Hadithi: Sitosahau alichonifanyia daktari wa saratani ya matiti

Ohoooo
 
SITOSAHAU ALICHONIFANYA DAKTARI WA SARATANI YA MATITI
SEHEMU YA KUMI NA TANO
TULIPOISHIA
“Nina miaka minne tangu nije hapa Tanzania nimefanya kazi na hii familia kwa utiifu mkubwa, lakini hawajawahi kunilipa pesa, kiukweli nakula vizuri navaa vizuri lakini hata nyumbani sijawahi kuwatumia chochote, ninadai zaidi ya milioni sita za mshahara lakini pia nilitamani wanipe hata hela kidogo mwishoni mwa mwaka huu niende nikamuone mama anaumwa, ila wao hawaonyeshi kunijali, nimepamiss kwetu sana”

“Mh…kweli??” nilimuuliza

“Ndio”

“Oh pole sana my dear….”

“Asante” alisema “Kwa hiyo wewe usiwe na wasiwasi kwamba mimi natoka naye hapana, sina hata ratiba hiyo mimi ya kuwa naye usijali….” Aliniambia

ENDELEA
Baada ya maongezi yale Jacque aliniaga na kuondoka zake huku akiniacha mimi nikiwa njia panda sijui kama ni kweli hayupo na yule mtu au yupo naye kimahusiano. Niliketi nikawa nawaza mambo mengi sana, mahusiano ni kitu kigumu kwangu kuamua.

Nikiwa nawaza kama dakika kumi hivi, ndipo nilipopokea tena simu kutoka kwa Hemed, nikaongea naye, akaniuliza

“Umeshaamini kwamba sipo naye??”

Nikamuambia “Nikaamini kivipi”

“Si amekuambia mwenyewe sipo naye?” alisema

“Khaaa” nilishtuka sana nikafikiria haraka haraka nikahisi labda ndiye aliyemtuma kuja kuniambia hivyo ili nimkubalie, hivyo nikamuambia “Kwa hiyo umemtuma aje kuniambia hivyo ili nikukubali unioe??”

“Hhahahaa…hapana bwana….ni kwamba ninajua amekuja hapo”

“Sawa….nyie endeleeni na mapenzi yenu mimi sina shida”

“Kiukweli Pendo nakupenda kama jina lako lilivyo, lakini wewe hupendeki sijui unanionaje, hivi unadhani ningekuwa mimi nipo naye kwenye mahusiano ningeweza kukupeleka hadi nyumbani??” aliniambia ni kweli maneno yalionekana ya kweli, ila mbona nilikuwa nimeambiwa na majirani

Nikamuuliza “Mi nitajuaje ulitaka kumkomoa tu”

“Hapana pendo, naomba ulifikirie hili….nimeshamuambia mama kwamba nina mchumba mpya nitampa namba yako atakupigia muongee basi”

“Mh tena??” nilimuuliza

“Yeah ndo hivyo….”

“Usimpe kwanza” nilimuambia

“Nishampa”

“Ah bwana” nilisema lakini kadri nilivyokuwa nazidi kusikia maneno yake nilijikuta nazidi kumuamini zaidi

“Nini??? Halafu vipi maziwa bado yanauma??”

“Hapana hayaumi”

“Okay, basi nitafanya mpango nije niyawekee dawa nyingine ili yasije yakaanza kukuuma tena” alisema maneno ambayo yalilileta tabasamu langu

“Dawa gani?” nilimuuliza

“Dawa ile niliyokupa siku ile”

“Hahaha….acha mambo yako, mimi sina mpango na hayo mambo yako” nilisema lakini nikamsikia kama anamkaribisha mtu na kukata simu, nafikiri alikuwa bado yuko hospitalini kama daktari.

Niliendelea kukaa nikiwaza mambo mengi, ila ghafla nikiwa katikati ya msongo wa mawazo simu yangu iliita na ilikuwa ni namba mpya, nikapokea

“Hallo” nilisema

“Hallo..mwanangu hujambo??” sauti ya kike iliyoonekana kuwa ya mtu wa makamo ilisikika upande wa pili

“Sijambo nani?” nilimuuliza

“Nimepewa namba hapa na mtoto wangu wa mwisho anaitwa Hemed, ameniambia wewe ndio mkwe wangu” aliniambia maneno ambayo yalinishtua kidogo, sikuamini kwamba Hemed yupo serious na mimi kiasi kile

