ENDELEA NA HISTORIA YA KWELI YA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA
Sehemu ya Sita.
Katika sehemu iliyopoita nilieleza namna ambavyo Watusi, Paul Kagame, Fred Rwigyema na wenzake walivyoingia kwenye vikundi vya kijeshi chini ya Museveni na kushiriki vita ya Kagera na baadae kushiriki katika kumuondoa madarakani Rais Milton Obote.
Katika sehemu hii ya sita nataka tuangalie namna ambavyo moto wa mauaji ya Kimbari ulivyowaka na hatimaye tuangalie namna ambavyo Paul Kagame ameibuka kuwa mtu mwenye nguvu zaidi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki na Ukanda wa maziwa makuu.
Ili kuelewa namna ambavyo mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yalivyoanza ni vyema kwanza kuelewa namna ambavyo RPF (chama tawala cha sasa nchini Rwanda chini ya Paul Kagame) ilizaliwa na kubadilika kutoka kuwa umoja wa wanaharakati na baadae kuwa kikindi cha kijeshi na sasa chama cha siasa
Turudi nyuma kidogo….
Baada tu ya Milton Obote kushika nchi kupitia uchaguzi ambao ulikuwa na utata mkubwa mwaka 1980 na hatimaye Yoweri Museveni kujitenga naye akishutumu uchaguzi kutokuwa wa haki na kuanzisha kikundi chake cha National Resistance Army, Milton Obote mara moja alianzisha kampeni ya kukipiga vita kikundi hicho kwa nguvu ya jeshi lakini pia kwa propaganda akishutumu kuwa kikundi hicho kiko chini ya "Banyarwanda" (watu wa Rwanda) na si raia wa Uganda.
Hii ilipelekea mwaka 1982 serikali ya Milton Obote kulazimisha Watusi wote waliopo nchini Uganda kuwa wanapaswa kuishi kwenye kambi za wakimbizi pekee na si mitaani kama raia.
Ikumbukwe kwamba Watusi wamekuwa wakiikimbia Rwanda tangu miaka ya 1960s, hivyo wengi wao walikuwa wamelowea Uganda, Congo na hata Tanzania na kufikia hatua ya kuishi maisha ya kawaida uraiani kama raia wengine wa nchi hizo. Kwa hiyo kitendo cha Milton Obote kutangaza kwa hakuna Mtusi anayeruhusiwa kuishi uraiani isipokuwa kwenye kambi za wakimbizi pekee ilizua taharuki kubwa sana.
Watusi wote ambao walikuwa bado wanajificha na kuendelea kuishi uraiani, walikamatwa na kufungwa na wengine kuuwawa.
Hata kwenye kambi za wakimbizi zenyewe nako Obote aliweka mashushushu ambao waliwakamata Watusi ambao walionekana kuwa na misimamo mikali kupinga serikali yake au kumuunga mkono Museveni na kikundi chake cha NRA na kisha kuwatia jela na wengi wakipotezwa kusikojulikana.
Hii ilipelekea kuibuka kwa wimbi la wakimbizi wa Kitusi wapatao 40,000 kukimbia Uganda na kurudi Rwanda. Ubaya zaidi walipofika Rwanda kutokana na wakimbizi hawa kiwa Watusi serikali ya Rais Juvenile Habyarimana ilitangaza kuwatambua watu 4000 pekee kati ya wote 40,000 waliorejea.
Kati ya hao waliobaki na kukataliwa kurejea Rwanda, serikali ya Uganda chini ya Milton Obote ikatangaza kwamba itawachukua wakimbizi 1000 tu.
Kwa maana hiyo walisalia watu 35,000 katikati ya mpaka wa Rwanda na Uganda wakiwa hawana kwa kwenda. Rwanda nyumbani kwao serikali ilisema haiwatambui, na Uganda ambako waliishi kwa miaka kadhaa nako serikali ilisema haiwataki tena na haiko tayari kuwaruhusu kuingia. Kwa hiyo wakabaki kwenye ombwe la sintofahamu kubwa.
