Naomba nizungumze yafuatayo. Nilikuwa kwenye kikosi cha kikapu cha kanda ya Mashariki kwenye michezo a UMISETA mwaka 1991/1992. Edibily Lunyamila alikuwa kwenye kikosi cha mpira wa miguu cha kanda ya Magharibi. Hii ndio ilikuwa mara kwanza kumuona. Tuilkuwa tunacheza michezo yetu (kikapu) nje ya uwanja wa Amaan. Baada ya mechi zetu, ukisikia kanda ya Magharibi wanacheza, tulikuwa lazima tuende kumuangalia. Kwa jinsi alivyokuwa machachari na jinsi alivyokuwa anacheza, sikuwa na shaka kuwa atakuwa miongoni wa wachezaji bora kabisa kutokea Tanzania. Haikupita muda tuliporudi Dar es salaam, nikamuona uwanja wa zamani wa Taifa anaingia na kwenda jukwaa la Yanga (baada ya kusajiliwa).
Mimi ni mpenzi wa kutupwa wa Simba SC. Nikajua tutapata matatizo sana nae tukikutana. Pamoja na ushabiki wangu wa Simba SC, hakuna mchezaji wa Yanga aliyekuwa ananikuna kama yeye. Nilikuwa tumbo joto wakati wa mechi za watani wa jadi kwa sababu yake. Mchuano na purukushani zake na Kasongo Athumani zilikuwa kabambe. Kasongo ilibidi atumie ubabe na nguvu nyingi kumzuia. Alikuwa na kasi, uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, na chenga. Angeweza kabisa kucheza mpira wa kulipwa zaidi ya kuchezea Yanga na baadae Simba. Ningependa sana nikutane nae siku moja nipate fursa ya kuongea nae.