Historia ya kweli ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda

Historia ya kweli ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda

Kweli yapo mengi yakusisimua juu ya changamoto ya bara letu La Africa, kwa ujumla tu ninakushuru sana muwasilishaji was hoja na nikutie moyo usichoke kutuhabarisha.
 
MUENDELEZO WA HISTORIA YA KWELI YA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA [emoji1206].


Sehemu ya mwisho.


Katika sehemu hii ya mwisho, nitafanya hitimisho ili tuendelea na mjadala tu kuhususiana na kisa hiki cha kweli, tuendelee…

Baada ya Jenerali Dallaire kupata uhakika kwamba ndege iliyodunguliwa ilikuwa imembeba Rais Juvenal Habyarimana alituma wanajeshi kumi wenye asili ya Kibelgiji kwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu Agathe Uwilingiyimana ili kumpa ulinzi yeye na familia yake na pia kumpeleka mpaka kwenye kituo cha redio cha taifa cha Radio Rwanda ili apate kulihutubia taifa na kuwasihi raia wawe na utulivu.

Lakini kulikuwa na kikosi cha kijeshi cha weledi cha serikali ya Rwanda kinachoitwa 'Gendarmerie' (Presidential Guard) walikuwa tayari wameshaidhibiti Radio Rwanda na walianza kurusha matangazo na kuutangazia umma kwamba Rais Habyarimana ameuwawa na watusi (RPF) na hivyo wakati wa 'kuingia kazini' (kuuwa watusi) ulikuwa umewadia.

Askari wale wa Kibelgiji walidhibitiwa na makomando wa Presidential Guard na kunyang'anywa silaha. Kisha walimchukua Waziri Mkuu Uwilingiyimana mpaka nyumbani kwake ambako walimuua yeye pamoja na mumewe. Watoto wao walisalimika baada ya kujificha nyuma ya fenicha.
Kisha askari wale kumi wa Kibelgiji walipelekwa mpaka kwenye kambi ya jeshi la Rwanda ya Kigali ambako waliteswa na kisha kuuwawa kwa amri wa meja wa jeshi la Rwanda aliyeitwa Bernard Ntuyahanga.

Usiku wa siku hii ya tarehe 6 April mpaka siku ya tarehe 7 April 1994, wanajeshi wa Rwanda na wahutu wenye msimamo mkali walikuwa wanapita nyumba kwa nyumba mjini Kigali wakiwa na orodha mkononi wakiua wanasiasa wenye ushawishi pamoja na waandishi wa habari.

Ndani ya usiku huu wa kwanza mawaziri ambao wana msimamo wa kati waliuwawa na wale ambao walisalimika walienda kujificha.
Walifanya hivi ili kuondoa uwezekano wowote wa kuundwa serikali kwa dharura.

Katika kikao cha kamati ya dharura ambacho pia Dallaire aliitwa kushiriki, Kanali Bagorosa alimpendekeza Augustin Bizimungu kuwa Mnadhimu mpya wa jeshi (mnadhimu rasmi wa jeshi alikufa kwenye ndege pamoja na Rais Habyarimana) lakini Dallaire alifanikiwa kuweka msimamo wa kumkataa Bizimungu kutokana na msimamo wake mkali. Hivyo Marcel Gatsinzi ambaye ni muhutu mwenye msimamo wa kati akachaguliwa kuwa mnadhimu mpya wa jeshi.

Baada tu ya kuteuliwa, Gatsinzi alifanya juhudi kubwa kuzuia jeshi lisijihusishe na mauaji ya watusi. Kitendo hiki kiliwaudhi mno akina Bagorosa pamoja na viongozi wengine wa juu wa jeshi ambao walikuwa na msimamo mkali. Hii ilipelekea siku kumi baadae Gatsinzi kuuwawa na nafasi yake kuchukuliwa na Augustin Bizimungu ambaye alipendekezwa awali na Kanali Bagorosa.

Mauaji yalikuwa yanasambaa kwa kasi kubwa ya ajabu. Kingine ambacho kilisaidia zaidi ni tamaduni ya watu wa Rwanda kutii mamlaka. Amri zilikuwa zinatolewa kutoka Kigali na kisha kufika kwa Magavana wa majimbo ambao nao walielekeza wananchi wao kutekeleza amri hizo kwamba wanapaswa kumuua kila mtusi wanayemuona mbele yao.

