SIKU 100 ZA MHE SAMIA RAIS WA TANZANIA.
Na Elius Ndabila
0768239284
Mara nyingi duniani Viongozi wa nchi huanza kupimwa utumishi wao kwa kipindindi Cha siku mia moja. Lakini siyo sheria wala kanuni ni utaratibu tu ambao watu wanadhani unaweza kuwasaidia kujua uwezo wa kiongozi wao kuelekea katika kutimiza majukumu yao makubwa aliyopewa.
Leo Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan anatimiza siku 100 tangu apokee kijiti hiki kwa mjibu wa katiba baada ya kifo Cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt Magufuli aliyefikwa na umauti kwa ugonjwa wa Umeme wa Moyo. Makala hii itakuangazia kinagaubaga juu ya uongozi wa awamu ya sita wa Mhe Samia Suluhu HASSAN baada ya Siku zake 100 tangu kuapishwa kwake.
Kwanza Ifahamike kuwa viongozi waliopita tunaweza kuwatazama katika jumla ya miaka yao waliyokaa madarakani. Kwa mfano maendeleo ya awamu ya tano ya hayati Dkt Magufuli tunayapima kwa miaka mitano na miezi miatano ya utawala wake. Na Maendeleo ya awamu ya nne tunayapima kwa miaka kumi ya Dkt Jakaya Kikwete hali kadharika kwa awamu zingine zilizopita. Leo sihitaji kuelezea Maendeleo ambayo kama Taifa tumeyapata kwa awamu zilizopita, leo ninataka kuzungumza kinagaubaga mafanikio ya Mhe Samia ya siku 100 za uongozi wake.
Katika kuzungumzia siku mia moja za Mama Samia, Rais wa Tanzania, leo ninataka nigusie kwa undani juu ya uongozi wake wa siku 100 tangu alipoapishwa tr. 19/3/2021 baada ya kufariki kwa Rais wa awamu ya tano Dkt Magufuli na wakati huo Mhe Samia akihudumu kama makamu wa Rais.
Kwa siku hizi mia Moja tunaweza kumtazama Rais SAMIA SULUHU HASSAN kama kiongozi ambaye amewatuliza mioyo Watanzania ambao baada ya kufariki kwa Magufuli hawakujua hatima ya nchi. Mhe Samia kwa siku mia Moja amekuwa mwarobaini wa majawabu ya Watanzania ambao walidhani nchi haitaenda. Lakini kwa ujumla Rais Samia kwa siku hizi mia Moja hakuna mashaka kuwa amekuwa tiba ya majeraha na amekuwa kiungo mhimu kwa Watanzania wote bila kujali Dini, rangi, vyama au ukabila. Kauli yake ya "KAZI IENDELEE" ni kibwagizo tosha kuonyesha utawala wa haki.
Kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ilikuwa ni ndoto yake tangu siku ya mwanzo alipoapishwa. Rais Samia Suluhu aliahidi kuwa serikali yake itasimamia kwa umakini suala la uhusiano baina ya Tanzania na nchi jirani na kuwa chachu ya kujenga jamii bora baina ya mataifa hayo.
"Kwa jirani zetu na marafiki zetu niwahakikishie tutaulipa wema mliotuonesha kwa kuimarisha na kushamirisha uhusiano wetu nanyi," alisema Rais Suluhu katika hotuba yake ya kumuaga Hayati Magufuli mkoani Dodoma.
Pia ujumbe huo ulileta majibu ya swali la mustakabali wa Kidiplomasia wa Tanzania na Jumuiya ya kimataifa. Kwamba Rais amethibitisha kuwa yupo tayari kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwaita "Marafiki zetu" ikiwa na maana ya kuwakaribisha katika mashauriano ya Kidiplomasia na kuwahakikishia ushirikiano madhubuti. Kwa siku mia Moja ndani ya Ikulu Mhe Samia amethibitisha hilo kwa mifano kedekede.
