Bila shaka yoyote kuna wana JF wengi labda wanajiuliza kwa nini sitaki kuwa na majibizano ya moja kwa moja na huyu mchochezi anayejiita Mohamed Said. Mwanzoni nilifikiri huyu bwana kweli ana nia ya kuandika historia ya watu waliochangia kwa namna mbalimbali katika harakati zetu kama Watanganyika kupigania uhuru wa nchi yetu. Hivyo mimi pamoja na wachangiaji wengine kwa nia njema kabisa tulijaribu sana kumwelimisha kuwa si kweli hao wazee wake wa Gerezani ndio waliotoa mchango mkubwa kuliko Watanganyika wengine. Dar es Salaam ambako ndiko yalikuwapo makao makuu ya serikali ya kikoloni, pamoja na kuwa mji mkuu wa Tanganyika, kalikuwa kamji kadogo chenye wakazi wasiofikia hata laki mbili. Dar es Salaam ilikuwa ndani ya Jimbo la Pwani, moja ya majimbo manane nchini Tanganyika, na liliunganisha ambayo hivi sasa yanajulikana kama Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Pwani na Mkoa wa Dar es Salaam yenyewe.
Kwa sababu lengo hasa la Mohamed Said halikuwa la kuandika historia ya kweli kama alivyodai mwanzoni, badala ya kutupongeza wengine tuliokuwa tukimpa somo kuhusu Watanganyika ambao yeye hayuko tayari kuwataja kabisa ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, akaanza kutukejeli kuwa na sisi kama tunataka tuandike historia yetu. Baada ya hapo tukamshauri kwamba kama ni hivyo, basi hiyo historia anayoiandika aseme wazi kabisa ni ya Wazee wake wa Gerezani na asithubutu kudai kuwa ni ya Watanganyika. La haula ! Mohamed Said kwa chuki ambayo imetawala hisia zake potofu, akashindwa kuficha tena hasa lengo lake - anapiga vita dhulma waliyofanyiwa na wanayoendelea kufanyiwa Waislaam pamoja na kwamba wenyewe ndio walitoa mchango mkubwa katika kudai uhuru. Mohamed Said, bila kificho, anadai haya ni mapambano dhidi ya mfumo Kristo ambao umetumiwa kukandamiza Uislaam toka na baada ya uhuru.
Mimi Mag3 nimejaribu kumweleza kuwa pamoja na kuwa na uelewa mkubwa wa mambo ya siasa katika miaka ya 1950's sikuwahi kuwasikia wala kuwaona hao wazee wa Mohamed wa Gerezani. Pamoja na kufika Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwazoni mwa miaka ya 1960 baada ya uhuru sikuwasikia hawa Wazee ukiacha Zuberi Mtemvu ambaye jitihada zake, pamoja na mapungufu yake ya kimkakati, hazikumfikisha mbali. Tumejaribu kumwelewesha Mohamed Said jinsi TAA ilivyoundwa mwaka 1929, malengo yake yaliyoainishwa katika katiba na uendeshwaji wake kwa kutojihusisha na mambo ya siasa. Wengine tumempa somo kuhusu maraisi wa TAA (waliokiongoza) tangu kuundwa kwake na Gavana Cameron hadi kuundwa TANU (chama cha siasa) mwaka 1954 na Mwenyekiti wa TANU tangu wakati huo hadi tunapata uhuru. Tumemwomba awataje hao wazee wake walioongoza hivyo vyama, yeye kakazania porojo za wazee wake !
How convenient kwa wenye mawazo potofu kama Mohamed Said kuwa mbinu za kuhusisha Ukristo na mfumo wa serikali baada ya uhuru hazingeweza kufanikiwa bila kwanza kumchafua Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Na kumchafua Mwalimu hakungeweza kufanikiwa bila kuzua kinachoitwa chuki yake dhidi ya Uislaam na hivyo kuwateka Waislaam ambao mathalan dini imehusishwa, watatetea mada mradi mtoa mada ni Muislaam mwenzao. Bahati nzuri Waislaam wa Tanzania walio wengi (hasa ninaoshirikiana nao - marafiki, ndugu na comrades) wanaelewa fika hizo mbinu chafu zenye kujali maslahi ya watu wachache na si taifa letu tunalolipenda la Tanzania na hawako tayari kuzibariki bila tafakari. Hii ni moja ya sababu inayonizuia kujibizana na Mohamed Said moja kwa moja (people might not notice the difference) na ninawaachia Waislaam hawa wenye mapenzi ya kweli na taifa letu, wachambue mchele na pumba katika haya ninayoyaandika.