Vijana wa Interahamwe ambao niliwaeleza huko nyuma ambao walikuwa wameandaliwa siku nyingi kwa silaha za jadi (mapanga) pamoja na mafunzo walikuwa wanaongoza wananchi wengine kufanya mauaji kwa majirani zao na marafiki zao.
Kila mtusi aliuwawa na hata wahutu ambao walikiwa wanawaficha au kuwahirumia watusi nao waliuwawa.

Katika miji mengine mauaji yalikuwa yanafanyika kwa urahisi kabisa kutokana na majirani kujuana vyema makabila yao.
Ila kwenye sehemu kama Kigali ambako kuna mchanganyiko mkubwa wa watu mauaji yalikuwa yanafanyika kwa uangalifu. Ni hapa Kigali ambako kwenye barabara viliwekwa vizuizi lukuki vya wanajeshi na vijana wa Interahamwe.

Vizuizi hivi vilikiwa ni kwa ajili ya kukagua vitambulisho vya taifa. Vitambulisho hivyo vilikuwa vinaonyesha pia kabila la mtu. Wahutu walikuwa wanaachwa na watusi wakiuwawa mara moja. Kama raia alikuwa hajabeba kitambulisho basi alihukumiwa kutokana na muonekano wake. Kwamba watusi ni wembamba, warefu, sura nyembamba na pua ndefu. Raia wenye muonekano huu walikuwa hawaulizwi mara mbili, shingo zao zilikuwa ni halali ya panga za vijana wa Interahamwe na jeshi la Rwanda.

Mauaji yalisambaa nchi nzima isipokuwa kwenye maeneo ambayo yalikuwa chini ya RPF kama vile majimbo ya Ruhengeri, Byumba, Kibungo na baadhi ya maeneo ya Kigali.

RPF walikiwa wanasonga mbele kwa ufanisi mkubwa wakiteka mji baada ya mji.

Wahutu kwenye miji ambayo RPF walikuwa wanaiweka kwenye himaya, walikuwa wanaikimbia miji hiyo kuhofia wanajeshi wa RPF kulipiza kisasi kwa kuwauwa. Ndipo hapa ambapo ndani ya siku chache sana za mwezi April karibia Wahutu 500,000 walivuka daraja maeneo ya Maporomoko ya Rusumo kuja Tanzania na kupokelewa kwenye kambi za wakimbizi za Umoja wa Mataifa.

Sehemu nyingine zote za nchi mauaji ya watusi yaliendelea na yalifanyika kimkakati kabisa.

Kanali Théoneste Bagorosa ambaye alijipachika uongozi wa kamati ya dharura, kupitia kamati hiyo wao ndio walikiwa kama wanaongoza nchi. Bagorosa ndiye ambaye alikuwa anatoa amri na kuhutubia kwenye radio kusisitiza mauaji ya 'mende' kwenye nyumba yao. Bagorosa pia alifanya vikao na viongozi wa juu wa vikundi cha Interahamwe na Impuzamugambi na kuwapa maelekezo ya namna ya kuongoza wananchi kufanya mauaji hayo.

Vinara wengine wa mauaji haya alikuwa ni waziri wa Ulinzi Augustin Bizimana, kamanda wa Paratroopers Aloys Ntabakuze, na kiongozi wa Presidential Guard Protais Mpiranya. Lakini pia kulikuwa na mfanyabiashara maarufu mjini Kigali aliyeitwa Felician Kabuga ambaye alikuwa anawasaidia rasilimali fedha Interahamwe ili waendelee na morali ya mauaji.

Siku ya tarehe 8 April, mauaji yakiwa yanaendelea kwa kasi, kanali Bagorosa akaitisha tena kamati ya dharura na kupendekeza serikali ya mpito. Theodore Sindikubwabo aliteuliwa kiwa Rais wa muda huku Jean Kambanda akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa muda.

Baraza la mawaziri lote liliundwa na wanachama wa 'power wings' wa vyma vya siasa vya MRND na CDR.
Serikali hii ya muda iliapishwa siku ya tarehe 9 April 1994 na mara moja makao makuu ya serikali yalihamishwa kutoka Kigali kwenda Gitamara ili kuepuka mapigano ambayo yalikuwa yanategemewa kati ya RPF na vikosi vya serikali.

Kamati ya dharura ilivunjwa… lakini Bagorosa ndiye alikuwa kwa uhalisia anaiendesha nchi. Yeye ndiye alikuwa na maamuzi ya mwisho ya katika kila jambo. Serikali iliyotangazwa ilikuwa ni kama geresha tu ili kuhalalisha kile ambacho kilikuwa kinaendelea.

