Mohamed, mbona unachanganya wasomaji?
Huko nje unaeleza ni historia ya Nchi, hapa nyumbani unatueleza kitu tofauti, soma hapa chini kauli yako
''Mohamed Said said:
Syll...
Mimi nakuhadithieni historia ya nyumbani kwetu nimeandika kitabu cha historia ya jamii yangu ambayo kabla haikuwapo.''
Si akina Shivji wameandika wakaja kukuhoji baada ya hapo ''ukanuna' hawakuandika ulivyotaka. Ukadai 'wamepotosha'' au umesahau
Wanakila sababu ya kushangaa kwasababu hukuwaeleza ukweli.
Wao wanajua ni historia ya Tanganyika kumbe wewe unajua ni ya
'nyumbani kwetu nimeandika kitabu cha hostoria ya jamii yangu ambayo kabla haikuwepo''
Mohamed, Wanafunzi watafanya vipi reference ya '' historia ya nyumbani kwako'' kwa mujibu wako. Kuna kosa gani kwa wahadhiri ambao pengine leo wanakusoma na kubaini historia pendwa au ngano hii inahusu Familia.
Mag3
Nguruvi...
Kuwa historia hii ni historia ya nyumbani kwetu ndicho kitu kinachofanya historia hii iwe tofauti na zote zilizopata kuandikwa kuanzia Kimambo na Temu (1969), Uloto (1971), Chuo Cha CCM Kivukoni na Shivji at.al (2020).
Msome Daisy hapo chini.
Utangulizi nimeandika mimi:
''Aisha ‘’Daisy’’ Sykes Buruku ni binti ya Abdulwahid Sykes mmoja kati ya wazalendo 17 waliounda chama cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanganyika.
Daisy kama anavyofahamika zaidi kwa jina hili, ni msichana wa kwanza Mwafrika kusoma Shule ya Wasichana ya Aga Khan mwanzoni mwa miaka ya 1950 na msichana wa pili kuingia Chuo Kikuu Cha Afrika ya Mashariki, Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 1960.
Daisy amefahamiana na wazalendo wengi mmoja wapo akiwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na machifu mashuhuri kama Mangi Mkuu Thomas Marealle waliokuwa wakifika nyumbani kwa baba yake wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Katika kuadhimisha miaka 50 ya kifo cha baba yake, Daisy ameandika makala haya kukumbuka siku zile zilizojenga haiba ya baba yake na ya wazalendo walioshiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika.
Kwa miaka mingi Daisy amekuwa akiishi na kufanya kazi nje ya Tanzania.''
Daisy anaeleza:
''Lakini kile ambacho kimeathiri fikra zangu na kubakia na mimi katika kumbukumbu zangu ni kufika pale nyumbani kwa uongozi wa juu wa Waafrika kabla ya uhuru, machifu kutoka makabila mbalimbali ya Tanganyika na viongozi wa vyama vya wazalendo vilivyokuwa ndiyo vinainukia, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi Waafrika katika wa serikali ya kikoloni.
Kutokana na hadhi hii ya baba yangu na umaarufu wake na kule kupenda kukirimu watu, nikawa si mgeni kwa machifu mashuhuri na nikawa nawahudumia walipokuwa mara nyingi wakija nyumbani.
Wageni hawa mashuhuri waliokuwa wakija nyumbani ni pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle, Machifu Abdiel Shangali, John Maruma kutoka Moshi, Adam Sapi Mkwawa kutoka Iringa, Kidaha Makwaia kutoka Usukuma, Abdallah Fundikira, Harun Lugusha kutoka Tabora, Humbi Ziota kutoka Nzega, Michael Lukumbuzya kutoka Ukerewe na Patrick Kunambi kutoka Morogoro na wengine wengi.
Hawa machifu kwa kawaida walikuwa wakija na wake zao, wanawake warembo ambao hawakuacha kunifanya mimi kuwashangalia.
Nakumbuka katika machifu wale, alikuwapo chifu mmoja na wa pekee mwanamke - Mwami Theresa Ntare kutoka Kasulu Kibondo.
