Unapokishika kitabu kimoja mkononi, haijalishi kina kurasa ngapi, tambua kwamba umeshika kazi iliyofanyiwa utafiti wa muda mrefu. Hakuna mtu anaandika kitabu bila utafiti, hivyo unaposoma kitabu kimoja ni sawa utasoma utafiti wa mtaalam fulani mwenye fani fulani. Ni sawa uko darasani unamsikiliza mhadhiri wa chuo kikuu akikupa madini kuhusu mada au somo fulani. Maana yake ni kwamba ukiweza kumudu kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi ni vitabu 12 kwa mwaka, ni sawasawa na kukaa darasani na kuwasikiliza wataalam 12 wakikupa nondo mmoja baada ya mwingine. Ukijenga hiyo tabia ya kusoma kila mwezi kwa miaka mitano, maana yake utakuwa umekutana na kuwasikiliza wataalamu sitini (60) ndani ya miaka mitano. Ukiamua kwamba hii ndio iwe tabia yako maisha yako yote, ina maana katika maisha yako umezungukwa na wataalam wa fani zote, utakuwa ni mtu mwenye maudhui na maarifa mengi. Mtu yeyote ambaye hana tabia ya kusoma vitabu ni sawa sawa na mtu 'aliyeacha kuishi', ni sawa na mtu aliyekufa - lakini anatembea.
Baadhi ya faida azipatazo mtu mwenye tabia ya usomaji wa vitabu;
- Kujenga uwezo wa kufikiri kwa kina (Critical thinking), hivyo hufanya maamuzi bila kukurupuka, maamuzi yaliyofanyiwa tafakuri jadidi.
- Kujenga maudhui (Content) ya kutosha, hata kwenye mazungumzo au mabishano, mtu mwenye tabia ya kusoma vitabu huzungumza kwa staha, kwa hoja, kwa sauti yenye utulivu, bila kupayuka. Kukwepa hoja ya msingi iliyopo mezani, kumshambulia mtoa hoja badala ya kutoa hoja, kupiga makelele ni dalili za watu wasio na tabia ya usomaji vitabu. Ukikaa kwenye mazungumzo au mabishano unaweza kuona kwa uwazi kabisa nani ni msomaji wa vitabu na nani si msomaji.
- Huboresha afya ya akili, kuimarisha kumbukumbu, ubunifu na ufanisi katika shughuli za kila siku. Hata viongozi wengi wazuri ni wasomaji wazuri wa vitabu.
- Ni namna nzuri ya kutumia muda wako vizuri, kujiliwaza, kujifariji, kujitia moyo, kuepuka msongo wa mawazo, na kukuepusha kutumia muda vibaya na kujihusisha na tabia mbaya kama vile ulevi, uvivu, uzinzi, sigara ina maana utaweza kutumia muda wako vizuri na hivyo kuboresha maisha yako.
Watanzania walio wengi, hata baadhi ya viongozi hawana tabia ya usomaji wa vitabu na matokeo yake wengi wanatia huruma, hawana maudhui, hawana hoja, hawana uwezo wa kuunga ama kupinga hoja fulani, wanatumia nguvu nyingi, makelele, mashambulizi binafsi, ubabe badala ya kujenga hoja. Yote haya ni matokeo ya ukosefu wa tabia ya kusoma vitabu.
EWE NDUGU ANZA TABIA YA USOMAJI WA VITABU SASA