Mauaji yaliendelea, amri ilitolewa kwamba asiachwe hata mtusi mmoja akiwa hai. Hata mtoto mchanga.

Kuna matukio mengi sana ya kusikitisha ambayo yalitokea lakini sitaingia ndani sana kwenye sehemu hii kama ambavyo nimesema awali.

Lakini hatuwezi kusahau tukio la mauaji kanisani eneo la Nyarubuye. Siku ya April 12, watusi wapatao 1,500 walikuwa wamejificha ndani ya kanisa katoliki la eneo hili. Kasisi wa kanisa hili, Padre Athanase Seromba aliwatonya Interahamwe juu ya uwepo watusi kanisano kwake. Interahamwe walitumia bulldozer kulisambaratisha kanisa lote na waliomo ndani. Wale ambao walikuwa wanajaribu kukimbia walikatwa mapanga mpaka kifo.

Tukio lingine ambalo hatuwezi kulisahau ni maelfu ya watusi ambao walikuwa wamejificha kwenye majengo ya shule ya ufundi ya Kigali (École Technique Officielle) mahala ambako wanajeshi wa Ubelgiji sehemu ya UNAMIR walikuwa wameweka kambi. Baadae Ubelgiji iliondoa wanajeshi wake wote nchini Rwanda baada ya wale kumi waliotumwa kumlinda waziri mkui Uwilingiyimana kuuwawa na Presodential Guard. Baada ya wanajeshi wa Ubelgiji kuondoka eneo hili, vijana wa Interahamwe walivamia na kuua watusi elfu kadhaa ambao walikuwa wamejificha hapa.

Japokuwa mauaji haya katika historia inakumbuka zaidi watusi na wahutu wachache kwamba ndio waliuwawa. Lakini mara nyingi tunasahau zaidi ya watu wa kabila la Watwa 30,000 ambao nao pia waliuwawa. Watu wa kabila la Twa walikuwa nao wanahesabika kama wasaliti. Wahutu wenye msimamo mkali waliwashutumu kwamba walikuwa wanawasaidia RPF kuingia kwenye miji.

Sasa basi;

Nilieleza kwamba Kagame alikuwa amefanikiwa kuingiza makomando 1,000 ndani ya Kigali ambao walikuwa wanalinda wanadiplomasia wa RPF katika Bunge. Mauaji ya kimbari yalipoanza tu, vikosi vya serikali vilishambulia jengo la Bunge kwa lengo la kuua makoamndo wa RPF ambao walikuwa pale. Lakini makomando hawa wa RPF walifanikiwa kwa ufasaha kabisa kudbibiti vikosi vya serikali na kuwarudisha nyuma nje kidogo ya Kigali.

Kagame aliongoza RPF kupambana kutokea Kaskazini mwa nchi wakiwa wamejigawanya kwenye makundi matatu na huku wakitafuta namna ya 'kulink' na makomando ambao walikuwa ndani ya Kigali.

Ndani ya siku chache RPF walipambana kuelekea kusini wakiiweka kwenye himaya mji wa Gabiro na sehemu kubwa inayozunguka kigali upande wa mashariki na Kaskazini. Hawakutaka kuivamia Kigali mara moja au Byumba, bali walipigana katika mtindo ambao walikuwa wanauzunguka mji wote wa Kigali kwa nje.

Mwishoni mwa mwezi April, RPF walikuwa wameweka eneo lote la mpaka wa Rwanda na Tanzania kwenye himaya yao. Kutokea hapa walisonga mbele kuelekea magharibi ya mji wa Kibungo na hatimaye kusini mwa Kigali.

Mpaka kufikia May 16 walikuwa wamekata mawasiliano ya barabara kati ya mji wa Kigali na Gitamara ambao ndipo ilikuwepo serikali ya mpito. Mpaka kufikia June 13, RPF walikuwa wameuweka mji wa Gitamara kwenye himaya yao na kuilazimu serikali ya mpito kukimbia na kwenda kuweka makazi kwenye mji wa Gisenyi.

Mpaka hatua hii RPF walikiwa wamefanikiwa kuizunguka Kigali kila pande na pia ndani ya mji kulikuwa na makomando wao.

Tusisahau kwamba vikosi vya serikali walikuwa na silaha nzito zaidi askari wengi zaidi. Kilichokuwa kinawasaidia RPF ni mbinu adhimu za kivita za Kagame. Ni hapa ambapo Jenerali Dallaiire alimuita Kagame "master of psychological warfare".