Kama nilivyoeleza huko nyuma kwamba Paul Kagame ni 'born tactician' anajua ku-capitalise katika mazingira yote. Yaani anajua kuona fursa katika kila mazingira na muda mwingine hata kushawishi mazingira yatengeneze fursa.
Wanyarwanda hawa 35,000 ambao walisalia mpakani wakikataliwa na nchi yao ya Rwanda na ugenini Uganda walikaa mpakani kwa kipindi kirefu sana. Ndipo hapa Paul Kagame akaanzisha programu maalumu za propaganda na kushawishi vijana wa Kitusi walioko pale mpakani (kati ya wale 35,000) kujiunga na NRA ya Museveni ambaye yeye na Fred Rwigyema walikuwa ni waanzilishi wake wakishirikiana na Museveni.
Nieleze pia jambo lingine muhimu…
Wakati haya yote yanaendelea, ikumbukwe kwamba tangu mwaka 1979 baada tu ya Idi Amin kupinduliwa kutoka madarakani, Watusi wote walioko Uganda walianzisha taasisi yao iliyoitwa Rwandese Alliance For National Unity (RANU). Hii ilikuwa ni taasisi ya kwanza ya kisiasa kuwa chini ya 'wakimbizi' Afrika Mashariki. Lengo kuu la Taasisi hii ilikiwa ni kuratibu mipango ya kurejesha watusi wote nchini Rwanda kwa amani.
Turejee tena kwenye kile nilichokuwa naeleza…
Vijana wa Kitusi ambao walikuwa mpakani pamoja na wale wengine 35,000 wakashawishiwa kujiunga na NRA ya akina Museveni, Rwigyema na Kagame.
Nilieleza kwa uzuri kabisa namna ambavyo Milton Obote aliondolewa madarakani na NRA… sasa mpaka mwaka 1986 ambapo Milton Obote alitolewa madarakani, NRA ililuwa na wapiganaji wapatao 16,000 na nusu yao walikuwa ni Watusi.!
NRA ikashika nchi, Museveni akawa Rais, Fred Rwigyema Waziri wa Ulinzi na Naibu Amiri Jeshi Mkuu, na Paul Kagame Mkuu wa Intelijensia ya Jeshi na Watusi wengi kupata nyadhifa za juu na nyeti katika jeshi na serikali ya Uganda.
Paul Kagame na Fred Rwigyema walitumia ushawishi wao na kuifanya serikali ya Museveni kutangaza kuwapokea tena Watusi wote ambao walisalia pale mpakani kutokana na kukataliwa na Rwanda na serikali ya Milton Obote. Lakini pia serikali ya Uganda ilitangaza kwamba Watusi wote ambao wamekaa Uganda kwa miaka 10 au zaidi watapatiwa uraia.
Huu ulikuwa ni moja kati ya wakati wa raha zaidi kwa Watusi. Ilikuwa ni neema kubwa. Shukrani zao japo zilikwenda kwa serikali la Uganda lakini shukrani za dhati na zaidi zilikwenda kwa vijana wao Paul Kagame na Fred Rwigyema kwa kufanikisha kuileta Neema hii.
Fred Rwigyema na Paul Kagame wakageuka kuwa mashujaa katika jamii ya Watusi.
Sasa basi…
Ile RANU ambayo nimeeleza hapo awali huwa ilikuwa inafanya Kongamano kuu kila mwaka kujadili uratibu wa mikakati ya kurejea tena Rwanda.
December mwaka 1987 likafanyika Kongamano kuu la saba la RANU jijini Kampala. Katika Kongamano hilo Fred Rwigyema akachaguliwa kiongozi wa taasisi hiyo na Paul Kagame akiwa Makamu wake.
