakumbuka siku ile nililala nikiwa na furaha sana, usiku ule niliota ndoto za ajabu ajabu na mara kadhaa nilistuka na kuamka, sikukumbuka kama niliwahi kuota ndoto kadhaa kwa muda wote nikiwa pale kitandani kama siku Ile!
hata hivyo maumivu yalikua yakipungua kabisa na kesho yake asubuhi niliweza kujigeuza na kukaa kitandani mwenyewe huku nikifanya mazoezi ya kukutanisha mikono na kuinyoosha, bado mdomo haukuweza kutoa maneno ya kueleweka ingawa nilijitahidi kabisa kuhakikisha yanatoka
Baada ya mwezi mmoja hivi ....
niliweza kusimama na kuchechemea na kutoka nje kutazama jua na kurudi ndani, sio hivyo tu bali niliweza kushika kikombe cha uji na kunywa mwenyewe, sasa ningeweza kutoka kwa kuchechemea kuzunguuka nyumba kisha ningerudi ndani bila kuwa na msaada wowote, na nilikuwa naelewa mazingira yale niliyokuwepo yalikua maeneo ya porini kabisa na sikuweza kuona nyumba yoyote zaidi ya shamba kubwa ambalo limezunguuka ile nyumba, pamoja na hayo kulikua na uzio wa seng’eng’e ambao ulizunguushiwa nyumba yote, pamoja na kuwa nyumba hii ilikua porini lakini ilikua imejengwa kisasa kwa mbao imara na kwa namna ya ujenzi wa Kijerumani hivi, na kisha kulikua na umeme wa jua ambao ulileta mwangaza katika nyumba hii, mzee huyu pia alikua na piki piki yake aina ya watco ambayo alitumia mara kadhaa kwenda kuchukua mahitaji mbali mbali...
Siku hiyo alikuja Yule mzee akiwa na furaha sana alikuja na kiboksi kidogo hivi na kukifungua kilikuwa na vidude vya plastiki hivi na kisha akanitaka niweke mdomoni na kingine nikafunga kwa juu kwenye kidevu,
Aliniambia natakiwa kuvaa kila siku labda nivitoe tu wakati wa kula tu!
, ni kweli vifaa vile vilikua vinavuta taya zangu na kuweka mdomo katika hali ya kawaida na nikaanza kutoa maneno mawili , matatu, sentensi na hatimaye ndani ya mwezi mmoja mwingine nikaweza kabisa kuongea ingawa kwa pole pole hatua kwa hatua lakini niliweza kufanya mazungumzo kabisa na kueleweka, hakika Mungu ni mwema sana na hatimaye nilikua naelekea kupona kabisa na sasa niliweza kutambua jina la wenyeji wangu hawa yaani mzee Tito na mkewe Imelda, hakika walikuwa ni watu wema sana hawa watu,
Hata kama walikuwa wameshiriki kwa namna yoyote kunifanya hivi nilivyo bado ningeweza kuwasamehe kabisa makosa yao kwa jinsi walivyonihudumia kwa namna ya pekee na kunijali kabisa bila shaka kuna mengi zaidi nataka kujua kuhusu watu hawa, hata hivyo kwasasa nilikuwa na jambo moja tu,
Mimi ni nani na nimetokea wapi? Na kwanini niko hivi nilivyo leo? Wakati mwingine nilikuwa naogopa hata kumuuliza mzee Tito kuhusu asili yangu
“isije kuwa Mzee Tito na mama Imelda ndio wazazi wangu mimi! , halafu nikawauliza kuhusu hili jambo nikazidi kuwatia simanzi” yalikuwa ni mawazo katika hisia zangu,
Hata hivyo sikuwa na namna nyingine zaidi waswahili walisema njia rahisi ya kujua jambo ni kuuliza, na mimi sikuwa na njia nyingine isipokuwa kuuliza, kwahiyo nilisubiri mpaka kuhakikisha mwili wangu umeimarika kabisa ili niweze kuanzisha safari nyingine ya kujitambua!