Kagame alikuwa anachukua advantage ya kwamba… kwanza vikosi vya serikali walikuwa wameelekeza nguvu zao zaidi na akili zao katika mauji ya kimbari badala ya kuweka kipaumbele cha kupambana na RPF. Lakini mafanikio ya RPF kuchukua mji baada ya mji pia yalikuwa yamefanya vikosi vya serikali kuishiwa morali na Kagame alifanya hivi makusudi ndio maana akaiweka Kigali kuwa ya mwisho kuiteka.

Kwa hiyo sasa alikuwa anafanya mashambulizi ya ufanisi ya kushtukiza kwa masaa kadhaa pale Kigali na kisha ana-retreat. Wanasubiri masaa mengine kadhaa wanashambulia tena kisha wana-retreat. Tena na tena na tena. Alichokuwa anafanya ni kama kuwachekecha vikosi vya serikali na kuwachosha. Hii ilifanikiwa, kwani tarehe 4 July, RPF walifanya shambulio kubwa na kufanikiwa kuwashinda kwa urahisi kabisa vikosi vya serikali na kuiweka Kigali kwenye himaya yao.
Ilipofika tarehe 18 July walichukua mji wa Gisenyi na eneo lote la kaskazini magharibi ya Rwanda na kuifanya ile serikali ya mpito kukimbilia Zaire.

Mpaka hapa maana yake ni kwamba Rwanda yote sasa ilikuwa chini ya himaya ya RPF isipokuwa eneo dogo la kusini magharibi ambalo lilikuwa chini ya jeshi la Ufaransa walioingia Rwanda chini ya Oparesheni maalumu ya Umoja wa Mataifa.

Kwa hiyo, mpaka hapa ni rasmi kwamba RPF walikuwa wamezima mauaji ya Kimbari. Tarehe rasmi ya mauaji ya kimbari kukoma ni tarehe 15 July 1994 japokuwa Rwanda wenyewe wanaadhimisha siku hii kila mwaka tarehe 4 July kama siku ya Ukombozi wa Taifa na ni siku ya mapumziko.

Umoja wa mataifa unatoa takwimu kwamba watu 800,000 waliuwawa kwenye mauji yale huku serikali ya Rwanda yenyewe ikisisitiza kuwa ni watu 1,071,000. Inakisiwa kwamba Wahutu walikuwa ni 10% ya watu hawa waliouwawa.

Mauaji haya ni moja ya mauaji mabaya zaidi kuwahi kutokea katika historia ya dunia yetu hii. Ni mauaji ambayo yanapaswa kutufunza mambo mengi sana. Kwamba ubaguzi, unyonyaji, ukandamizaji na kujikweza huzaa chuki kwa wale wanaoteswa. Chuki hii inaweza kufurukuta rohoni mwa watu hawa kwa miongo kadhaa lakini siku itakapopata ufa wa kujipenyeza, moto wake unaweza usizimike pasipo kuitafuna dunia.

Kuna vitu vingi vingi sana sana najua sijavigusia kwenye hitimisho langu hili. Naomba kwa makala hii tuishie hapa huko mbeleni tukipata wasaa tunaweza kuirejea na kugusia yale ambayo nimeyaacha katika mfululizo huu.

Dunia yetu itakuwa mahala salama na pazuri pa kuishi endapo wote kwa pamoja tutajifunza kwamba hakuna aliye mbora kuliko mwingine. Tukijifunza kuheshimu utu, kujiheshimu na kuheshimiana. Tukiwa mawakili wa haki na umoja. Na sote tukikumbuka kwamba sisi ni wana wa baba mmoja.


Naomba niishie hapa.

Asanteni sana kwa kuifuatilia na karibuni kwa majadiliano.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ndugu mtoa uzi na swali je imekuaje bizimungu kuendelea kuwa rais mpaka mwaka 2000 wakati kagame alikua tayari kaisha iweka nchi chini ya himaya yake?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Nashukuru sana sana muwasilishaji kwani nimejifunza mengi sana katika historian ya mauaji ya Rwanda, swali language nlikua napenda kujua VP mahusiano ya sasa kati ya Mh. Kagame na Mseveni yanauimara au kunatofauti maana kumekua na migogoro ya hapa na pale he shida no nini? Pia Luna wakati kulikua na sintofahau baina ya mh kagame na mmoja was wakuu was nchi za maziwa makuu he inawezekana akawa ana ndoto ya kutaka kujenga dola LA Afrika mashariki?
 