Kwanza ameendelea Kukuza na kuendeleza Diplomasia na nchi zingine za ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa ujumla.Rais Samia kwa kipindi hiki kifupi ameendelea kujenga mahusiano ya kikanda na Kimataifa kwa kuwa anaamini kuwa maendeleo ya nchi ni ya kutegemeana na kushirikiana. Akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza alisistiza kuwa ataendelea kudumisha mahusiano ya Tanzanzania na nchi zingine yaliyokuwepo tangu mwanzo na kuendelea kuimarisha Yale ambayo yalikuwa yameanza kulegalega. Kwa kipindi hiki Cha siku mia moja Pamoja na kutembelewa na wageni mbalimbali toka nje ya nchi Mbali Mbali Duniani lakini pia hata yeye kwa kipindi hiki kifupi ameshafika nchi za Uganda na Kenya. Kabla ya utawala wake ikumbukwe kuwa ilizuka Vita ya maneno kati ya Kenya na Tanzania ambayo ilisababisha hata mdororo wa biashara wa nchi hizi mbili. Mhe Samia na Rais wa Kenya Mhe Uhuru Kenyatta walikaa na kulitatua tatizo hilo ambalo lilikuwa linatia dosari katika mahusiano ya nchi hizi mbili. Baada ya viongozi hawa kukaa walifanikiwa kutatua changamoto hiyo na kujenga mazingira mazuri ya Diplomasia ya kiuchumi Kati ya Tanzania na Kenya. Tukumbuke kuwa uchumi wa sasa unajengwa zaidi na diplomasia ya uchumi ambayo inajengwa na mahusiano ya nchi na nchi. Nchi zote ambazo uchumi wake unakua na kuimalika basi ujue kuwa mahusiano yake na mataifa uko vizuri. Dunia ya sasa mahusiano ni Uchumi, hakuna mahusiano ya hadithi tu. Mahusiano ya nchi huimalishwa na fursa, kama hakuna fursa hakuna mahusiano. Mhe Rais Samia kwa siku mia Moja ameonyesha ni muumini wa Diplomasia na ndiyo maana kazi ya kwanza ilikuwa ni kumteua Mwanadipolomasia mahili Balozi Mulamula kuwa Waziri wa Mambo ya nje.
Mhe Samia awali alizungumza kuwa Tanzania haiwezi kujifungia na kujenga miradi yake mikubwa pekee yake.Tuna miradi mikubwa, lazima wenzetu watusaidie kuijenga.Alisema hivyo akiamini nchi inaweza kuingia makubaliano na taasisi zingine zenye mikopo ya riba nafuu ili kuweza kusaidia kujenga miradiikuwa hasa Treni ya Umeme alimaarufu (SGRA) na Mradi wa kufua Umeme wa Nyerere.Mwanadipolomasia nguli Mlamula alimuona kama tiba tosha kuhakikisha zile tofauti ndogo ndogo zilizokuwa zinapandkizwa juu ya Tanzania zinamalizwa mara Moja, na tumeona sasa Tanzania huko nje haiandikwi vibaya kama ilivyowahi kuwa huko nyuma. Hivyo siku mia Moja za Mhe Rais Samia zimeandelea kujenga mahusiano mazuri na mataifa mengine huko nje.
Vita dhidi ya Corona katika siku mia Moja za Mhe Samia imekuwa ni vita ya kitaifa na ya kila mmoja. Sasa si aibu tena kupambana na huu ugonjwa.Mhe Samia ameonyesha njia Mpya ya kupambana na Vita dhidi ya Corona kwa kuanza kuunda tume ya kitaifa iliyokuja na mapendekezo ya nini nchi ifanye. Mhe Samia kwa siku zake mia moja uongozi wake ameonyesha kuwa Corona ipo na nilazima Tanzania nayo kama nchi ianze kupambana ugonjwa huu kama mataifa mengine. Mhe Rais alisema kuwa Tanzania si kisiwa kuwa sisi tupo salama kama Watu huko kwingine wanafariki.Ili kuonyesha msistizo katika hilo aliamua kuunda tume ambayo alisema itaishauri serikali nini Cha kufanya katika mapambano hayo. Ikumbukwe kuwa ugomvi mkubwa wa Tanzania na baadhi ya mataifa na kuanza kulegalega kwenye mahusiano na Baadhi ya nchi ilikuwa ni namna Tanzania inavyolichukulia suala la covid 19. Tume iliyoundwa ilikuja na mapendekezo karibia 20 ambapo Moja wapo ilikuwa ni Tanzania kuchukua hatua za kujikinga kama zilivyo nchi nyingine. Baada ya tume Rais Samia amesistiza kuchukua hatua zote ambazo wenzetu wanazichukua hususani uvaiji wa Barakoa, kunawan.k. Mapambano hayo yameiweka Tanzania katika sura mpya katika medani za Kimataifa kwani mwanzo Tanzania ilitafsiriwa kama wakaidi juu ya mapambano haya. Haya ni mafanikio ya awamu ya sita.
