Kitu kimoja nilicho na hakika nacho kwa asilimia 100% ni kwamba wale wote wenye mapenzi ya kweli kwa taifa letu la Tanzania wanasita sana kuchangia hii hoja inayofinyangwafinyangwa na huyu anayejiita Mohamed Said. Bila kumung'unya maneno nayaita madai ya Mohamed Said la kutoa elimu ya historia ya kweli ni porojo hatari iliyojaa uchochezi ambayo lengo lake hasa ni kuleta uhasama wa kidini miongoni mwa wananchi. Sijui anachotegemea kufaidika nacho kwa kupanda hii mbegu ya hatari ambayo nina hakika mtu kama Mohamed Said anajua fika madhara yake.
Mohamed Said ni kama kipofu ambaye baada ya kusimuliwa na wazee kwamba tembo ni mnyama mkubwa kuliko wanyama wengi anapata nafasi ya kumpapasa tembo. Kwa bahati mbaya anaupapasa mguu wa tembo na si mwili wote halafu katika imani yake anadai anao uwezo wa kutoa somo kuhusu umbo la mnyama tembo na ushuhuda wake, kuwa tembo ni kama gogo la mti mkubwa, ndio ukweli na anayesema tofauti hajui kitu. Watu wote wanaolalamikiwa na Mohamed Said kuwa walisahauliwa, wengi wao walikuwa wakazi wa Dar es Salaam eneo la Gerezani.
Kabla ya uhuru Tanganyika iligawanywa katika majimbo makuu manane na katika majimbo yote hayo, jimbo la pwani kwa ujumla lilikuwa moja ya majimbo yaliyokuwa nyuma kimaendeleo kiuchumi, kielimu na kisiasa na hiyo ni licha ya kuwa makao makuu ya serikali ya kikoloni yalikuwa Dar es Salaam. TAA ilianzishwa na watumishi wa serikali (civil servants) na kwa wakati wote kazi kubwa ya TAA ilikuwa ni kulalamika ikidai haki ya wafanyakazi bila upendeleo na hasa ubaguzi wa rangi katila utumishi kubwa ukiwa uonevu dhidi ya wazawa, mtu mweusi.
Jimbo la Ziwa ni moja ya majimbo yaliyokuwa mbele kiuchumi, kielimu na kisiasa na kama kuna kitu kinaweza kudaiwa kuwa kilisahaulika katika harakati ya kupigania uhuru ni mchango wa Jimbo la Ziwa (Bukoba, Mwanza, Mara na Shinyanga) Jimbo la Ziwa ndilo lililoongoza kwa idadi ya watu, idadi ya makabila, idadi ya mali asili na idadi ya machifu ambao nafasi yao ilikuwa kubwa tu katika kuhamasisha watu. Moja wa watu ambao mchango wao nitautaja kidogo tu ingawa alifanya jitihada kubwa labda zaidi ya wazee wa Mohamed Said ni Paul "Kishamapanda" Bomani.
Historia ya harakati za uhuru ni zaidi ya porojo za Mohamed Said, watu walipigania uhuru kama Watanganyika na bila kubaguana kikabila, kidini wala kijinsia. Ndio maana mimi sitaki kabisa kuwa na majibizano na huyu Mohamed Said moja kwa moja ila kwa kuwa hoja ileletwa JF, akae tayari kupewa somo kuhusu umbile zima la mnyama tembo na sio mguu moja wa tembo alioupapasa. Hapa mimi nitaongea sana kuhusu mchango wa Jimbo la Ziwa na baadaye kuonyesha jinsi maadui wa nchi yetu wanavyowatumia kidini watu kama huyu Mohamed Said.
Baadaye nitaeleza jinsi Mkoa wa Mara yenye makabila karibu hamsini yalivyoweza kushirikiana bila mfarakano na kuitikia mwito wa Mwalimu Nyerere katika hizo harakati za kudai uhuru. Je mwamko wa wakazi wa jimbo la Ziwa ulikuwaje na mapokezi gani aliyapata kila wakati Mwalimu aliporudi kwenye hili jimbo ambalo idadi ya wakazi wake kwenye miaka ya 50s ilikuwa mara tatu ya majimbo mengi Tanganyika kama Pwani. Pia nitaonyesha ni wakati gani walianza kuyasikia hayo majina anayodai Mohamed Said ya wazee wa Gerezani Dar es Salaam !