Ukitaka haya yote chifu tafuta mtu anaitwa habibu anga au the bold huyo ndio mwandishi wa hii story huyu kaiga tu anaelezea kila kitu
Nashukuru sana sana muwasilishaji kwani nimejifunza mengi sana katika historian ya mauaji ya Rwanda, swali language nlikua napenda kujua VP mahusiano ya sasa kati ya Mh. Kagame na Mseveni yanauimara au kunatofauti maana kumekua na migogoro ya hapa na pale he shida no nini? Pia Luna wakati kulikua na sintofahau baina ya mh kagame na mmoja was wakuu was nchi za maziwa makuu he inawezekana akawa ana ndoto ya kutaka kujenga dola LA Afrika mashariki?

Sent using Jamii Forums mobile app
 
This guy Paul Kagame ni mtu hatari sana ni master mind aliyetukuka, hakika mimi binafsi huwa namkubali sana, yuko calm na very focused sana. Nafikiri ni moja kati ya maraisi bora kabisa waliowahi kutokea Afrika Mashariki.
 
HUU NI MFULULIZO WA HISTORIA YA KWELI YA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA

Sehemu ya kwanza

“..kama unasoma ujumbe huu, muda huu… uko mpweke! Pengine ushahidi pekee uliobakia ni kijipande hiki cha maandishi. Sijui kama kuna yeyote kati yetu aliyesalimika kufika kizazi chenu mwaka huu mtakaosoma andishi langu. Sijui hata kama tumeshinda au tumeshindwa vita tunayopigana sasa hivi. Sijui, lakini naamini mwaka huu mliopo nyinyi sasa mwaweza kuwa na jibu sahihi. Vyovyote vile lakini jambo lililo dhahiri ni kwamba hakuna yeyote wa kizazi chetu mliye naye sasa hivi kwenye miaka yenu muusomapo ujumbe huu. Kwa hiyo wacha niwaeleze sisi tulikuwa akina nani, na kwa namna gani tulipambana mpaka tone la mwisho la damu mwilini mwetu ili kutetea kizazi chetu kisifutwe juu ya uso wa dunia. Wacha niwaeleze namna ambavyo japo tulikamuliwa damu mpaka kutiririka kufanya mifereji lakini lakini tulisimama kutetea kizazi chenu na ninyi watoto wetu. Wacha niwaeleze kisa kilichotikisa ulimwengu. Wacha niwaeleze kuhusu mifereji ya damu kwenda Ethiopia.!”

March 21, 1994 maeneo ya Uganda ambayo yanapakana na Rwanda, katika ziwa viktoria serikali ilituma vikosi vya jeshi kudhibiti eneo hilo kwa hali ya dharura. Agizo hili la serikali kutuma jeshi halikuwa kwa ajili ya kidhibiti eneo hilo kutoka kwa adui bali agizo lilikuwa ni kudhibiti eneo hilo dhidi ya maiti, maiti za binadamu. Sio maiti mbili au tatu, si mamia bali maelfu ya maiti za binadamu ambazo zilikuwa zinaingia ziwani Victoria zikiletwa na maji ya mto Kagera.

Maiti hizi zilikuwa nyingi kwa maelfu kiasi kwamba mapaka zilikuwa zinafanya maji yatoe harufu. Serikali ya Uganda ilituma jeshi eneo hili ili kudhibiti eneo hili maji yake yasitumiwe na wananchi kwa matumizi ya nyumbani au shughuli za uvuvi. Lakini jeshi lilikuwa eneo hili ili kuhakikisha kuwa taharuki iliyozuka baada ya maelfu ya miili hii kuonekana haigeuki na kuvuruga amanai katika eneo hili. Lakini pia jeshi lilikuwa hapa ili kubaini miili hii ilikuwa inatoka wapi.

Kadiri ambavyo jeshi la Uganda lilivyokuwa linafuatilia kwa kurudi nyuma kufuata mto Kagera ndivyo ambavyo walizidi kubaini kwamba maiti hizo zinaletwa na maji kutoka tawi la mto Kagera lililopita kusini mwa Rwanda. Na kadiri ambavyo walizidi kufuata chanzo cha maiti hizo zinakotoka ndivyo ambavyo walikuwa wanaikaribia Rwanda na maji ya mto rangi yake kuwa nyekundu zaidi.