Nafasi nyingine zote za uongozi na nafasi za kiutendaji waliwekwa maveterani ambao walipigana katika vita za kumng'oa Idi Amin na kumng'oa Milton Obote.
Kwa hiyo kufumba na kufumbua RANU ilibadilishwa kutoka kuwa taasisi ya kisiasa na kuwa chombo cha kijeshi. Na Rwigyema na Kagame hawakuishi hapo tu bali waliibadilisha jina RANU na kuwa Rwanda Patriotric Front (RPF).
Kwa hiyo ilikuwa rasmi sasa kwamba Paul Kagame na Fred Rwigyema walikuwa na misuli ya kijeshi kufanya kile ambacho walikuwa wanakiota tangu wangali watoto.
Walikuwa na maelfu ya vijana wa kitusi mikononi mwao ambao walikuwa na weledi wa kutosha wa kijeshi kutoka NRA ya Museveni na kwa sasa waliwasajili chini ya kikundi chao kipya cha RPF.
Sasa ulikuwa muda sahihi kabisa wa kwenda kuiweka Rwanda kwenye kiganja cha mikono yao na kuisuka upya vile ambavyo walihisi ni sahihi.
Yoweri Museveni
Jaribio la Kwanza - Octoba, 1990
Mwanzoni mwa mwezi huu octoba, Rais Juvenile Hibyarimana alikuwa amesafiri kwenda Marekani Kuhudhuiria Kongamano la Kimataifa kuhusu watoto ambalo liliandaliwa na Umoja wa Mataifa.
Rais Yoweri Museveni naye pia alikuwa Marekani kuhudhuria Kongamano hilo hilo.
Pual Kagame naye alikuwa Marekani kwa miezi kadhaa sasa kwa ajili ya kozi maalumu ya kijeshi katika chuo cha kijeshi cha Command and General Staff Collage kilichopo kambi ya Leavenwortg huko Kansas.
Kwa miezi kadhaa Kagame na Rwigyema walikuwa wakiwasiliana kwa simu kupanga mikakati ya kumuondoa madarakani Rais Juvenile Hibyarimana na serikali yake ya Kihutu.
Fursa hii ya Rais Hibyarimana kutowepo ndani ya nchi ilikuwa ni fursa adhimu kwao kutekeleza azma yao.
Kwa hiyo mpango ambao walikuwa wakiupanga kwa miezi kadhaa ulikuwa umefika muda wake wa kuutekeleza.
Kwa hiyo siku ya tarehe 1, october 1990 majira ya saa mbili na nusu usiku.… wanajeshi wa weledi wa juu (Special Forces) wenye asili ya Kitusi wapatao 50 waliondoka kutoka kwenye kambi zao za jeshi la Uganda kuufuata mpaka wa Rwanda na Uganda.
Walieleke moja kwa moja mpaka eneo la mpakani la Kagitumba ambako waliwatandika risasi walinzi wa mpaka mahali hapo na kusonga mbele kuingia Rwanda. Kama muda wa saa moja baadae walifuatiwa na maelfu mengine ya wanajeshi ambao walikuwa wamevalia sare za jeshi la Uganda.
Hawa waliluwa ni wanajeshi Uganda sawia kabisa lakini wenye asili ya Kitusi.
Walikuwa na silaha nzito nzito kama vile mashine guns, autocannons, vifaru, pamoja na rocket lauchers aina ya BM-21, vyote hivi vilitoka kwenye jeshi la Uganda.
Jeshi la serikali ya Rwanda walikuwa na wanajeshi wengi zaidi pamoja na vifaa bora zaidi kama vile magari ya kivita pamoja na helikopta ambazo walikiwa wamezipokea kama msaada kutoka kwa nchi ya Ufaransa miezi michache iliyopita. Lakini walikuwa wamezidiwa kete moja adhimu kwenye medani ya vita… hawakujiandaa!!
