Kauli alizowahi kuzitoa Mh. Jaji Mustapher Mohamed Siyani kusisitiza haki na weledi ili Mahakama zijijengee imani kwa umma mpana.
Jumatatu, 31 Agosti 2020
MASHAURI YA UCHAGUZI YASIATHIRI IMANI YA WANANCHI KWA MAHAKAMA – JAJI SIYANI
Na Innocent Kansha – Mahakama Dodoma.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani amewataka Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama ya Tanzania kusikiliza mashauri uchaguzi kwa kuzingatia weledi na kutenda haki ili wasiathiri Imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.
Akifungua awamu ya tatu ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa Mashauri ya uchanguzi kwa Waheshimiwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi Tanzania, Jaji Siyani amewataka Mahakimu hao wafawidhi kusimamia masjala kwa karibu zaidi, ili mashauri yanayofunguliwa yaweze kushughulikiwa ndani ya muda stahiki.
Jaji Mfawidhi aliwakumbusha Mahakimu hao kutilia mkazo matumizi ya Teknologia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili mashauri yanayofunguliwa kwa njia ya mtandao (E-Filing) yaweze kusikilizwa na kumalizika kwa wakati.
“Mafunzo haya ni muhimu kwenu binafsi na Mahakama kama taasisi, umuhimu wake hauelezeki kwa maneno mepesi, kwa wale ambao wamewahi kusikiliza mashauri ya uchaguzi wanaelewa nini ninachozungumzia hapa”, alisistiza Jaji Siyani.
Alisema, katika kuyashughulikia mashauri yatokanayo na uchaguzi, suala la muda ni jambo la muhimu kwani viongozi wa ngazi za juu wa Mahakama pia wameelekeza mashauri hayo kutodumu Mahakamani kwa zaidi ya miezi minne tu na si vinginevyo, hivyo amewataka Mahakimu hao kujiandaa kutekeleza majukumu maelekezo hayo muhimu.
Jaji Mfawidhi alisema Mahakama haiwezi kujitenga na mchakato wa kidemokrasia wa nchi yetu,hivyo ushiriki wa muhimili uko katika hatua zote ikiwemo kabla ya kuanza kwa uchaguzi na hata baada ya matokeo kutangazwa. Aliongeza kuwa Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka dhahiri kuwa Mahakama ndicho chombo chenye kauli ya mwisho katika kutoa haki. Source :
MASHAURI YA UCHAGUZI YASIATHIRI IMANI YA WANANCHI KWA MAHAKAMA – JAJI SIYANI