Wanajeshi wa Uganda ambao walishiriki kwenye ukaguzi huu wa mto huu wanakiri kwamba licha ya baadhi yao kupigana mstari wa mbele kwenye vita mbali mbali lakini hakuna yeyote kati yao ambaye aliwahi kushuhudia ukatili mkubwa wa kiasi hiki.

Siku hii jeshi la Uganda linakisia kwamba waliokota si chini ya miili elfu kumi ya binadamu na yote ilionekana kuletwa na maji ya mto Kagera kutoka nchini Rwanda. Ajabu ni kwamba miili yote hii ilikiwa inamfanano fulani. Maiti zote zilikuwa za watu warefu, wembamba, wenye nyuso ndefu na pua za kuchongoka. Haikuhitaji kufikiria sana kufahamu kuwa maiti hizi zilikuwa za watu wa kabila la Tusi (Tutsi).

Miezi kadhaa baadae ndipo ambapo jeshi la Uganda na ulimwengu wote walikuja kuelewa kwa nini maiti zilikuwa zinatupwa mto Kagera. Ni ujumbe gani ambao ulikuwa unajaribu kutumwa.

Kwamba Watusi nchini Rwanda walikuwa waapenda kujisifu kuwa mababu zao wana asili ya nchi ya Ethiopia. Kitendo hiki cha watesi wao kuwatupa mtoni, walikuwa wanawaua na wakiwa wanatupa maiti zao mto wanawaambia kwamba “wanawasafirisha warudi kwao Ethiopia ambako wamekuwa wakijisifu ndio asili yao.”

Sio kwamba jeshi la Uganda hawakuwa na taarifa juu ya hali tete iliyopo Rwanda kwa muda wa karibia wiki nzima iliyopita bali hawakujua kama hali hiyo tete ilikuwa ni ya kinyama kiasi hicho.

Wanajeshi hawa wa Uganda walikuwa wameshikwa na bumbuwazi na vihoro vilivyo wapasua mioyo kwa kuona miili hii elfu kumi ya binadamu isiyo na uhai. Kitu ambacho walikuwa hawakijua na hakuna ambaye alidhahania ni kwamba ndani ya siku mia moja zijazo ulimwengu ulikuwa unaenda kushuhudia moja ya tukio la kikatili zaidi tangu kuubwa kwa ulimwengu. Karibia maiti za binadamu milioni moja zikiwa
zimetapakaa mitaani nchini Rwanda iking’ong’wa na nzi na kuliwa na mbwa.

GENESIS

Rwanda: Kabla ya Ukoloni


Asili rasmi kabisa ya watu wa kwanza kuishi katika eneo ambalo leo tubalitambua kama nchi ya Rwanda ni watu wa kabila la ‘Twa’ (Watwa). Kabila hili la wawindaji si la kibantu bali ni sehemu ya makabila yanayotambulika na wanahistoria kama ‘pygmy’ ambao sifa yao kuu ni ufupi. Mtu mzima anayetoka makabila ya namna hii anakadirwa kuwa na wastani wa urefu chini ya sentimita 150. Watwa waliishi Rwanda enzi za kale sana miaka ya 8000 BC na 3000 BC.

Kuanzia miaka ya 700 BC mpaka 1500 AD makabila ya Kibantu kutoka maeneo ya jirani yalianza kuhamia eneo hili.

Kuna nadharia mbali mbali kuhusu ni namna gani haswa makabila haya ya kibantu yalihamia hapa na baadae kupelekea kutokea Makabila ya sasa ya Wahutu na Watusi.

Nadharia ya kwanza inadai kwamba; Wahutu ndio walikuwa wa kwanza kuhamia eneo hili na kuanzisha shughuli za kilimo. Baadae watu wenye asili ya Ukushi (Watusi wa sasa) nao wakahamia kwenye eneo hili na kulitawala.

Nadharia ya Pili inadai kwamba; kuna uwezekano kwamba Watusi si wakushi bali ni wahamiaji tu kutoka maeneo ya jirani kipindi hicho cha kale ambao walihamia na kujichanganya na jamii waliyoikuta hapo (Wahutu) lakini wao walikuwa wafugaji. Chini ya nadharia hii inadai kwamba kuibuka kwa Wahutu na Watusi hakukutokana na kuwa na utofauti wa kinasaba au asili ya mababu bali ulitokana na utofauti wa kimadaraja/matabaka ya kijamii.
Tabaka la wale walio wa daraja la juu ambao walikuwa wafugaji walijitanabaisha kama Watusi wakati ambapo tabaka la chini ambao walikuwa wakulima walijitanabasha kama Wahutu.

