ENDELEA NA HISTORIA YA KWELI YA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA [emoji1206]
SEHEMU YA 10
Le Clan de Madame
Mkataba wa makubaliano ambao ulisainiwa Arusha kwa kiasi kikubwa ulikuwa chanya kwa pande zote na kila mtu, yaani Kagame, Habyarimana na vyama vya upinzani waliridhia kabisa mkataba huo.
Lakini shida ilikuwa kwa Wahutu wenye msimamo mkali chini ya CDR na hata ndani ya MRND. Wengi wao hawakukubali mkataba huo kwa sababu moja kuu, kuona kwamba ati watusi warejee kuwa sehemu ya uongozi wa nchi.
Kwao hili waliona na tusi zito na kitu ambacho abadani hawawezi kukikubali.
Vuguvugu hili likapamba moto na wahutu wenye msimamo mkali wakiongozwa na kikundi kidogo cha watu wenye ushawishi mkubwa serikalini ambao walijiita 'le clan de madame' (inner circle ya akazu).
Walianza kuratibu maandamano ya Wahutu nchi nzima kupinga mkataba ambao Rais Habyariamana alitiliana saini na RPF.
Kwa kuwa japokuwa walikuwa wanafanya maandamano lakini bado serikali ya Habyarimana haikuwasikiliza wala kurudi nyuma kwenye mkataba wake na RPF, hivyo wakaamua kwenda mbali zaidi. Wakaanza tena mauaji dhidi ya Watusi.
Mauaji haya yalifanyika zaidi maeneo ya Kaslazini Magharibi mwa Rwanda na yalidumu kwa muda wa siku sita mfululizo wakishuhudia mamia ya watusi wakiuwawa na nyumba zao kuchomwa moto na Wahutu. Mara ya kwanza Kagame hakutaka kufanya chochote kile au kuchukua hatua za kijeshi zozote akiamini kwamba umebaki muda mchache watakuwa sehemu ya serikali na watahakikisha kwamba mauaji hayo yanakoma.
Ubaya ni kwamba kama nilivyoeleza kuwa Rais Habyarimana alikuwa anaheshimika na Wahutu wenye nguvu kutokana na mkewe kutoka kwenye familia yenye ushawishi mkubwa nchini humo. Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kwamba Rais Habyarimana alikuwa kama amewekwa kiganjani kimaamuzi na alikuwa hawezi kufanya lolote bila mkewe kukubali. Hii ndio sababu ambayo ilimfanya ashindwe kufanya lolote pale ambapo akazu walianza kuratibu mauaji dhidi ya Watusi. Na mkewe abadani asingeliweza kukubali watu wake wa 'le clan de madame' kuchukuliwa hatua.
Kwa hiyo mauaji dhidi ya Watusi yaliendelea sehemu mbali mbali na serikali ya Habyarimana ilishindwa kufanya chochote licha ya kusaini makubaliano ya amani na RPF.
Nimeeleza kwamba mwanzoni Kagame hakutaka kuchukua hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya mauaji yaliyokuwa yanaendelea ili kuheshimu mkataba ambao walisaini Arusha.
Lakini kuna jambo moja lilitokea.
Watusi ambao miji yao ilivamiwa na kuanza kuuwawa, baadhi yao walifanikiwa kutoroka kutoa kwenye miji hiyo na kukimbilia kwenye maeneo ambayo yalikiwa yanashikiliwa na RPF ili kuokoa maisha yao.
Watu hawa ambao walikimbilia kwenye maeneo yaliyo chini ya RPF kuna siku walikutanishwa na Kagame na kuongea nao. Walimsimulia kinaga ubaga namna ambavyo Watusi wananyanyasika na kuuwawa kama wanyama wa mwituni hapo Rwanda. Inaelezwa kwamba siku hii ilikuwa ni moja kati ya siku chache sana ambapo Kagame alishuhudiwa machozi yanamtoka hadharani kutokana na simulizi hizo za mateso ya Watusi ambazo alisimuliwa na watu hao waliotoroka kutoka mikononi mwa Wahutu.
Ndipo hapa pasipo jumuiya ya kimataifa kutegemea, Kagame akatoa tamko rasmi kwamba yeye na RPF wanajitoa kwenye mazungumzo ya amani ya Arusha na pia wanajitoa kwenye mkataba wa amani uliosainiwa.
Alijenga hoja kwamba haoni dhamira yoyote ile ya serikali kuzuia mauaji dhidi ya watusi ambayo yalikuwa yanaendelea nchini Rwanda hivyo wanachukua jukumu mikononi mwao kukomesha mauaji hayo yanayoendelea.
Ilikuwa tayari imepita miezi sita tangu mapigano ya RPF na vikosi vya serikali yasimame ili kupisha mazungumzo ya amani Arusha. Na leo hii baada ya miezi sita Rwanda ilikuwa inarejea tena vitani.
Siku hii ilikiwa ni February 8, 1993.