ITAENDELEA
 
SITOSAHAU ALICHONIFANYA DAKTARI WA SARATANI YA MATITI
SEHEMU YA KUMI NA SITA
“Oooh mama…shikamoo” nilisema kwa uoga huku nikianza kutokwa na kajasho kembamba, sikuwahi kuongea na mkwe kabla

“Marahaba…uko wapi mwanangu”

“Niko kazini kazini kwangu mama”

“Haya sawa mwanangu….aaah aliniambia kuhusiana na suala lenu la kutaka kufunga ndoa lakini sijafahamu kwamba mtakuja lini huku”

“Mmh......Sijajua ila tutakuambia mama”

“Hamna shida mwanangu karibuni sana….sana sana” alisema kwa ukarimu wa hali ya juu nilijikuta naanza kupangawa.

Baada ya mama kukata simu nilijikuta nachukua kitambaa na kujifuta jasho, nikasema “Eyuiiiiw” nikiwa navuta pumzi ndefu na kuiachia kama Tom wa kwenye Tom and Jerry.

Haikuishia hapo, jioni nilirudi nyumbani nilipofika nyumbani nilimkuta baba akiwa anaangalia TV Sebuleni, nikamuamkia kisha nikapita zangu kuelekea chumbani.

Nilipomaliza nilivua nguo nikaingia bafuni na kuoga, baada ya kuoga nikaenda jikoni ambapo nilimkuta mama akimalizia kuaandaa chakula cha usiku, nikamuamkia pia tukaongea maneno machache halafu na mimi nikaenda sebuleni kuungana na baba kwenye taarifa ya habari.

Katika kuangalia taarifa ya habari muda mrefu baba akaniuliza “Hivi unafahamianaje na Doctor Hemed”

Lilikuwa swali la mshtuko lililoudundisha moyo wangu puuuh lakini nilikausha kama vile sijasikia, ndipo akasema “Si naongea na wewe Pendo?” nikamgeukia na kumuuliza

“Mimi??”

Akasema “Ndio kwani tupo wangapi hapa?”

Baba yangu alikuwa amezoea kufoka, si unajua maaskari wa nchi yetu hii, ndipo nikamuuliza “Kwani umeniulizaje baba?”

Baba akasema “Nimekuuliza mnafahamiana vipi wewe na Doctor Hemedi Kwio??”

“Hemed Kwio??? Ndiyo yupi?” nilijifanya sielewi anachoniuliza lakini nilikuwa nimeshamsoma muda mrefu

“Kuna daktari mmoja anafanya kazi katika hospitali Aga Khan… hamfahamiani?”

“Mh…anaitwa Ahmed umesema?? Yupo yupoje??” niliuliza kumchora zaidi ili asiifahamu dhambi ambayo nimeitenda na dakta huyo

“Anaitwa Hemedi Kwio, ni kijana mmoja mchangamfu sana ambaye anaonekana mtu wa mazoea ni mkakamavu sio mrefu sana lakini ni mweupe anapenda kunyoa funk” aliniambia nikajua ndo yule yule

“Mh…kama vile namfananisha na doctor mmoja juzi alinipa matibabu pale…..” kabla sijamaliza sentensi mzee akasema

“Anyway, ni kijana mstaarabu sana, nilijua mnafahamiana maana naona ananiita mkwe, kumbe ni utani tu” alisema mzee

Nilijikuta natabasamu kwa sababu niliona kama kuna mchezo nachezewa na Hemed, mara Jacque aje ofisini, mara Mama yake anipigie, mara baba amsifie, kiukweli sikujua anataka nini kwangu.

“Haha…labda anakutania tu…sina mazoea naye” nilikana

“Mh okay….lakini kaa makini anaweza akawa anamaanisha kitu, ana wanawake wengi kama mtu akiwa naye basi avumilie, au aweze kumdhibiti awe wa kwake peke ake….japo sio kijana mbaya ana pesa nyingi kwenye sector zingine”

Nilitulia kimya, ila baada ya muda niliamua kuificha aibu yangu kwa kuingia chumbani nikaenda kujipumzisha na kuamua kumtafuta kwa message za kawaida

“Hello mambo Hemed”

Naye akajibu “Safi mke wangu uko poa?”

“Niko poa, lakini nashindwa kuelewa”

“Nini??”

“Baba yangu amejuaje ninatoka na wewe??”