Makabila haya yote matatu, Watwa, Wahutu na Watusi wanazungumza lugha moja na kwa wote kwa pamoja wanajulikana kama ‘Banyarwanda’.

Idadi ya watu ilipoongezeka katika eneo hili walianza kujitambua kupitia makundi madogo madogo yaliyoitwa ‘Ubwoko’ au ‘koo’ kwa kiswahili. Ilipofika katikati ya miaka ya 1700 koo nyingi ziliungana na kuunda ‘Falme’.
Moja ya Falme ambazo zilikuwa imara zaidi ulikuwa ni ‘Kingdom of Rwanda’ ambayo watawala wake wote walitokea katika koo ya Kitusi ya Nyiginya.

Ufalme huu ulifikia kileleni kipindi cha utawala wa Mfalme Kigeli Rwabugiri chini ya falsafa yake ya kujipanua na kuteka falme nyingine na kuzifanya sehemu ya Kingdom of Rwanda.

Chini ya Mfalme Rwabugiri alianzisha mfumi wa kiuchumi wa ‘ubuhake’ na baadae ‘uburetwa’.
Katika mifumo yote hii miwili, iliwanufaisha zaidi Watusi na kuwafanya Wahutu kama vijakazi wao kuwafanyia kazi za uzalishaji na kuwa askari vitani kwa ujira wa kupata fursa ya kumiliki mifugo na kutumia ardhi.

Watusi walipaa juu zaidi na kuwa raia daraja la kwanza ma Wahutu kubakia kuwa tabaka la chini kabisa ndani ya Kingdom of Rwanda.

Rwanda: Wakati wa Ukoloni

Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ulilitoa eneo hili kuwa koloni la nchi ya Ujerumani. Wajerumani walitawala eneo hili kwa kushirikiana na Mfalme na hivyo kuwapa wepesi wa kutawala koloni bila kuwa na askari wengi wa kijerumani ndani ya ardhi ya Rwanda. Yuhi V Musinga ndiye walikuwa Mfalme wa Rwanda kwa kipindi hiki na anakumbukwa zaidi kwa kuwapokea Wajerumani kwa mikono miwili.

Ikulu ya Mfalme wa Rwanda maeneo ya Nyanza

Wajerumani ndio walikuwa watu wa kwanza kuanza kuwapandikizia Watusi kasumba ya kuwa wao si Wabantu. Wakoloni wa Ujerumani ndio ambao walieneza propaganda kwa kuwafundisha Watusi kwamba kutokana na tafiti zao za kina wamegundua kwamba wao (Watusi) mababu zao wa kale walihamia eneo hilo kutokea Ethiopia. Hivyo wakawashawishi kuamini kwamba Watusi wana vinasaba vya ‘uzungu’ (Caucasian) na hivyo ni wao pekee ndani ya Rwanda walistahili kupata nafasi za ajira kusaidizana kazi na wazungu chini ya utawala huo wa Wajerumani.

Katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Ubelgiji iliziteka Rwanda na Burundi kutoka mikononi mwa Ujerumani na mwaka 1919 League Of Nations ilizifanya rasmi nchi hizo kuwa makoloni ya Ubelgiji.

Mwanzoni Wakoloni wa Ubelgiji walianza kuitawala Rwanda kwa mtindo ule ule wa kushirikiana na Ufalme lakini baadae wakajilimbikizia madaraka yote ya kutawala kama ambavyo walifanya kwenye koloni lao la Kongo.

Baadae wakaanza ‘kutaifisha’ mali za Wanyarwanda katika mfumo wa kufanana kabisa na mfumo wa asili wa uburetwa na walioathirika zaidi na kampeni hii ya utaifishaji walikuwa ni Wahutu.
Ardhi yao ilinyang’anywa… Mifugo ilitwaliwa na kuwafanya Wahutu kuwa si tu vijakazi wa Wakoloni bali pia vijakazi wa Watusi.

Mwanzoni mwa miaka ya 1930s Ubelgiji walifanya upanuazi mkubwa wa sekta ya Elimu, afya na ajira za umma. Lakini wanufaika wakuu walikuwa ni Watusi.

Mwaka 1935 Ubelgiji walifanya kitu ch a ajabu sana ambacho kilipanua zaidi mpasuko wa kijamii na kitabaka uliopo ndani ya Rwanda. Walianzisha mfumo wa raia wote kuwa na vitambulisho. Vitambulisho hivi viliwatambua raia wote katika makundi manne kulingana na makabila yao. Watwa, Wahutu, Watusi na Raia wa kuomba (Naturalised).