Ukusanyaji kodi usiozingatia sheria na taratibu za nchi umepigwa marufuku na kukomeshwa na Mhe Samia. Alisistiza anataka kuona watu wanalipa Kodi kwa kuwa kodi ndiyo ijini ya kuiendesha nchi, lakini alisema ni lazima kodi ilipwe kwa kuzingatia sheria za nchi zilizopo na si kutumia task force ambayo matokeo yake Biashara zilipungua. Katika siku 100 za uongozi wake amedhibiti ukusanyaji holela wa kodi ambao kuna Baadhi ya maofisa walianza kutumia task force na kuwafanya wafanyabiashara wengine kufunga biashara zao au kuhamishia Biashara zao nje ya nchi. Ikumbukwe kuwa kulipa kodi ni takwa la kisheria na kila mfanya biashara anapaswa kulipa kodi. Lakini kukusanya kodi kinyume na taratibu hasa kwa kutumia nguvu na vyombo vingine vya dola ni kuhatarisha usalama wa biashara na kupunguza makusanyo ya serikali pale Biashara zinapofungwa. Mama Samia baada ya kuapishwa tu alisema kazi ya kwanza ni kuhakikisha TRA na vyombo vingine vinavyokusanya kodi kukusanya kwa mjibu wa sheria. Alikataza mamlaka kufungu akaunti za Wafanyabiashara kibabe na zaidi aliwaasa wote waliokuwa wamefanyiwa hivyo kufunguliwa akaunti zao. Alienda mbali kwa kuitaka Wizara inayohusika na uwekezaji kutokuwa kikwazo. Kwa siku hizi 100 tumeshuhudia Wawekezaji wengi wakianza kurudi baada ya kuhakishiwa usalama wa biashara zao na mitaji yao. Wafanyabiashara waliokuwa wamekimbilia nchi za jirani kwa unyanyasaji wa sheria za TRA wameanza kurejea. Hata Waziri wake wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba alisema watu wote ambao akaunti zao za benki zilikuwa zimefungwa zifunguliwe ili waendelee na biashara zao. Katika siku 100 amejaribu kufanya mabadiliko katika sekta hiyo ya TRA kwa kuwaondoa Baadhi ya maofisa wakuu ambao alidhani ni kikwazo katika sekta hii mhimu.
Katika uongozi wa Siku mia Moja wa Rais Samia amefanikiwa kukutana na makundi mahususi katika Taifa. Alianza kwa kukutana na Wazee wa Tanzania pale Dar er salaam, baadae akakutana na kundi la Wanawake pale na Dodoma na hivi karibuni amekutana na uwakilishi wa kundi la Vijana wa nchi hii pale Mkoani Mwanza. Makundi haya ni mhimu na mahususi katika Ujenzi wa Taifa. Ni makundi yanayoweza kuelezea changamoto zao na kama kiongozi ukajua namna ya kuzitatua. Na kwa historia ya nchi yetu ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa nchi kukutana na makundi haya matatu ndani ya siku chache na kuwasikiliza. Tulishazoea kuona viongozi wengi wakionana na Wazee, lakini Mhe Samia amekuja na ladha tofauti.
Akiwa Mwanza alirusha kombola kwa Vijana ambao badala ya kutafuta changamoto za Vijana na kupendekeza suluhu ya matatizo ya vijana lakini wao wamegeuka kuwa wapiga debe wa Wanasiasa kitu ambacho alisema hapendi kukiona. Alikazia kwa kusema hata sera ya Vijana ambayo imeasisiwa tangu mwaka 2007 haijawa na maboresho yanayoakisi mabadiliko ambayo nchi na Dunia imekuwa ikiyapitia. Hotuba ya Mhe Rais ilikuwa inaonyesha kuwalenga Wizara ambayo imepewa jukumu la kuwalea Vijana kama wamelala. Akiwa huko katika Mkutano huo ndipo alipotumia nafasi hiyo kumtumbua DC na Mkurugenzi wa Morogoro ambao alisema wameshindwa kushughulikia matatizo ya Vijana.
