Watu wengi wanaamini kwamba maisha yetu ya baadaye yapo mikononi mwa watoto wetu. Ndoto zao zitajenga dunia ambayo tutaishi kesho, na matendo yao, mawazo yao, na maadili yao yatajenga mwelekeo wa jamii. Kwa hiyo, tukiwa kama watu wazima, ni jukumu letu kuwaongoza katika mwelekeo sahihi. Pia ni lazima tuwafunze maadili na kujua kujithamini wakiwa bado wadogo ili kuwasaidia kukua kama watu binafsi wanaowajibika, wenye huruma na wenye kuelewa wengine.
Kuna msemo maarufu usemao“Watoto ni waigaji wakubwa, kwa hiyo wape kitu kizuri cha kuiga.” Kwa kutilia maanani hili, hivi karibuni Wizara ya Mambo ya Nje ya China ikishirikiana na Shirikisho la Wanawake wa China, walizindua programu maalumu ya kukuza mawasiliano kati ya watoto wa China na Afrika. Programu hii ambayo imeendelea kwa siku sita imewawezesha watoto wa China na wenzao wa nchi zinazoshiriki za Afrika kutembelea Jumba la Makumbusho ya Kasri la Beijing na maeneo ya kitamaduni katika Jimbo la Henan la China.
Mpango huu utasaidia sana kupanua wigo wa kujenga uhusiano mzuri wa kirafiki kati ya watoto wa pande hizi mbili, na baadaye watakapokuwa wakubwa watarithi mikoba ya mababu zao na wazazi wao ambao kwa moyo mmoja walianzisha uhusiano mzuri wa kirafiki na kindugu ambao umeendelea kukita mizizi hadi hii leo.
Watoto hawa kutoka nchi za Afrika kama vile Namibia, Afrika Kusini, Somalia, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati walikaribishwa na watoto wenzao wa China kwenye sherehe iliyofanyika katika Kituo cha Watoto cha China na kupata kushiriki kwenye shughuli mbalimbali zilizoandaliwa kwa ajili yao, zikiwa ni pamoja na michezo, kuchora na ngoma na maonesho ya kungfu, pia wametengeneza vipochi vinavyonukia uturi na vikaragosi, na kuhisi uzuri na mvuto wa utamaduni wa jadi wa Kichina.
Mawasiliano haya kati ya watoto wa China na Afrika ni uwekezaji mzuri unaofanywa na China, hasa ikizingatiwa kwamba hivi sasa kuna fursa nyingi sana kwa pande zote mbili. Fursa hizi zinatarajiwa kuongezeka zaidi hapo baadaye, na hivyo kama kizazi cha watoto wa sasa kikiendelea kushikamana na kujenga mahusiano mazuri, basi uhusiano katika nyanja mbalimbali pia utaimarika zaidi na kuwa mzuri katika siku za baadaye.
Kama alivyosema Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wanawake wa China Bi. Huang Xiaowei kuwa watoto wanabeba mustakabali na matumaini ya China na Afrika, na mawasiliano kati ya watoto yataongeza uhai mpya katika kuendeleza urafiki kati ya China na Afrika. Haya ni maneno sahihi kabisa.
Mara nyingi tumekuwa tukishuhudia fursa zikitolewa kwa vijana, lakini kundi la watoto, kidogo linaonekana kusahauliwa kwasababu fursa kwao sio nyingi sana. Kupitia program kama hizi za kuwakutanisha watoto wa China na Afrika, watoto wataweza kujifunza lugha, utamaduni na mambo mengine mengi ili kuwaandaa hapo baadaye waje kuwa chachu ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika.
Wahenga wanasema “Kama tutakuza ndoto za watoto, ulimwengu utabarikiwa, na kama tukiwaangamiza, dunia pia itaangamia”. Katika harakati za kukuza ndoto za watoto hawa, kama itakumbukwa mwaka 2023 Mke wa Rais Xi Jinping wa China ambaye pia ni balozi wa kuhimiza elimu ya watoto wa kike na wanawake wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa Mama Peng Liyuan, akishirikiana na Shirika la Marais Wanawake wa Afrika kwa Maendeleo (OAFLAD) kwa pamoja walianzisha kampeni ya huduma ya afya kwa watoto yatima wa Afrika ijulikanayo kama "Kufurahisha Mioyo ya Watoto: Hatua ya Pamoja ya China na Afrika".
Watoto wanapokuwa na afya njema ndipo watakapoweza kushiriki kwenye program maalumu zinazoanzishwa. Hivyo tunatarajia kwamba program kama hizi ziwe nyingi na endelevu, na pia zishirikishe watoto wa nchi nyingi zaidi za Afrika. Watoto hawa mbali ya kuja China, pia wawezeshwe kutembelea na kukutana na watoto wenzao wa maeneo mengine mbalimbali ya Afrika. Kwa kufanya hivyo watapata fursa ya kushiriki katika ujenzi wa uhusiano mwema zaidi wa pande mbili.