Hivyo basi siku hii ya February 8, 1993 RPF wakarudi tena vitani dhidi ya majeshi ya serikali.
Mapigano ya safari hii RPF hawakupata upinzani mkubwa kama miezi sita nyuma. Walikuwa wanawashinda vikosi vya serikali kwa urahisi sana na kuyaweka maeneo mengi zaidi kwenye himaya yao.
Shida kubwa ambayo walikuwa nayo vikosi vya serikali ni morali ndogo, nidhamu na uzoefu.
Katika kipindi hiki uchumi wa Rwanda ulikuwa umetetereka kwa kiasi kikubwa sana kutokana na serikali kutumia fedha nyingi kugharamia vita kwa miaka kadhaa. Sarafu ya Rwanda pia, faranga, ilikuwa imeshuka thamani kwa kiwango cha kutisha dhidi ya dola ya marekani.
Hivyo serikali ya Rwanda ilikuwa haina fedha ya kutosha kulipa wanajeshi wake mishahara kwa wakati. Na hii ilishusha mno morali ya wanajeshi.
Lakini pia katika kipindi hiki serikali kutokana na woga na kujihami walikuwa wameongeza ukubwa wa jeshi kutoka wanajeshi 10,000 mpaka kufikia wanajeshi 30,000 ndani ya muda mfupi sana. Wanajeshi hawa hawakuwa na uzoefu wa uwanja wa vita na pia hawakuwa na nidhamu ya kiaskari. Mara nyingi waliripotiwa kuvamia raia na kubaka wanawake na kuua wengine.
Hivyo basi licha ya Kagame kuwa na wanajeshi wachache mno kulinganisha na vikosi vya serikali, lakini waliwazidi weledi wa kijeshi, nidhamu na uzoefu. Na hii ndio sababu ya RPF safari hii kuwapiga vikosi vya serikali kwa urahisi mno.
Vikosi vya RPF vilipigana kutokea Kaskazini mwa Rwanda na kushuka kusini. Waliiweka tena Ruhengeri kwenye himaya yao ndani ya siku moja tu ya mapambano. Kesho yake wakaichukua Byumba na kuendelea kuchukua mji baada ya mji.
Rwanda ilishuhudia kwa mara nyingine tena maelfu kwa maelfu ya wahutu wakikimbia miji yao kwenda kwenye maeneo yaliyo chini ya vikosi vya serikali ili kuwakimbia RPF.
Mtikisiko huu mkubwa wa ushindi wa RPF kila siku ulifika mpaka Ufaransa ambao walikuwa wanamfadhili kwa kiasi kikubwa Rais Habyarimana kutokana na wao kuwa na maslahi ya moja kwa moja ndani ya Rwanda.
Kwa kupaniki, serikali ya ufaransa ikatuma vikosi vya wanajeshi wake kuja Rwanda kusaidia vikosi vya serikali kuwadhibiti RPF.
Baada ya vikosi vya wanajeshi wa Ufaransa kuwasili angalau waliweza kuwatikisa RPF kwa siku kadhaa na kutoa upinzani halisi wa kijeshi. Lakini hii ilikuwa ni kwa siku chache mno kabla ya RPF kurudi tena kwenye ubora wake na kuwadhibiti sawasawa vikosi vya serikali na Ufaransa kwa pamoja.
Mpaka kufikia February 20, 1993… RPF walikuwa wamebakiza kilomita 30 tu kuingia mji mkuu wa Kigali. Wachambuzi karibu wote wa masuala ya medani za vita wanakubaliana kwamba kama RPF wangefanya shambulizi mara moja tu kwa nguvu ambayo walikuwa nayo na kwa jinsi walivyokuwa wamewadhibiti vikosi vya serikali na Ufaransa basi wangeweza kuiweka Kigali mikononi mwao na kujitangazia ushindi.
Lakini Kagame alifanya kitu cha ajanu ambacho mpaka leo hii yawezekana ni yeye mwenyewe pekee akilini mwake ndiye anaelewa kwa nini alichukua maamuzi yale.
Kagame hakuishambulia kigali wala kuingiza wanajeshi wake. Na hakuishia hapo tu, akatangaza kusitisha mapigano dhidi ya vikosi bya serikali.!!
Hii ilikuwa ni ajabu kweli kweli. Hakuna ambaye alitegemea au kutarajia kitu hiki. RPF walikuwa wameshinda nguvu vikosi vya serikali na shambulizi dogo tu lilitosha kuiweka Kigali kwenye himaya yao. Kwa nini Kagame hakutaka kuishambulia Rwanda? Na kwa nini aliamua kutangaza kusitisha mapigano?
Hakuna anayejua zaidi ya Kagame mwenyewe…
Suala hili liliwachkukiza mno makamanda wenzake wa ngazi za juu wa RPF na kukatokea sintofahamu kubwa sana nusura kuipasua RPF.
Lakini suala moja hatupaswi kusahau ni kwamba, Paul Kagame ni "master of psychological warfares".