Shambulio hili lilikiwa ni la kushitukiza kwao na hawakuliona likija kwa hiyo vijana wa RPF walikuwa wamejiandaa kiakili na kimkakati kuzidi jeshi la Rwanda. Na zaidi ya yote walikuwa na 'mbabe wa vita' Fred Rwigyema akiwaongoza kwenye oparesheni hiyo ya kushtukiza.
Vijana wa RPF walienda kwa kasi mno na walikuwa wanafanikiwa kwa haraka mno kutimiza lengo. Ndani ya masaa machache walikuwa wameingia zaidi ya kilomita 60 ndani ya Rwanda waliuweka mji wa Gabiro mikononi mwao.
Ndani ya siku moja tu RPF walikuwa wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana na ilikuwa dhahiri kwamba majeshi ya serikali yalikuwa yamezidiwa nguvu na RPF. Kulikuwa na kila dalili kwamba muda wowote kuanzia siku ya pili ya uvamizi huo wa RPF mji wa Kigali ulikuwa unaelekea kuwekwa chini ya Himaya ya RPF na huo ndio unaweza kuwa ndilo anguko la serikali ya Rais Juvenile Hibyarimana.
Lakini kuna jambo la ajabu kabisa likatokea. Jambo ambalo kwa kufikiria kwa haraka haraka lilikuwa haliwezekani kabisa. Katika siku ya pili vikosi vya RPF vikiwa vimewazidi nguvu majeshi ya serikali na wakielekea kuiweka kigali mikononi mwao… katika mzingira ya kutatanisha sana, mwanajeshi na jasusi mbobezi wa uwanja wa vita kuwahi kutokea ukanda huu wa Afrika Mashariki, Fred Rwigyema aliuwawa kwa kupigwa risasi.
Nasema ilikuwa ni jambo la ajabu kwa kuwa vijana wa RPF walikuwa wamewazidi nguvu majeshi ya serikali na walikuwa wanaelekea kuiweka mikononi mwao mji wa Kigali. Lakini jambo la ajabu zaidi Rwigyema aliuwawa akiwa kwenye base (kambini) sio akiwa 'front line' au kwenye mapambano.
Kila mtu kuanzia wapiganaji wa RPF na mpaka viongozi wa jeshi la Rwanda walibakiwa na bumbuwazi wasielewe ni nini ambacho kilikuwa kimetokea. Inawezakanaje Rwigyema auwawe kirahisi hivi tena akiwa kwenye base sio 'front line'? Kulikuwa na kila harufu ya hila kuhusika kwenye kifo hiki. Na mtu pekee mwenye uwezo wa weledi na uthubutu kumfanyia hila ya namna hii komando na jasusi mbobezi wa kaliba ya Fred Rwigyema ni mtu ambaye naye ni mwenye weledi na ubobezi wa kufanana na Rwigyema au kumzidi na si vinginevyo.
Ndipo hapa ambapo unadhihirika msemo wa kwamba kwenye maisha hakuna rafiki au adui wa kudumu… bali kitu pekee ambacho ni cha kudumu ni maslahi.
Yoweri Museveni ambaye nyuma ya pazia alikuwa anajua kila kitu kuhusu uvamizi huu na huku akisaidia kwa siri waasi wa RPF baada ya kupewa taarifa hii ya kuwawa kwa Rwigyema naye alipatwa na mshtuko mkubwa asielewe nini ambacho kilikuwa kimetokea.
Wote wawili, yeye na Kagame walikuwa nchini Marekani, Kagame akiwa Kansas na yeye Museveni akiwa New York. Moja kwa moja akainua simu kumpigia kagame akiwa na swali moja tu la kuuliza… "qu'est-ce qui s'est passé?" (Nini kimetokea?)
Alihisi kabisa… na pengine alijua kabisa kuwa Paul Kagame anajua cha zaidi kuhusi kifo cha Fred Rwigyema.
Itaendelea...
Sent using
Jamii Forums mobile app