Katika hali kama hii iliyokuwa tabu kufahamika, tukiwa watoto tulipata kujua maisha ya jamii nyingine, lugha zao, utamaduni wa makabila mengi ya Tanganyika kabla ya watu wengi kutoka sehemu nyingine za pwani hawajajua chochote kuhusu watu hawa.
Nilibahatika kukutana na katika utoto wangu na lile tabaka la Waafrika waliokuwa watumishi wa serikali, kundi dogo makhsusi lililokuwa linakua na liliopembuka kwa elimu zao kutoka Chuo Cha Makerere, Uganda na vyuo vingine.
Hiki ndicho kilikuwa kizazi kipya cha Watanganyika wasomi waliohusika na kuasisi siasa fikra ya uhuru itakayopelekea Waafrika kujitawala - Hamza Mwapachu, Zuberi Mtemvu, Mzee John Rupia, Steven Mhando, Dunstan Omari, Dossa Aziz kwa kuwataja wachache.
Kulikuwa pia na tabaka jingine la watu maarufu kutoka Zanzibar kama Ahmed Rashad Ali and Abdul Razak Abdul Wadud ambao walikuwa kama sehemu ya familia yetu.
Siwezi kumsahau Maloo, Mburushi kutoka Congo ya Mashariki ambae alikuwa anakaa nyumbani na baba kwa muda mrefu sana kiasi tuliamini ni mmoja katika familia ya Sykes.
Lakini aliyeshika nafasi ya juu kabisa katika fikra zangu nikiwa mtoto alikuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni kupitia kwake ndipo tukapata kujua kwa mara ya kwanza kuwa kuna kabila linaitwa, ‘’Wazanaki.’’
Kila alipokuwa anakuja nyumbani kwetu kuja kwake kulikuwa jambo maalum kulikosababisha minong’ono watu wakizungumza kwa sauti za chini wakipeana taarifa kuwa, ‘’Nyerere anakuja au keshafika.”
Kwangu mimi hii ilikuwa ishara ya kutimiza kazi yangu kwani siku zote nilikuwa nikiambiwa kutengeneza kifungua kinywa cha chai na mayai kila alipokuja nyumbani akitokea Shule ya Mt. Francis, Pugu alipokuwa akisomesha.''
Daisy anaendela kueleza:
''Nakumbuka katika akili yangu ya kitoto kumuona Mwalimu Nyerere akiishi nyumbani kwetu kwa muda katika nyumba yetu ya Mtaa wa Stanley baada ya kuacha kazi wakati marafiki zake wa karibu baba na Dossa Aziz walikuwa wanamtafutia nyumba ya kuishi.
Nyumba yetu ya Stanley kwa kuwa ilikuwa kwenye makutano ya barabara mbili ilikuwa na mjengo wa kipekee kwa nyakati zile.
Nyumba kubwa na yenye vyumba kadhaa ilikuwa upande wa Mtaa wa Stanely na upande wa Mtaa wa Sikukuu ilikuwa nyumba nyingine inayojitegemea ikiwa na sebule na chumba cha kulala hapo hapo.
Ingawa upande huu wa nyumba ilikuwa na nafasi ya kutosha ilikuwa vigumu kwa wanaume wawili wakubwa kuishi pamoja.
Naamini baba yangu mdogo Abbas ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba ile ikabidi ahame aende kweye nyumba yetu nyingine Mtaa wa Kipata au ajibane nyumba kubwa ili Mwalimu Nyerere apate utulivu na faragha katika nyumba ile.
Mwalimu Nyerere na Hamza Mwapachu ni watu walionivutia sana mimi kwa kiwango cha juu kwa namna walivyokuwa wakilitamka jina langu, ‘’Daisy,’’ kwa lafidhi yenyewe ya Kiingereza kama wanavyozungumza Wazungu na hii ikalifanya jina hili langu la utani linigande na liwe ndilo jina langu halisi.
Nikiwa mtoto nakumbuka sana vipi baba akishughulishwa na kutaka kuona kuwa Mama Maria na watoto wake hawakosi chochote kuyafanya maisha yao kuwa mepesi, ya starehe na furaha akihakikisha chakula kinapelekwa dukani kwa Mama Maria kila siku katika duka lake dogo lilikuwapo Mtaa wa Livingstone kona na Mtaa wa Mchikichi, hiki kikiwa kielelezo chake kikubwa kabisa cha huruma na ukarimu wake.