“Anajua kwa sababu nimemuambia nataka nikuoe, kwanini lakini hutaki nikuoe Pendo??”

“Hemed, nimeshakuambia usubiri tujuane, sasa mambo gani inakuja kumuambia baba yangu kwamba nipo na wewe unajua nimejisikia aibu kiasi gani??”

“Samahani kwa hilo ila nimemchana ukweli mimi nakuja kutoa posa”

“Acha hizo, mimi sitaki bwana…tena nitakublock” nilikuwa nimekasirika sana kwa sababu hakukuwa na sababu ya msingi kumuambia baba yangu wakati bado tuko kwenye ugomvu kuhusiana na Jacque hatujamaliza mambo halafu yeye analeta ujinga mwingi, nilikasirika sana.

Niliamua kumzuia (block) kwenye WhatsApp na kwenye simu za kawaida pamoja na jumbe fupi, halafu nikatulia zangu kimya.

Kesho yake asubuhi nilipoenda ofisini nilikuwa nimeshikilia pochi, simu yangu ilikuwa ndani ya pochi ndipo nikamkuta Hemed amesimama kando ya barabara kaegemea gari yake iliyokuwa pale. Alinitazama akatabasamu.

Mimi nikafungua duka nikaingia ndani akanifuata
“Wewe mbona umeniblock?” alinifokea

“Nini?” nilimuuliza “Umeamka na mimi mbona unanifokea asubuhi asubuhi?”

“Tatizo unaringa Pendo….”

“Naringa nini baabu?? Embu niache nifanye kazi zangu usiniharibie siku mimi” nilijikuta nina hasira za ajabu na hata sikujua jeuri hiyo mimi ninaipata wapi….

“Simu iko wapi??” aliniuliza

“Sina” nilimjibu kwa hasira

“Imekuwaje? Umeharibu au?” aliendelea kuniongelesha kwa sauti nyepesi yenye kuonyesha kujali lakini nilikuwa na hasira bado

“Unaniuliza nini. Nimeipasua maana sitaki usumbufu mimi acha nikae niinjoy maisha yangu”

Hemed alisogea anataka kuingia dukani lakini nikampa onyo “Ninaomba usiingie huku ndani, sikuhitaji sikutaki sikutaki sikutakiii uwiii” nilisema maana kila nikikumbuka maneno ya baba kwamba ana wanawake wengi ndio kabisa nilikuwa nachokaaa na kumchukia.

“Okay basi poa samahani kama mimi ndio nimepelekea wewe kuharibu simu yako, naomba unisamehe sana”

“Haya ondoka sasa” nilisema

“Ok”

Hemed bila kipingamizi aliondoka zake na kuniacha nikiwa peke yangu pale dukani, sikuwa na shida kwa sababu simu yangu nilikuwa nayo ila ni njia tu ya kumkwepa mwanaume yule mara baada tu ya kusikia taarifa kwamba anapenda wanawake

Mimi sikuhitaji niwe na mwanaume ambaye anapenda wanawake wengi, mapenzi kwangu ni wivu mkubwa na ndiyo maana hata niliachana na yule mwanaume wangu wa kwanza.

Mchana ulipofika jua lilikuwa ni kali sana, yule Farida ambaye alikuwa amepanga kwa Hemed alinifuata ofisini, akaniambia
“Shoga nililipenda sana hili gauni, naomba unisaidie kwa shilingi elfu ishirini na mbili nimejichanga sana”

“Mmmh…kweli?” nilisema huku nikiliangalia gauni lenyewe

“Ndio, nimelipenda sana ikabidi nirudi tu wasije wakaliwahi”

“Mh sawa” nilisema huku nikijaraibu kuuvuta mdoli nitoe ngo hiyo, halafu nikamuuliza swali “Hivi kweli Hemed anatoka na Jacque?”

Farida akajibu “Mh sifahamu ila kuna tetesi hizo, sijui lakini….ila nikuambie kitu shoga angu?” aliuliza

“Niambie”

“Yule mwanaume anakupenda, hajawahi kumleta mwanamke nyumbani, kila siku anakuongelea, kama inawezekana, ishi naye, pia ni mwanaume mwenye pesa na anajua kujali sana”

“Kweli?” niliuliza na kumpatia gauni

“Kweli rafiki yangu”

“Kwani anafanya biashara gani nje na udaktari?”

