Katika kuhakikisha ulinzi na elimu vinatolewa kwa wananchi, Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Wanamaji nchini kimeendelea kuyafikia makundi mbalimbali ya watumiaji wa vyombo vya majini ambapo leo kimetoa elimu ya ukatili wa kijinsia na mbinu za namna bora za kujiokoa pindi inapotokea ajali katika vyombo hivyo.
Akitoa elimu hiyo leo Agosti 6,2024, katika Boti ya Kilimanjaro, Mkuu wa Dawati la jinsia na Watoto kutoka kikosi cha wanamaji, Mkaguzi wa Polisi Inspekta Avelina Temba amewaomba wananchi hao kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio na maadili katika jamii.
Soma Pia: Polisi yahimiza Wananchi wote kuwa waangalizi wa Watoto
Inspekta Avelina ameongeza kuwa wazazi wanapaswa kufuatilia kundi la watoto ambalo tafiti zake zimeonyesha kuwa kundi hilo liko katika hatari ya ukatili ambapo amewataka kuwasikiliza watoto ili kuzitambua changamoto wanazopitia.
Naye Mkaguzi wa Polisi, Inspekta Anna Ugomba amebainisha kuwa lipo kundi la akina baba ambao wanafanyiwa ukatili na wake zao ikiwemo kunyimwa unyumba ambapo amewataka kutoa taarifa hizo kwa Jeshi la Polisi ili wahusika wa vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.