Uhuru wa vyombo vya habari, baada ya kuapishwa tu Mhe Rais aliagiza online tv zote ambazo zilikuwa zimefungiwa kufunguliwa. Mhe Rais kwa mkutadha wa kawaida ni muumini wa haki, lakini aliwataka wanahabari hao kuzingatia weredi wao katika kuhabarisha umma. Siku mia Moja wanahabari wanamuona Mhe Rais kama rafiki wao kwani kufungua online TV zote kumeongeza wigo wa ajira kwa watu ambao ajira zao zilipotea baada ya vyombo vyao kufungiwa.Siku mia Moja za Mhe Samia zimeandelea kuimarisha uhuru wa habari hasa kwa kitendo chake Cha kufungulia online tv zote ambazo ni zaidi ya 440 zilizosajiliwa. Hivyo siku 100 za Mhe Rais zimeongeza wigo wa habari na ukombozi wa vyombo hivi.
Suala la Uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa kwa vyama vyote vya siasa ambalo ni kwa mjibu wa sheria zilizoanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini na Katiba ya nchi. Mhe Samia baada ya kuapishwa amefungua milango kwa wanasiasa kufanya kazi zao za kisiasa na pia ameruhusu majadiliano Kama kuna mahali kuna mikanganyiko na kuhitaji majadiliano ya pamoja. Pia amefungua milango kwa Wanasiasa kwani amesema atakutana na viongozi wa vyama vyote ili kuedelea kudumisha demokrasia hapa nchini. Lengo la Mhe Rais ni kuona fursa sawa kwa vyama vya siasa huku siasa zikiwa safi na za kujenga Umoja wa Kitaifa na si siasa za kuligawa Taifa. Hayati Magufuli aliamua kusimamisha shughuli za kisiasa kwa maelezo kuwa zinapoteza muda mwingi wa kufanya kazi za Maendeleo ya nchi na zinachochea uhasama. Yeye aliamini kuwa siasa zinapoteza muda wa kufanya shughuli za Ujenzi wa Taifa. Lakini Mwanamama Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Tanzania baada ya kushika hatamu ya uongozi tumeanza kuona viongozi wa vyama vya siasa wakitembea kote nchini kufanya siasa.
Suala la utawala bora Mhe Samia amekuwa kielelezo kwa siku mia Moja. Amesistiza wasaidizi wake kufanya kazi kwa kufuata sheria na si vinginevyo, na kwa siku hizi mia Moja hakuna malalamiko ya utawala au maigizo yasiyozingatia sheria. Sheria zinaongoza kufanya maamzi na mabavu. Na kwa msistizo alitoa maagizo kuwa sheria zitumike kwa 70% na utu, ubinadamu (Utashi) utumike 30%. Hivyo Mhe Rais ndani ya siku hizi mia moja ameweka misingi imara ya utawala bora ambayo ndiyo nguzo kubwa ya maendeleo na ustawi wa maisha ya wananchi.
Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha kuheshimu na kusisitiza utawala wa sheria ambayo unastawisha upatikanaji wa haki na usawa, amani na utulivu lakini pia kujenga mshikamano na utengamano wa Kitaifa.
Kauli zake nyingi zinaleta tabasamu kwa Watanzania wengi ambao baada ya kifo Cha Rais Magufuli walikuwa hawajui hatima ya Tanzania na hasa ukizingatia nchi yetu haikuwahi kushuhudia Rais kufariki akiwa madarakani.Mhe Samia ameleta matumaini mapya na anabeba dhima nzima ya mwanamke anayetaka kuona familia yake inafurahia muda wote. Falsafa ya Mhe Samia ni mwenye sauti ya upole lakini sauti yenye maamzi magumu lakini yanayozingatia sheria. Ninaamini wale Watafiti ambao Prof Lipumba alikuwa akiwatumia kwenye kampeni zake kuwa Watanzania hawana furaha na kuwa Watanzania wanazeeka haraka kwa kuwa hawana furaha, basi kwa kipindi hiki Cha Mama Samia Prof LIPUMBA akipewa fursa ya kuja na utafiti wake atasema Watanzania wengi wameongeza furaha hasa baada ya kupata matumaini kuwa bado Taifa lipo salama, na utawala bora unaheshimika na kuzingatiwa.
