Na Mwananchi Mwenye Hasira Kali.
WENGI tunaendelea kukuombea pumziko la amani. Hatuwezi kukuhukumu kwa lolote hasa sasa wakati huu ambapo uko mbele ya Mhukumu mwenye haki. Tunachoweza kufanya ni kumuomba Mwenyezi akupatie taji la haki ambalo amewawekea watumishi wake, waliomtumainia na kumwamini.
Tunakuombea siyo kwa sababu tunataka kujifurahisha au kujifariji bure, sisi wengine tulikuamini kwa dhati, tunaendelea kuamini ulivipiga vita vilivyo vizuri, na hata ulipomaliza mwendo, kazi njema ya kutukuka umeiacha nyuma yako, haya uliyoyafanya yataendelea kusimulia uzalendo wako usiotiliwa shaka kwa Tanzania, ushujaa wako wa kusimama kidete na bila kuyumbishwa na mataifa ya nje, ulilinda na kutetea rasilimali zetu kwa dhati, ukatupa tafsiri sitahaki ya taifa huru.
Ukautafsiri utajiri wetu wa rasilimali kwa vitendo, Tanzanite ikaanza kuwa mali ya Tanzania, masoko ya dhahabu yako kila mkoa wenye madini, Taifa sasa linajivunia msimamo wako, Afrika itaendelea kukumbuka kama kiongozi uliyeonyesha njia kwa vitendo namna ya kulinda na kuzifanya rasimali za Afrika ziwanufaishe waafrika wenyewe, wengine wamekuwa wajuzi wa maneno zaidi kuliko vitendo.
Miaka yako mitano tu ya Urais wa Tanzania umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutuonyesha wazi kwamba kale tulikokuwa tunaambiwa ni kasungura kadogo (keki ya taifa) kumbe siyo tu ni sungura bali ni nyati aliyenona. Ndiyo maana miaka yako mitano umeweza kuihamishia serikali yote Dodoma, umepeleka umeme vijijini karibu vyote, umejenga hospitali za rufaa, hospitali za wilaya na mikoa, vituo vya afya na zahanati kuliko wakati mwingine wowote na mambo mengi tu ambayo awali yalikuwa ya kusadikika.
Ndani ya chama umekijengea uwezo wa kujitegemea, umeweza kukikomboa kuondokana na utegemezi wa fedha za matajiri ambao walikiweka mfukoni, kimejikwamua kiuchumi, mali zake ambazo zilikuwa zinafujwa hovyo hovyo, umeziratibu vyema na sasa chama kinajua kinamiliki nini na wapi na kinapata mapato yanayokiwezesha kujitegemea ndiyo maana, kimeweza kuendesha shughuli za uchaguzi ndani ya chama kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, ukiwa Mwenyekiti wake bila kutembeza bakuli kwa wafadhili.
Siandiki haya ili kukutetea kwa wanaokubeza leo, mimi ni nani hata nijipe kazi iliyotukuka hivyo leo, sistahili kuwa mtetezi wako, mtetezi wako wa haki ni Mwenyezi Mungu aliye hai, ambaye ukingali tumboni mwa mama yako alikutakasa na kukufanya kuwa mtumishi wake kwa watu wa Tanzania uwatumikie kwa utumishi uliotukuka, lakini pia kazi zako njema zinakutetea na historia itakuwa shuhuda wa haya toka kizazi hiki hata cha tano na saba cha Mama Tanzania. Ninaandika kuililia Tanzania na kukisikitikia Chama Cha Mapinduzi.
Naililia Tanzania kwa namna ile ile Bwana Yesu alivyoulilia Mji wa Yerusalem, “Laiti ungalijua hata wewe katika siku hii yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako. Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke, watakuzingira na kukuhusuru pande zote; watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutabua majira ya kujiriwa kwako.”
Hayati Rais Magufuli hakuwa mtakatifu na wala hakujinasibu hivyo, alikuwa binadamu kama sisi na yapo mapungufu yake kama binadamu na pengine kama kiongozi. Lakini mzaha, kejeli na dharau anazofanyiwa leo na watanzania hawa hawa, wengine viongozi aliowaamini ni hakika zitarigharimu taifa hili.
Uamuzi wake wa kutetea rasilimali za watanzania, kulinda maslahi ya taifa lake, kwa ajili ya watanzania wenyewe, leo umegeuzwa dhihaka kwake, majitoleo yake ya kuijenga Tanzania mpya yanafanywa kuwa dharau iliyotukuka, kila anayejua kuandika na kutukana au kukejeli, anamwandika kumzodoa na kumfanya dhalili kadiri anavyoweza, hakika hii ndiyo sura ya Tanzania ambayo sikuwahi kuifikiria itafika hapa.
Tuliomsoma Walter Rodney katika How Europe Undeveloped Africa, walau ilisaidia kututambulisha kwamba Afrika limefanywa shamba la mataifa ya ulaya, wanakuja kuvuna wanavyoweza wanakwenda, kinachotokea ni kubadilisha tu mbinu za uvunaji lakini malengo na shamba ni vile vile. Ilianza biashara ya utumwa, ukaja ukoloni, ukaja ukoloni mambo leo ukiambatana na ubeberu, ukaitikiwa vyema na utandawazi. Nawapongeza kwa umakini huo, wenzetu wanajua wanachokitafuta kwetu, sisi hatujielewi ni akina nani tunataka nini kutoka kwa nani.
Ndiyo maana wakitokea watu aina ya kina Magufuli, wanabezwa, wanatwezwa, wanavikwa kila aina ya sifa chafu na mbaya ili tu ipatikane sababu ya kuwapuuza na kushusha hadhi ya mbele ya jamii. Kwao kuendelea kumsifia mtu aina ya Magufuli ni sumu kwa maslahi ya mataifa yao, kwa sababu atakuwa mfano na anaweza kuzalisha akina Magufuli wengine wa kutosha, hawataki hiyo.