Kutokana na Watusi kuwa ndio raia wa daraja la kwanza na tabaka la juu huku Wahutu wakiwa ni watu hafifu wa kudharaulika nchini humo, ilifikia hatua Wahutu wenye mali au ushawishi walikuwa wanahonga fedha ili kupatiwa vitambulisho vya Kuonyesha ni Watusi na watawala hawakuwapa Utusi kamili bali waliwapa ‘utusi wa heshima’ (Honorary Tutsi).

Hadhi ya Wahutu wote iliendelea kushuka kwa kasi wakionekana ni kabila na kizazi cha “Washenzi” huku Watusi wakionekana ndicho kizazi cha “wastaarabu” na kabila lenye darja.

Lakini kuna suala ambalo lilifanyika mwanzoni likionekana kuwa na manufaa makubwa lakini kadiri siku zilivyokwenda lilianza kuwa kama mkuki mgongoni. Kanisa Katoliki.

Kanisa Katoliki lilikuwa limeenea sana nchini Rwanda na raia wake wengi wakiwa ni waumini wa kanisa hilo. Tukumbuke kwamba tangu kipindi hicho Wahutu ndio walikuwa idadi kubwa zaidi ya raia wote ndani ya Rwanda. Hii ilimaanisha pia kwamba waumini wengi wa kanisa Katoliki walikuwa ni Wahutu.

Kwa kiasi fulani ndani ya kanisa Katoliki mapadri na watawa wengine walikuwa wanajisikia hatia kuacha waumini wao kuwekwa kwenye kundi la kizazi cha “washenzi” na kudharaulika ndani ya jamii. Kwa hiyo zikaanza juhudi za makusudi za kanisa katoliki kutoa elimu kwa vijana wenye asili ya Kihutu.

Baada ya miaka kadhaa kukaanza kuwepo walau kidogo uwiano wa wasomi wa Kihutu na Kitusi.

Mwaka 1957, mwezi March kikundi cha wasomi na watu wenye ushawishi wenye asili ya Kihutu walifanya jambo la “kimapinduzi” ambalo lilipanda mbegu mpya kwenye nafsi za watu wa kabila na kizazi cha cha Kihutu. Waliandaa waraka ulioitwa _'Manifeste des Bahutu' (Bahutu Manifesto).
Huu ndio ulikuwa waraka wa kwanza rasmi kubainisha kwamba Wahutu na Watusi ni mbari (race) mbili tofauti.

Katika waraka huu, wasomi hawa na watu hawa wenye ushawishi walijenga hoja kuu kwamba… Watusi wanapaswa kutoka kwenye jukumu lao walilojivesha la kuwa watawala wa Rwanda na badala yake nafasi hiyo ya kutawala Rwanda wapewe Wahutu. Hoja yao hii waliijenga kwenye nadharia ambayo wenyewe waliita “Statistical Law”, kwamba kitakwimu Wahutu ni wengi mno kushinda Watusi. Si sawa wakiendelea kutawaliwa na kufanywa vijakazi na Watusi.

Wanasema kwamba kabla kibanda cha nyasi kuungua kwanza utaanza kukiona kinafuka moshi. Kuna vugu vugu lilianza chini kwa chini ndani ya Rwanda.

Waraka huu… Bahutu Manifesto, ulitoka tarehe 4 March mwaka 1957. Japokuwa ilikuwa ni miaka takribani 37 kabla ya mwaka 1994, lakini ndio siku ambayo mbegu ya mauaji ya kimbari ilipandwa.

Usikose sehemu inayofuata.

Itaendelea...



Sent using Jamii Forums mobile app
Dah inasikitisha, ukabila sio kitu kabisa😭
 
Siku hii jeshi la Uganda linakisia kwamba waliokota si chini ya miili elfu kumi ya binadamu na yote ilionekana kuletwa na maji ya mto Kagera kutoka nchini Rwanda. Ajabu ni kwamba miili yote hii ilikiwa inamfanano fulani. Maiti zote zilikuwa za watu warefu, wembamba, wenye nyuso ndefu na pua za kuchongoka. Haikuhitaji kufikiria sana kufahamu kuwa maiti hizi zilikuwa za watu wa kabila la Tusi (Tutsi).
Sawa; time will tell
 
Back
Top Bottom