Ameongeza kasi, ubunifu na maarifa katik uwajibikaji na kuendelea kuwachukulia hatua kali wanaovunja sheria. Mhe Samia amejipambanua katika kuhakikisha sheria haiwi kikwazo Cha watu kulijenga Taifa. Na amekuwa anasistiza Kama sheria ni kikwazo basi zifanyiwe marekebisho. Katika siku mia Moja za uongozi wake amefanya mabadiliko makubwa kwenye sekta mbalimbali katika kuongeza kasi ya kuchapa kazi.
Kuendelea kusimamia miradi ya kimkakati ambayo ilianzishwa na mtangulizi wake Hayati Magufuli yeye Mhe Samia akiwa makamu wa Rais. Mhe Samia alisema ataendelea kuijenga miradi yote ya kimkakati ambayo ilisimamiwa na mtangulizi wake na ameendelea kuisimamia kwa vitendo. Ujenzi wa SGR unaendelea na Mradi wa kufua Umeme wa Nyerere unaendelea kwa kasi kubwa. Hii imemjengea heshima kubwa Mhe Rais ambaye amekuwa Shujaa dhidi ya Watu waliodhani ataiacha.
Moja ya miradi hiyo mikubwa na ya kimkakati ni pamoja na kuendelea kujenga Bwawa la umeme la Nyerere ambalo litazalisha Megawatt 2115, kuendelea kujenga treni ya Umeme kutoka Dar es salaam hadi mwanza(SGR) na bomba la kusafishia mafuta kutoka Tanga hadi Hoima nchi Uganda. Hii ni sehemu tu ya miradi ya kimkakati.
Rais Samia kwa siku hizi mia Moja pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia kwenye teuzi zake, lakini amejitahidi kwa Kiwango Kikubwa kuwakumbuka Vijana. Vijana wengi wameendelea kuaminiwa katika nafasi nyeti za kiutumishi.
Hata hivyo haki na wajibu vimepewa kipao mbele katika uongozi wake. Hataki kuona watu wanaonewa au kudhulumiwa, anataka kuona mkondo wa sheria unafuatwa na hekima ikipewa nafasi.
Kwa mara ya kwanza bajeti ya serikali imepitishwa kwa zaidi ya asilimia 94 tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi. Bajeti hii ambayo inamtazama zaidi mtu wa chini haikupata Kura hata Moja ya hapana. Kura 94% waliunga mkono na 6% walisema hawapingi bajeti Wala hawakatai. Walikuwa hawafungamani na upande wowote. Na ni kwa mara ya kwanza kila Jimbo litapata bilion Moja ya ukarabati wa barabara mara baada ya kuahirishwa. Hii haijawahi kutokea.
Yapo Mambo mengi ambayo Mhe Samia Rais wa Tanzania ameonyesha umahiri wa kuyashughulikia kwa kipindi hiki Cha siku mia Moja. Rais amekuwa salaam ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania "KAZI IENDELEE". Salaam inayoleta matumaini makubwa na kujenga mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Wajibu wa Watanzania ni kuendelea kumuombea Mhe Rais ili yale aliyokusudia aweze kuyafanya, lakini wale waliopewa nafasi ya kumsaidia basi wamsaidie kwa dhati ili asikwamishwe wala kucheleweshwa. Mhe Rais na WASAIDIZI wake Wana kazi kubwa kuhakikisha Uchumi ulioshuka kutokana na janga la ugonjwa wa COVID 19 unaimalika tena. Lakini kubwa ni kuendelea kufanya siasa zenye matokeo ya kuibua changamoto na kupata suluhisho la hizo changamoto.
Nchi ijiepushe na siasa zinazo weza kurudisha Maendeleo ya nchi nyuma kwa kutengeneza migogoro isiyo na maana tena ya kutengenezewa. Lakini namna Mhe Rais anavyoteua wasaidizi wake unaonyesha dhahiri anaenda kukomesha siasa za kutengeneza migogoro. Kwani uteuzi wake umekuwa unaangalia zaidi uwezo wa mtu na si ukada wa vyama.