Ndiyo maana sasa wamefanikiwa kwa muda mfupi sana, hata kabla majembe na makoleo yaliyotumika kumzika hayajapukutisha udongo wote wa kaburi, tayari kishaanza kuonekana hafai, hakuwa na maana na anageuzwa kichekesho. Sasa hivi kwa kuwa tu alikuwa anatumia sana maneno uzalendo na ubeberu, maneno haya yanatumika kama kielelezo cha bezo na kejeli, kutumia neno ubeberu sasa hivi unaonekana wa kizamani, huna nafasi katika Tanzania ya sasa, ukijiita mzalendo unaonekana kituko na kioja.
Natokwa na machozi kwa ajili ya Mama Tanzania, watu wako wanacheza ngoma wasiyoijua, wanitikia kibwagizo cha wimbo wa kigeni. Wayahaudi walipokuwa kando ya Mto Babeli, wakiwa utumwani waliowachukua mateka walitaka wawaimbie nyimbo za Sayuni, walikataa kata kata, wanawezaje kuimba wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni? Wakaapa bora ulimi ugandamane na kaa la kinywa kuliko kuikubali fedheha hiyo. Leo Watanzania tunaimbishwa wimbo wa kujitukanisha, kumkashfu Rais Magufuli katika nchi yetu wenyewe, aibu gani hii, Mungu atusamehe tu.
Spika wa Bunge Job Ndugai aliyekuwa akisisitiza kwamba Rais Magufuli “atake asitake tumauongezea muda”, ili aendelee kutawala kinyume na Katiba leo amekuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kabla hata suti aliyokwenda nayo Chato kuzika hajairudia kuivaa, kukejeli na kuonyesha miradi ya kimkakati iliyoanzishwa chini ya Rais Magufuli ni ya hovyo, haina manaa, kweli ubinadamu kazi.
Kwamba ndege hazihitajiki tena, huyu huyu aliyekuwa mstari wa mbele kusifia kwamba alikuwa Rais shujaa ametufuta aibu ya Taifa kutokuwa na ndege, kwamba Bandari ya Bagamoyo ina maana sana tena baada ya Rais kufariki, kweli?
Kwamba Rais alishauriwa vibaya, kisa? Mpendwa Spika wetu alipatiwa wasilisho kuhusu Bandari hiyo akiwa ziarani China, kwa nasibu tu, alikwenda kwa kazi nyingine ikatokea wakawapatiwa wasilisho hilo. Kama ilikuwa kazi nyingine na wasilisho hilo lilitolewa by the way, kiongozi wetu huyu wa mhimili anataka tumuelewe vipi kuhusu mradi huo. Anafikia hitimisho kwamba rais alishauriwa vibaya kuhusu mradi, Rais alielezwa kwa kina athari zake kwa taifa, halafu eye kukutana na bodi hiyo anataka tumuamini zaidi kuliko Rais aliyepata taarifa kamili na za kina?
Kama anajua ulikuwa na faida hizo na kama kiongozi wa mhimili muhimu kama Bunge, alishindwa nini kuteta na Rais hata faragha, ili kumweleza msimamo wake na uzuri wa mradi huo kwa maslahi ya taifa, kwanini asubiri mpaka Rais Magufuli afariki dunia? Huyu kweli ana dhamira njema na taifa hili?!
Kwa CCM, hapa sitalia, nawasikitikia tu, bila shaka mnakumbuka enzi za kuficha sare za chama chenu mnapokwenda kwenye mikutano yenu, mlikuwa hamuwezi kuthubutu kupita na sare za chama Kariakoo, leo mnaona fahari kukatiza na kijani na njano kila mahali tena kwa heshima, nadhani hayo yameletwa na pepo za kusi au kaskazi tu, hakuna mtu asijidai kwamba amekijengea chama heshima, tena Magufuli ndo kabisa asithubutu kujinasibu kwa hili, kwanza alikuwa mchanga kwenye chama.
Kama ndivyo na kama Magufuli alikuwa mbaya kiasi hiki tunachokishuhudia leo kwa baadhi ya viongozi wa serikali na CCM, kiasi kwamba makada wote sasa mnamuona hafai na hana maana tena, aliwachelewesha na mipango yake ya ‘kishamba’, ninao ushauri huu kwenu.
Ili chama kiwe salama, futeni legacy yote ya Magufuli ili chama kiwe cha kisasa, anzeni na kuandika upya ilani, muachane na ile ya kishamba ya kurasa 303, achaneni na elimu bure, msijenge tena hospitali na vituo vya afya, umeme vijijini umetosha, watimueni wamachinga barabarani, achaneni na yote aliyoanzisha Magufuli.
Badala yake, ruhusuni yote aliyoyazuia, waiteni wachina wajenge bandari Bagamoyo na sisi tuwe wa kisasa kama Sri Lanka (si mnajua kinachoendelea kwao baada ya kujengewa bandari kama hii na China), naona mnatamani tufuate njia yao, ni kama tumechoka kuwa huru, wapeni wamiliki kwa miaka na masharti wanayotaka.
Halafu muandae ilani ya yenye jina, Anti- Magufuli Manifesto, ili tutembee nayo katika uchaguzi wa 2025, kwa kuwa Magufuli aliwaudhi na kuwakera sana Watanzania, kwa kuwa serikali yake ilikuwa ya kidikteta, bila shaka ilani yetu itapokelewa vyema na wananchi na kutupa ushindi wa asilimia 90.
ASANTE JOHN