Ni mtu mwenye kujua mno na ustadi wa hali ya juu kupambana kisaikolojia na kucheza na akili ya adui.
Binafsi, moja ya masuala ambayo yamenifikirisha sana wakati wa kuandaa makala hii basi ni hili tukio, kwa nini Kagame aliamua kutoshambulia Kigali siku ile ya February 20? Kwa nini aliamua kutangaza kusitisha mapigano?
Nikajaribu kuvaa viatu vyake na kuona kile ambacho Kagame alikuwa anakiona… (unaweza pia kunipa maoni yako inbox).
Katika tafiti zangu kuhusu makala hii jambo moja ambalo nimeliona ni ongezeko la silaha za kisasa kwa RPF katika kipindi hiki (February 1993). Silaha hizi zilikuwa zinachukuliwa kutoka kwa wanajeshi wa serikali kila mahala ambapo wanakuwa wamewashinda.
Hapa naona vitu viwili… Kagame alikuwa anataka kulimega jeshi la serikali vipande vipande bila kuwabakisha na kiwango kikubwa cha silaha kabla hajaichukua Rwanda. Kama angeliichukua Rwanda haraka hivi na Wahutu wenye silaha kukimbilia msituni wakiwa na kiwango kikubwa hivi cha silaha yawezekana mpaka leo hii bado Rwanda kungelikuwa na vita.
Sababu ya pili naamini Kagame alikuwa anajaribu kuwavuta zaidi jamii ya kimataifa kuwa upande wake na hakutaka kuonekana ni mroho wa madaraka.
Kwamba alikuwa anajaribu kuonyesha jamii ya kimataifa kuwa ana uwezo wa kuiweka Rwanda kiganjani mwake muda huo, lakini hakufanya hivyo ili kuwaonyesha kuwa haitaji madaraka (japo hilo ndilo lengo lake kuu) bali anataka amani Rwanda.
Huko nyuma Kagame alishafanikiwa kutengeneza taswira chanya kwa jamii ya kimataifa juu ya vikosi vyake vya RPF na kutokana na tukio hili Kagame alifanikiwa mno kupata mioyo ya viongozi wengi wa Kimataifa kuwa upande wake.
Na pia kama angeliichukua Rwanda kwa ushindi wa mara moja na kuindoa serikali iliyoko madarakani na kuingiza serikali yake… ingeweza kutafsiriwa kama amepindua wahutu na kuwarejesha watusi wenzake kwenye utawala wa Rwanda na ingeweza kuchochea vita isiyo na kikomo ya wenyewe kwa wenyewe kati ya wahutu na watusi. Na hili ndilo sababu hasa mpaka wamefikia hatua hii ya nchi kuwa vitani muda wote huo.
Pia au labda alikuwa anasubiri sababu kubwa zaidi ya kuhalalisha yeye kuchukua madaraka ya kuingoza Rwanda. Sababu kubwa zaidi ambayo hata jumuiya ya kimataifa itamuunga mkono na wasimuangalie kama mpenda madaraka.
Tukumbuke kwamba kagame ni 'born tactician, every move he makes means something.!'
Sababu hasa ya kufanya maamuzi ambayo aliyafanya February 20, 1993 ni yeye mwenyewe anaielewa.
Suala hili lilizua mpasuko mkubwa sana ndani ya RPF. Makamanda wenzake wakinung'unika kuwa amewanyima ushindi. Wengine bado wakilazimisha kwamba waivamie Kigali.
Lakini Kagame kutokana na nguvu aliyokuwa nayo na ushawishi wake akafanikiwa kuzima kelele zote hizi za wenzake na kufuata kile ambacho alikuwa amekiamua.
Ujumbe mkubwa zaidi ambao RPF walikuwa wameutuma kwa dunia ni kwamba RPF walikuwa na nguvu na weledi wa vita kuwazidi vikosi vya serikali.
Na Habyarimana alilijua hili. Hakutaka kuchelewa kabla 'mchele' haujamwagika wote. Safari hii ni yeye akamuomba Kagame warudi tena kwenye meza ya majadiliano.
Kagame alikubali. Siku mbili baadae walirejea kwenye meza ya majadiliano. Lakini safari hii kwa kuwa ni Habyarimana ndiye ambaye aliomba kurejea kwenye meza ya majadiliano hii ilimpa mwanya Kagame kutoa masharti yale ambayo alikuwa anayataka.
Mazungumzo haya hayakuwa Arusha tena kama awali, bali safari hii yalifanyika 'nyumbani' Uganda msuluhishi akiwa Rais Yoweri Museveni na wawakilishi kadhaa wa nchi za Ulaya. Hii ndio inaitwa kesi ya nyani kumpelekea ngedere.
Kagame alikuwa anawachezesha ngoma ambayo walikuwa bado hawajaijua… na muda si mrefu alikuwa anafikia lengo lake.
Itaendelea… Usikose!
Sent using
Jamii Forums mobile app