Matumizi ya Akili Bandia (AI) yanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya nguvu za kiuchumi na kijeshi duniani katika siku za usoni. Ushindani wa matumizi haya ya teknolojia umeifanya Marekani ianze kudhibiti mauzo ya nje kwenye chip za hali ya juu, na kuiondolea uwezo China wa kupata chip za hali ya juu za kompyuta, kuendeleza na kudumisha kompyuta kuu, na kutengeneza semiconductors za hali ya juu kwa madhumuni ya kijeshi na mengine, ili tu kupunguza maendeleo ya China kwenye masuala ya Akili Bandia.
Katika kuweka mambo sawa na kuondoa sintofahamu zilizopo katika uendelezaji wa teknolojia, China na Marekani hivi karibuni zilifanya mazungumzo yao ya kwanza ya ngazi ya juu kuhusu akili bandia mjini Geneva. Majadiliano yao yatazingatia hatari zinazojitokeza ambazo zinahusiana na mifumo ya AI, na jinsi nchi hizi mbili zinavyofafanua "hatari" na "usalama". Wakati huohuo pande zote mbili zitaelezea mbinu zao za ndani za kushughulikia hatari na kuweka kanuni za usalama wa AI, pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu usimamizi wa kimataifa.
Utafiti uliofanywa na Shirikisho la Kimataifa la utengenezaji wa vitu vya elektroniki IPC, unaonesha kwamba baada ya zaidi ya miongo miwili ya kupata bidhaa kutoka nje, Marekani sasa inajikuta katika hali mbaya. Inaweza kubuni na kusanifu vifaa vya kisasa zaidi vya elektroniki lakini haiwezi kuvitengeneza. Na hapa ndipo kichocheo cha ushindani kinapoanzia, kwani Marekani bado inataka kuendeleza utukufu na ukuu wake kwenye masuala ya teknolojia.
Marekani pia inaonekana kufumbia macho mfumo mzima wa utengezaji wa vitu vya kielektroniki. Mfumo huo unahitaji hatua nyingi ili kupata chip ya mwisho. Lakini kila mtu anafahamu kwamba hakuna nchi hata moja inayoweza kujitegemea kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho wakati chip inapopatikana.
Marekani inatawala soko la usanifu wa semiconductor, ikiwa na hisa 85% duniani, huku 5% ikisalia kwa nchi za Asia. Na China kwa upande wake pia ni muagizaji mkubwa na ina soko kubwa zaidi la semiconductor, ikiwakilisha 31.4% ya mauzo ya mwisho duniani kote. Kwa maana hiyo marufuku ya hivi karibuni ya Marekani kwa mauzo ya bidhaa za hali ya juu kweli inaleta kikwazo kikubwa kwa China. Lakini, hii haimaanishi kuwa China imeachwa tu bila rasilimali zinazohusiana na matumizi ya kompyuta na haiwezi kuunda chip zake.
Ikijibu marufuku ya teknolojia ya Marekani, China imetekeleza sera ili kufikia ushindani wa kimataifa. Kampuni ya Baidu, Tencent, na kampuni nyingine za teknolojia za China zilitangaza kuwa zina chip za kutosha za AI ili kupunguza athari za marufuku ya usafirishaji ya Marekani. Wakati huohuo Baidu kwa muda mrefu imekuwa ikitengeneza chip zake za Kunlun kwa ajili ya hesabu za AI.
Juu ya yote mazungumzo haya ambayo yalikuja baada ya makubaliano ya mwezi Novemba kati ya Marais Joe Biden na Xi Jinping, ambayo yanatilia mkazo juu ya haja ya kushughulikia hatari za mifumo ya hali ya juu ya Akili Bandia na kuboresha usalama wa Akili Bandia, huenda yakapunguza wasiwasi na mtazamo mbaya wa Marekani dhidi ya China. Vile vile Marekani kuweza kufungua milango yake na kuipa haki yake China ya kushindana kwa usawa kwenye masuala ya teknolojia bila kuiwekea vizuizi vyovyote.