Wamekabwa koo vita nzima sasa wameanza kuua wenzao kwa hasira ya kushindwa🤣🤣
- Tunachokijua
- Mnamo mwezi Juni Israel ilianzisha mashambulizi katika taifa la Iran na kuharibu baadhi ya mali zake huko maofisa kadhaa wa juu wa kijeshi wakiuawa. Mara baada ya shambulio hilo la kushtukiza Iran nayo pia imeendelea kujibu mashambulizi kuelekea Israel na kupelekea kuendelea kwa mzozo huo.
Madai
Kumekuwapo na picha inayomuonesha mwanaume mmoja akiwa amenyongwa kwa kuning’inizwa na kuelezwa kuwa tukio hilo linatekelezwa na Iran kwa watu wanoisifia Israel kwenye kipindi hiki cha vita.
Uhalisia wa taarifa hiyo pamoja na picha
JamiiCheck imefuatilia taarifa hiyo na kubaini kuwa si ya kweli aidha picha inayoambatana na taarifa hiyo si ya mwaka 2025.
Ufuatiliaji kwa njia ya Google reverse image search umebaini kuwa Picha inayomuonesha mwanaume akinyongwa ni ya Disemba 12, 2024. Anayeonekana akinyongwa ni Majidreza Rahnavard, ambapo tukio hilo lilitekelezwa katika mji wa Mashhad nchini Iran.
Majidreza alinyongwa hadharani siku 23 tu baada ya kukamatwa huku umri wake ukiwa ni miaka 23 tu. Iran ilisema kuwa huyo ni mtu wa pili kunyongwa hadharani. Mahakama ilimhukumu kwa kosa la "uadui dhidi ya Mungu" baada ya kubaini kuwa aliwachoma kisu hadi kufa wanachama wawili wa Kikosi cha Kujitolea cha Basij.
Picha ya MajidrezaAidha hakuna taarifa yoyote hadi sasa inayothibitisha kuwa kuna vitendo vya unyongwaji wa watu wanaoiunga mkono Israel unaondelea huko Iran.
Shirika la kimataifa la Amnesty lilihusianisha tukio hilo na maandamano yaliyokuwa yakiendelea nchini humo kuipinga serikali ya Iran. Diana Eltahawy, Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International kwa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, alisema:
“Kunyongwa hadharani kwa Majidreza Rahnavard leo umefichua sura halisi ya mfumo wa mahakama wa Iran: chombo cha ukandamizaji kinachotuma watu kunyongwa ili kueneza hofu na kulipiza kisasi dhidi ya waandamanaji wanaothubutu kupinga hali iliyopo. Kunyongwa kwa Majidreza Rahnavard kwa njia isiyo ya haki, chini ya wiki mbili baada ya kusikilizwa kwa kesi yake pekee, kunaonesha wazi jinsi mamlaka za Iran zinavyokandamiza haki ya kuishi na kupuuza kabisa hata muonekano wa mchakato wa haki wa kweli.”