Ilikuwa katika kipindi hiki cha mimi kuanza kupata akili katika kukua kwangu ndipo nilipokutana na wanawake wazalendo waliokuwa wanaochipukia katika uongozi wa Tanganyika, wanawake kama Bi. Lucy Lameck kutoka Moshi, Mary Ibrahim na akina mama wa Kiislam kama Bi. Titi Mohamed, Bi. Tatu bint Mzee, Bi. Hawa bint Maftah, hawa kutoka Dar es Salaam, wote hawa kwangu mimi walikuwa bibi zangu.
Kitu cha kufurahisha ni kuwa hawa akina mama wa Kiislam wote walivutwa katika siasa na Bibi Chiku bint Kisusa, maarufu akijulikana kama Mama Sakina.
Alikuwa Mama Sakina ndiye aliyewapa hawa wanawake wa Kiislam niliowataja hapo juu utambulisho na wakaja kuwa watu maarufu.
Baba yeye ndiye alikuwa kiongozi wa mikakati hii yote kwa sababu bila yeye kuwatia hima kwa kutumia ushawishi wake ingekuwa vigumu kuweza kuwatia hawa wanawake katika kuwahamasisha wanawake wenzao wa Kiislam na wao watoke majumbani kuja mstari wa mbele katika mikutano wakiimba na kutoa vibwagizo vya kuunga mkono TANU na kudai uhuru.
Hili jambo lilikuwa jipya, jambo ambalo katika utamaduni wetu kwa wakati ule halikutarajiwa na ni kinyume katika utamaduni wetu kwa wanawake wa Kiislam kulifanya katika siku zile.
Nimesikia mazungumzo mengi wakati baba na wenzake walipokuwa wakijadili majina na shughuli ambazo hawa akina mama walikuwa wahusishwe ili kuleta mvuto wa kisiasa katika mikutano yao ya TANU.
Nakumbuka vizuri sana jinsi baba alivyokuwa karibu sana na Mwalimu Sakina na ndugu yake Mwalimu Fatna (wote hawa watoto wa Mama Sakina), na jinsi alivyowaleta ndugu hawa karibu na Mama Maria na hawa wakamjulisha Mama Maria Nyerere kwa mama yao na mashoga zake Bi Hawa Maftaha, Bibi Titi Mohamed na Bi Tatu binti Mzee.
Hawa wanawake ndiyo waliomsaidia Mama Maria kufungua hilo duka lake dogo pale Mtaa wa Livingstone kona na Mchikichi, mahali ambako Mama Maria alishinda kutwa nzima akiuza duka lake.
Nikiwa mtoto nakumbuka kwenda kwenye dula lile kila siku mchana kupeleka chakula kwa Mama Maria, ambako hapakuwa mbali kutoka nyumbani kwetu.
Kwa kuwa baba alikuwa anataka ratiba hii yake ya chakula ifuatwe sawasawa kwa wakati wake, wakati mwingine hii ilikuwa changamoto kubwa sana kwa mama yetu, Bi. Mwamvua bint Mashu.''
Bwana Mag,
Ikiwa wewe au yeyote yule ana ukweli zaidi wa huu na aulete hapa barzani tuusome.
Hakika haya yote ni ya nyumbani kwetu wala hatuoni aibu kujifakharisha na historia hii.
Jirani na nyumba hii ya Abdul Sykes ipo nyumba ya bibi yangu na ipo hadi leo ingawa nyumba yote mbele ni maduka.
Si mbali na hapo ilikuwa nyumba ya Mzee Kubhe, Tewa Said Tewa na nyumba ya Ramadhani Fundikira.
Katika historia hii hakika mimi niko nyumbani kwetu.
Kulia ni Mama Sakina Bi. Chiku bint Said Kisusa, mke wa Shariff Abdallah Omar Attas, Bi. Titi Mohamed na wa kwanza kushoto ni Bi. Tatu bint Mzee na Julius Nyerere huyo katikati Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam wanamsindikiza Mwalimu safari ya kwanza UNO Februari, 1955. Sina majina ya hao akina mama wengine.