Juzi kuna kundi la Waislaam wamejitokea na bila kificho wamewaagiza waumini wao wasikipigie Chadema kura ! Ni bahati gani tamko kama hili halikutolewa na kikundi chochote cha Kikristo, lakini nachelea kusema kwa uhakika kuwa lingetokea hilo hivi sasa tungekuwa tunaongelea mengine. Katika uchaguzi wa mwaka 2010 alianza mwandishi wa gazeti la serikali kwa jina Ali Mkumbwa akatumia maneno yenye mtizamo na mwelekeo kama huo lakini hadi leo anaendelea kuchapa kazi bila wasi wasi katika mfumo Kristo. Watu kama Mohamed Said tusiwapuuze, nyuma yake kuna kubwa zaidi ya hili la kudai kuandika historia ya kweli na bila shaka hii mada inavyoendelea anazidi kujifunua kwa sura yake halisi - nimesoma kwa makini michango yake ya karibuni ambayo yaonyesha kabisa kuwa anataka nini. Anadai Uislaam unawapa watu woga na anaonya kuhusu yatakayotukuta sisi wazalendo ambao tumetanguliza Utaifa mbele ya Udini anaoupaka rangi akisahau hiyo rangi haibadilishi umbile.
Tumemtolea Mohamed Said mifano kuwa katika harakati zote za kudai mabadiliko popote pale duniani kimfumo au kiutawala, lazima anatokea kiongozi ambaye hupata sifa za pekee na huyu si mwingine ila ni yule anayefanikisha malengo ya harakati hizo. Mtanganyika hakutakiwa kusafiri hadi Dar es Salaam ndio awajue Wazee wa Gerezani na laiti hao wazee wangekuwa maarufu kiasi hicho, hawangemhitaji Mwalimu Nyerere aje awaongoze lakini nakumbuka katika ujana wangu jina tu Nyerere lilivyoenea mpaka kijijini na hadi leo, CCM inapokwama inamtumia Nyerere kama mtaji wake. Kwa nini hata Lindi, jina la Nyerere litajwe kwenye kampeni na wagombea na si la akina nani vile ! Abdul Sykes ! Jamani tuache hizi soga zisizokuwa na kichwa wala miguu, hadi watoto walizaliwa wakati huo wakaitwa Nyerere Mikindani hadi Kibondo, Usangi hadi Tukuyu na Mafia hadi Tumbatu. Na hapo bado Auckland hadi Edmonton, Kyoto hadi Guyana na Cape Town hadi Tripoli.
Nimeeleza Mwalimu alivyoona aibu kuongoza nchi huru na huku mji wake mkuu, ukiacha Uhindini na Uzunguni, wazawa wanaishi kwenue nyumba za makuti. "Operation Makuti" ilianzishwa makusudi kuwapa makazi bora hawa watu inaodaiwa Mwalimu hakutaka wapate maendeleo na hili ndilo lilikuwa lengo kubwa la kuanzishwa kwa Shirika la Nyumba. Wana JF mtafakari na muamue wenyewe kuhusu michango ya Watanganyika mbali mbali na "sacrifices" ambazo ilkuwa ni lazima zifanyike ili tuweze kujenga taifa lenye umoja na mshikamano. Kwa bahati nzuri au mbaya, Raisi wa chama cha siasa anaweza kuwa moja tu na Raisi wa nchi anaweza kuwa moja tu, na historia kamwe haitafuta ukweli kwamba Raisi wa Kwanza wa TANU na Raisi wa kwanza wa Tanganyika huru angeweza na alikuwa moja tu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Wanaolilia wazee wao, wakumbuke tu kitu kimoja, mtu aliyeongoza harakati hizo alipatikana kwa kura baada ya kuwa na sifa kuwashinda wengine.