“Ana biashara za madini pia, sijui anafanyaje ila amini tu ana pesa nyingi, ningepata hiyo nafasi mimi nisingeichezea kabisa” alisema mwanamke yule halafu akanipatia pesa alizokuwa amezitoa kwenye mkoba.

“Tatizo nikimuambia asubiri tuchunguzane hataki”

“Achana na kuchunguzana, kama ni wako ni wako tu….kama sio wa kwako hata mchunguzane miaka kumi bado utakuja kugundua sio wako….wewe kubaliana naye na naamini utanishukuru baadaye.

“Mmmh”

“Ndio…halafu kitu kingine yule anaharakisha kwa sababu umri umeenda hana mke, anatamani kuwa na familia kubwa, mwanamke aliyezaa naye anajisikia sana kwa sababu naye ana maisha na anaonekana kupenda zaidi maisha ya bata kuliko kujali mahusiano”
JE KWA USHAWISHI HUU BINTI ATACHOMOA? USIKOSE UKURASA WA 17

Hadithi fupi!
SITOSAHAU ALICHONIFANYA DAKTARI WA SARATANI YA MATITi
UKURASA WA KUMI NA SABA

Nilibaki nikiwa nawaza sana, na hata baada ya Farida kuondoka bado nilikuwa nikimuwazia Hemed, nilijihisi sihitaji kumpoteza licha ya kumuhisi sio mwanaume anayenifaa kwenye ndoa.

Niliendelea na majukumu yangu ya muda wote mpaka ilipofika jioni nikarudi nyumbani, nilipofika nyumbani nilimkuta mama akiwa amekaa sebuleni huku akiwa anaongea na mtoto wa anko ambaye alikuwa amekuja kututembelea nyumbani akitoka mkoani Shinyanga.

Nilisalimiana nao kisha nikaingia chumbani kwangu, kama ilivyokuwa ada nilikuwa nikifika nyumbani lazima nijiandae kwa kuoga, nikavua nguo zangu nikawa nimejifunga kitenge. Ghafla nikagongewa mlango ngo ngo ngo

“Nani? Ninavaa” nilisema

“Mi mama shika” aliniambia huku akifungua mlango na kuingiza mkono ndani ya chumba ukiwa umeshika box la simu mpya iPhone 13 pro max. nikashtuka kidogo na kusogea mlangoni.

Kwa kuwa nilikuwa nimejifunga khanga nilifungua mlango na kutazama nje nikamkuta mama ameshika lile box nikamuuliza “Ya nini??”

Mama akaniambia “Ameleta kijana mmoja hapa, mweupe mwenye ndevu nyingi, nafikiri nilishawahi kumuona mahali….amesema ni mchumba ako”

Baada ya kusikia maneno haya nilijua dhahiri ni Hemed lakini nilijifanya kama nashtuka yaani simfahamu “Mh wa wapi huyo?” niliuliza huku nikilipokea lile box

“Usijifanye humjui…ila kaa makini” aliniambia mama halafu akaondoka zake, alionekana anatamani na mimi mwanae nipate mtu wa kunioa lakini ndio hivyo nilikuwa sijapata.

Nilirudi ndani nikaketi kitandani, siamini, ni ndoto ya miaka mingi mimi kutamani kumiliki simu aina ya iphone lakini sikuwa na uwezo wa kumiliki simu hiyo, sasa ilikuwa imejileta yenyewe.

Nilifunua lile box kisha nikathibitisha kweli ilikuwa ni simu mpya kabisa, nilipata wazimu, ndipo nikachukua simu yangu na kuamua kumu-unblock Hemed halafu nikampigia

Hemed alipokea

“Hello mrembo” aliniambia

“Vipi doctor?” nilimuuliza

“Poa, umekuta mzigo nimemuachia mama yako hapo nyumbani?” aliniuliza moja kwa moja

“Mmmh….wewe ndiye umeleta?”

“Ndio, kwani hajakuambia ni mimi?”

“Mmh amenipa tu maelezo machache lakini nikajua ni wewe…”

“Okay samahani, niliumia sana uliposema kwamba ulipasua simu yako kwa ajili yangu, ndio maaa nimeamua kukununulia nyingine ili usinichukie”

Hemed alikuwa anaongea kwa hisia, alionekana ananijali sana, lakini sasa daaah tabia zake.

Nilijishangaa naanza tena kumpenda ghafla, ni mwanaume ambaye kila mwanamke angetamani kuwa naye katika maisha.

Nikamuuliza “Kwanini umemuambia mama kwamba mimi ni mchumba wako?”

