- Musa aliacha maisha ya kitajiri na kifalme nyumbani kwa farao na kwenda kuishi pamoja na ndugu zake Waisraeli waliokuwa maskini na watumwa. Imeandikwa:
Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo; akihesabu ya kuwa kushutumiwa kwake Kristo ni utajiri mkuu kuliko hazina za Misri; kwa kuwa aliyatazamia hayo malipo. (Waebrania 11:24-26).
Yesu naye aliacha utukufu mkuu mbinguni. Imeandikwa:
Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. (Wafilipi 2:5-8).
- Musa alitumwa na Mungu kwenda kuwatoa Israeli kwenye nchi ya utumwa wa farao na watesi wake ili kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi. Yesu alitumwa na Mungu kuja kuwatoa wanadamu kwenye utumwa wa ibilisi (farao wa kiroho) ili kuwaingiza kwenye mbingu.
- Musa alikuwa ni mpatanishi kati ya wana wa Israeli na Mungu pale walipotenda dhambi. Maombi yake ndiyo yaliyoepusha mapigo kutoka kwa Mungu. Yesu ndiye mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu. Yeye huwaombea wale wanaomwamini ili hatimaye wasije kuingia jehanamu ya moto.
- Musa aliwakomboa wana wa Israeli kutoka kwenye utumwa wa Misri kupitia sadaka ya damu. Waisraeli waliambiwa wachinje mwanakondoo wa Pasaka na kupaka damu yake kwenye miimo ya milango ya nyumba zao. Kisha Biblia inasema:
Na ile damu itakuwa
ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. (Kutoka 12:13, 23)
Bwana Yesu naye aliwakomboa wanadamu wote kutoka kwenye utumwa wa shetani kupitia sadaka ya damu. Biblia inasema:
Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. (Waebrania 9:11-12).
- Musa aliwaagiza Waisraeli waokote mana iliyodondoka jangwani kila siku ili wapate kula na kuishi jangwani. Imeandikwa:
Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa … (Kutoka 16:21).
Kwa kuwa hayo yalikuwa ni ishara ya mambo yajayo, alipokuja Bwana wa uzima mwenyewe, Yesu Kristo, akawa ameleta kile halisi ambacho kilikuwa kinasubiriwa. Imeandikwa: Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima. (Yohana 6:31-33).
- Watu waliumwa na nyoka jangwani. Mungu akamwambia Musa atengeneze nyoka wa shaba. Amwinue juu ili mtu aliyeumwa na nyoka akitaka kupona, ainue macho yake na kumtazama yule nyoka wa shaba. Waliofanya hivyo walipona. Walioshindwa kufanya hivyo walikufa. Imeandikwa:
Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi. (Hesabu 21:9).
Yesu alipokuja naye kafanya yaleyale. Nyoka ni ishara ya ibilisi na mashetani wote. Kuumwa na nyoka ni ishara ya kuwa na dhambi. Kila mwenye dhambi anatakiwa kumtazama Yesu kwa imani, naye atapona mauti – yaani kutupwa jehanamu ya moto. Anayekataa kumtazama Yesu anakuwa amechagua kufa! Imeandikwa:
Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. (Yohana 3:14-15)
- Musa alikataliwa na watu wake. Walimwambia: Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. (Kutoka 2:14).
Kisha aliondoka na kwenda nchi ya Midiani. Huko alioa mke ambaye hakuwa Mwisraeli. (Tazama: Kut. 2:16-21). Lakini baada ya hapo alirudi tena Misri na kuwatoa Israeli utumwani.
Yesu naye alikataliwa na watu wake. Imeandikwa: Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. (Yohana 1:11). Ni jambo lililo wazi kuwa hadi sasa Wayahudi hawamtambui Yesu kama Masihi wao. Lakini kama ilivyokuwa kwa Musa, Bwana Yesu akatoka kwa hao walio wake akaja kwa Mataifa, yaani watu wengine wote wasio Wayahudi. Huko amejipatia na anaendelea kujipatia ‘bibi harusi’ – maana Kanisa la Yesu, kwa ujumla wake, linaitwa ni bibi harusi wa Bwana Yesu (Tazama 2 Wakorintho 11:2). Na tena imeandikwa: Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu. (Warumi 9:25).
Lakini kabla ya kuingia Kanaani (yaani dunia kufika mwisho), Bwana Yesu, kama Musa, atamrudia Israeli. Imeandikwa: Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. (Warumi 11:25-26).
- Musa aliteua watu kumi na mbili akawatuma Kanaani. Imeandikwa: Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila. (Kumbukumbu 1:23). Bwana Yesu naye aliteua mitume kumi na mbili akawatuma. Imeandikwa: Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri. (Marko 3:14).
- Musa aliteua watu sabini kwa ajili ya kusimama mbele za Bwana. Imeandikwa: Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. (Hesabu 11:16). Bwana Yesu naye alifanya vivyo hivyo. Imeandikwa: Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. (Luka 10:1).