Mwanakijiji,
Huko kote tushapita.
Siwezi kukuzuia kufikiri upendavyo.
Muhimu kwangu ni watu wajue ipo historia nyingine na hili ni maarufu ndani na nje ya nchi kupitia "papers" zangu na kitabu nilichoandika.
Historia rasmi leo ina mwenza.
Nami Insha Allah naendelea na darsa.
Mohamed
Nikusahihishe kwanza. Historia haina mwenza. Kuna historia kamili au isiyokamilika. Historia 'rasmi' siyo lazima isiwe historia sahihi kwani rasmi yaweza kuwa ni historia sahihi lakini haijakamilika. Mtu akisema kuwa alipotoka Ubungo kwenda Kariakoo alipata maeneo ya Urafiki, Manzese na Magomeni halafu akaenda zake hadi Kariakoo anaweza kuwa ameelezea kitu sahihi kabisa na mtu wa kumwelewa atakuwa amemwelewa. Lakini akisema kuwa ndio ametaja sehemu zote alizopitia kwa hakiki siyo kamili kwani kuna maeneo mengine ambayo ameyaruka na hajatuelezea kama wakati anafanya hivyo alichepukia pembeni. Lakini kwamba ametuambia njia aliyoipitia kutoka Ubungo basi kwa kiasi kikubwa tutamwelewa.
Historia ambayo wengi wetu tumejifunza imetaja watu wengi sana na kinyume na unavyodai hakuna kitabu chochota kinachotumika katika shule za Tanzania (iwe msingi, sekondari au vyuo vikuu) ambayo inatumia kitabu 'rasmi' ambacho kinaelezea historia kuwa ya kupigania uhuru ilianzia na Nyerere mwaka 1954. HAKUNA KITABU HICHO.
Sasa uzuri wa historia ni kuwa ni somo ambalo linaweza kuongezewa taarifa zaidi ili kulifanya kuwa kamili zaidi na kuwasaidia watu kujua zaidi na zaidi. Nilipoagiza kitabu chako nilitaarajia kusoma historia yetu ya wazee wetu na mchango wa wale ambao walikuwa wamesahauliwa. Nilipokisoma taratibu nilianza kuona pattern ya ajabu ukitokea.
a. Kila mwenye jina la Kiislamu ulimuita Muislamu bila ya kujali kama alikuwa anaamini yale yale au hata kama alikuwa anashika dini. Wengine ambao unawataja kuwa ni "waislamu" kwa kweli kabisa walikuwa ni wenye imani za jadi zilichanganywa na Uislamu ndani yake na hata wengine wanaweza kabisa kuwa walikuwa ni washirikina! Lakini hili kwako si hoja kwani hoja kwako ilikuwa ni 'majina ya kiislamu".
b. Baada ya muda 'Waislamu' wakawa ni wale tu waliokuwa kwenye jumuiya fulani fulani watu wenye majina ya Kiislamu lakini hawakuwa kwenye jumuiya hiyo hawa ukaanza kuwapa makundi mengine lakini ukaanza kuwatofautisha kwa kuwataja kwa mahali wanakotoka.
c. Unapofika mwaka 1963 unaanza kuwagawa "Waislamu" siyo kwa imani zao au la bali kwa kuangalia waliokuwa ndani ya TANU na wale waliokuwa nje ya TANU. Waliokuwa ndani ya TANU wakaanza kuangaliwa kwa shuku na ilipofika wakati wa kuvunjwa EAMWS Waislamu wakawa ni wale tu waliohusiana na EAMWS lakini wale waliobakia ndani ya TANU na wakaunda BAKWATA hawakuwa WAislamu japo HAKUNA USHAHIDI hata mmoja kuwa waliopiga kura kule Iringa kulikuwepo na Wakristu, Maaskofu au Wachungaji. Kama kigezo chako cha kwanza cha "majina" kuwa ndio Uislamu ingetosha kabisa kufanya BAKWATA ni halali kwani wote walioanzisha walikuwa ni wenye majina ya Kiislamu!
d. Lakini kwa vile lengo lako lilikuwa kuandika habari za "Waislamu" ambao walikuwa wanakubaliana na wazee wako au ambao waliamini wameonewa basi ikabidi uhakikishe kabisa kuwa huandiki habari za Watu wengine ambao hawakuwa Waislamu japo michango yao labda ililinga na wengine hata ilizidi ya wale uliowaita 'wazee wako'. Lakini hukufanya hivi tu. Ukaamua pia kuwafuta Waislamu wengine wote ambao walikuwa hawakubaliana na wazee wako na kuwaweka kwenye footnotes za Kitabu au mwisho wa kitabu.
Sasa kumbe wakati unawatuhumu wengine kuwa wanafundisha historia "rasmi" ambayo imepotosha watu walitarajia kuwa na wewe ungeendika a more comprehensive history of Tanzania's early days. La hasha. Na wewe ukaenda kuandika historia yako 'rasmi' ambayo haikuwa na lengo jingine lolote bali kuonesha ukuu wa Waislamu katika harakati za kupigania uhuru na kuonesha kuwa wao ndio walitaka kuwa huru zaidi kuliko jamii nyingine. Kumbuka ukajikuta unatukuza watu fulani fulani tu na siyo ukweli wa historia. Wakati unamtuhumu Nyerere kupindisha historia kuwa alijipendelea na wewe mwenyewe ukafanya kile kile cha kupindisha historia na kuwapendelea Wazee wako. Wakati unamlaumu Nyerere kuandika historia ambayo imewaweka watu wengine pembeni - japo hakuna ushahidi wa Nyerere kuhusika kuandika historia - wewe mwenyewe ukaandika historia ukiwaacha watu wengine pembeni.
Kama vile wale wengine unadai walidai kuwa historia yao ilikuwa rasmi lakini haijakamilika wewe mwenyewe unadai sasa historia hii ya kwako ni 'kweli tupu' wakati nayo haijakamilika. Kubali yafuatayo kwanza:
a. HIstoria yako si kamili na haiwezi kuwa historia rasmi
b. Historia yako imeandikwa kwa ajili ya kuenzi wazee wako lakini siyo kwa ajili ya kuonesha ukweli wa historia
c. Historia yako imetokana zaidi na hisia kuliko historia.
d. Historia yako imelengwa katika kupotosha mchango wa Wazee wetu ili kuonesha upande mmoja wa wazee wetu (Waislamu wa Gerezani) walikuwa ndio magwiji wa uhuru wa Tanganyika na watu wengine wote wakiwa ni watu walionufaika na hao wazee wa Gerezani.
e. Historia yako ina lengo la kukana nafasi ya pekee (unique role) ya Nyerere kama Baba wa Taifa (hili jina hakuanza kuitwa baada ya kustaafu, upo ushahidi wa Kambona kumuita Nyerere "baba wa Taifa" katikati ya 1960s). Wazee wa Dar-es-Salaam walitambua nafasi hiyo ya Nyerere, waliiheshimu na waliishi naye katika uhusiano wa kuamianiana (patnership of trust).
f. HIstoria yako haitaki kukubali ukweli kwamba Nyerere kama Rais alikuwa na wajibu kwa Watanganyika wote na asingeweza katika dhamira safi kutoa upendeleo wa pekee kwa wazee fulani kana kwamba wazee wengine hawakushiriki. Kikundi cha wazee wanaomlalamikia Nyerere leo hii ni wale ambao walitarajia kuwa wangepata nafasi fulani au upendeleo fulani (Nyerere aliligusia hili katika hotuba yake ile ya 1962).
Kubali haya kwanza ili tuweze kusonga mbele.