Hemed alicheka sana halafu akaniuliza “Kwani wewe ni nani wangu?”

Nilishindwa hata kumjibu, nilijikuta nabaki kimya nikiwaza ndipo akaniuliza tena

“Eti mimi ni nani yako pendo?”

“Mi sijui” nilimjibu halafu nikatulia.

Hemed aliendelea kucheka kwa muda mrefu halafu nikamuuliza “Hivi kweli Hemed unanipenda?”

“Nakupenda ndio ina maana huniamini?”

“Hahaha naelekea kukuamini lakini kwani umenipendea nini kiasi hicho?” niliuliza

“Basi tu unajua mwanamke bora ni yule anayejituma, ninahitaji mke kama wewe…..sikupaswa kukuacha hivi hivi nahitaji kukutunza uwe mama mzuri kwa wanangu wawili tu”

“Mmmh”

“Ndio”

“Haya ngoja nikaoge nitakupigia kuna kitu nataka nikuambie”

“Sawa”

*
Nilikata ile simu kisha nikaitazama ile simu aliyoniletea, nilifurahi kweli, nilienda kuoga halafu nikarudi na kujaribu kuiwasha, sikuwahi kutumia iPhone kabla hivyo ilipelekea kuwa na kaugumu fulani.

Niliachana nayo nikasema kesho yake nitaenda kumpatia anisaidie kuiweka sawa kabisa, nilifurahi sana.

Nilitoka nikawa napiga story na binamu yangu ambaye alikuwa ametoka shinyanga, tukala, kisha tukalala, usingizi haukunipitia usiku kucha, nilikuwa natamani kukuche nianze kutumia simu ya iPhone, yaani usiku ulikuwa mrefu kweli kweli.

Asubuhi na mapema nilienda kazini kwangu, nilipofika tu hivi nilimtumia ujumbe Hemed nikamuambia aje dukani kwangu, akanijibu kwamba yuko bize labda atakuja baadaye.

Jioni saa moja alinitumia ujumbe
“Njoo hapa Mbuzi on Target tule nyama nikusetie na hiyo simu” aliposema hivi nilifunga haraka na kwenda aliponiita kwa sababu nilikuwa napafahamu.

Nilimkuta akiwa na rafiki zake wakiwa wanakunywa pombe, nikawasalimia na kuketi halafu nikaagiza juisi.

Tulikaa dakika kadhaa, akawa ananionyesha namna ya kutumia ile simu, licha ya kuwa tofauti kidogo na simu za android lakini niliielewa kwa haraka, baada ya hapo tulikula nyama akanipeleka chumbani alichonifanya kiukweli nilienda nyumbani nikiwa hoi kabisa.

Ilikuwa saa tano usiku, ila nilipofika hivi mama nilimkuta akiwa sebuleni anasoma biblia, akaniita jina langu

“Mwanangu pendo”

“Mama”

“Usidanganywe na vitu vidogo kama simu….naona umebadilika” aliniambia

“Kwanini mama unasema hivyo?” nilimuuliza

“Nakuambia yule kijana aliyekununulia simu ndiye uliniambia anataka akuoe??”

Nilitazama chini kwa aibu sijui nimjibu nini ila mama akajua na kuniambia “Achana naye hafai kuwa mumeo” aliniambia mama

“Kwanini mama unasema hivyo?”

“Nasema hivyo kwa sababu namjua vizuri, ni rafiki wa baba yako wa kipindi kirefu ila urafiki ulipotea kwa sababu ya tabia zake, nashangaa sasa hivi karudisha urafiki” alisema mama

Sikumuelewa anamaanisha nini lakini niliendelea kumuuliza maswali ili nimuelewe “Kwani alifanya nini mama?”

Mama akafoka “Nimeshakuambia hafai kuwa mume wako, achana naye, ukienda huko usije ukarudi hapa ukilia, nitakuchoma moto” aliniambia kwa hasira

“Mama”

“Nini??”

“Au kisa dini?”

“Nayo pia…..pia tabia….. ukienda huko kuachwa ni mara moja tu huna cha kumfanya….acha ujinga” aliniambia mama

Sikuwa na cha kumjibu mama ila niliamua tu kuondoka zangu na kwenda chumbani, siku hiyo hata sikuoga maana nilikuwa nimeshaoga pale hotelini. Nililala mpaka asubuhi.
ITAENDELEA
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…