SoC03 Je, ni Utu ama Sheria huinua taasisi?

Stories of Change - 2023 Competition

Mhenga Mpya

New Member
Joined
Jun 2, 2023
Posts
2
Reaction score
2
Ni Dhahiri kuwa binadamu amebarikiwa uwezo asilia wa kung’amua mambo na kufanya maamuzi . Uwezo huo ni utashi. Utashi aghalabu hutegemea pia maarifa/stadi alizonazo mtu husika ili kufanya maamuzi.

Utashi wa binadamu si tu pekee unahusika na maamuzi, bali hujijenga kwenye misingi ya Utu wa mtu husika. Watu wengi hudhani kinachomfanya mwenye wadhifa husika kuwa mwadilifu ni sheria ama taratibu zilizowekwa ili kumdhibiti. La hasha! Sheria haiwezi kumzuia mtu ama kiongozi mwenye dhamana kuomba rushwa. Sheria inashughulika na matokeo ya jambo mfano sheria inaweza kumuwajibisha mtu baada ya kubainika aliomba rushwa lakini si kumzuia kuomba rushwa.

Kinachoweza kumzuia kiongozi asikiuke taratibu/kanuni za taasisi husika ni maadili halisi yaliyojijenga katika Utu wake. Utu wa mtu ndiyo kielelezo na nguvu zake zilipo ,ndiyo nguvu ya ushawishi wa kiongozi yeyote yule. Utu ukipotea na heshima inapotea. Hivyo ili kuleta uwajibikaji katika taasisi zetu watu wafundishwe Utu na thamani ya Utu wao tangu utotoni, itakuwa ni vigumu sana kuutupa/ kuacha Utu wao hata wakiwa wakubwa kwenye majukumu yao. Ndiyo maana vitabu vya dini vinasisitiza kumlea mtoto katika njia ifaayo naye hataiacha hata uzeeni. Ni muhimu kuzingatia kuwa Utu unaweza kumzuia mtu asifanye uovu au asikiuke taratibu za taasisi lakini sheria kwa upande wake hushughulika na mtu baada ya kosa.

Namna nyingine ya kuongeza ufanisi katika uwajibikaji wa taasisi za biashara, elimu ama taasisi yeyote ile yenye mgawanyo wa ngazi za utawala/madaraka ni kubana masilahi ya wasimamizi wa idara pale uzembe unapofanyika. Kwa mfano; Prof Mussa Assad; CAG mstaafu alishauri kupunguzwa mishahara kwa wakuu wa idara wanaoshindwa kuchuka hatua za kuwawajibisha wale wote wanaosababisha uzembe kufanyika katika idara zao. Pia posho za kila mara zinaweza kuondolewa pale uwajibikaji ama ufanisi unaposhuka kiwango. Hii njia inaweza kuwa nzuri kuwabana mameneja na wakurugenzi wa taasisi kwani hakuna mkuu wa idara/kitengo anayependa kuona posho zinaondolewa ama mshahara wake ukipunguzwa mwezi hadi mwezi.

Sambamba na kubana masilahi ya wakuu wa idara wanaoshindwa kuwajibika kisawasawa; njia nyingine ya kuimarisha uwajibikaji ni kuwatunuku wafanyakazi wa taasisi wanaofanya vizuri katika idara zao. Ni muhimu taasisi iwe na utaratibu wa kuchagua siku ama wiki maalum kwa ajili ya kuwazawadia wafanyakazi wake wanaojitoa na kujituma kwa bidii ili kuleta ufanisi ndani ya taasisi. Ukiwa kama mkuu wa idara; uwe meneja, mkurugenzi ama mwenyekiti wa bodi usiridhike kwa kusema tu, wafanyakazi si nawalipa au wanalipwa mishahara? Hivyo sioni sababu ya kuwazawadia au kuwatunuku. Watu hujitoa zaidi kwa taasisi kutokana na wanavyothaminiwa na wakuu wa taasisi husika. Mkuu wa kitengo, jifunze kuwatambua na kuwathamini wafanyakazi wako kwa kuwapongeza. Kuwatunuku inaweza ikawa ni pamoja na kuwapatia cheti cha heshima, ama pesa kiasi fulani. Hii itawapa wafanyakazi morali ya kujibidisha zaidi na kujiona ni sehemu ya taasisi na mchango wao unatambuliwa na kuthaminiwa. Jaribu kutumia hii mbinu kwenye taasisi yako na utarudi na ushuhuda wa shukrani.

Njia nyingine ya kuinua uwajibikaji na kuleta tija kwenye taasisi ni uwepo wa mafunzo kazini mara kwa mara kwa ajili ya kuwanoa wafanyakazi na kuwaongezea stadi za kuwasaidia kutimiza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Kampuni zote kubwa duniani kama Tesla, Amazon na SpaceX huwa zina hizi programu za kwajengea uwezo wafanyakazi wake. Mafunzo haya yagharamiwe na taasisi husika na kama taasisi haitamudu gharama kwa mkupuo basi mafunzo yanaweza kufanyika kwa awamu. Ni muhimu kwa wakuu wa idara kutoa fursa sawa ya ushiriki wa mafunzo kwa wafanyakazi wao ili kuondoa upendeleo ambao unaweza shusha ari ya kutumikia taasisi.

Urasimu kwa mashirika ya serikali na binafsi upunguzwe ili kurahisisha upatikanaji na utoaji wa huduma kwa wananchi; urasimu mkubwa hupelekea mianya ya rushwa kujitokeza maana watu hawapendi milolongo katika maamuzi na hiyo kwao ni usumbufu. Hivyo baadhi ya watu hulazimika kutumia njia ovu ya kutoa hongo/rushwa ili kurahisisha kuhudumiwa.

Kwa upande wa kuleta uwazi Zaidi katika maamuzi, mifumo ya Tehama iboreshwe ili kuruhusu wananchi kufuatilia kwa karibu maamuzi ya mambo yote yanayowahusu. Mfano utangazwaji wa zabuni ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa nchi kama Canada ina tovuti ya wazi ya Buyandsell.gc.ca inayohusika na kutoa taarifa za manunuzi ya umma . Mexico ina mfumo unaojulikana kama Compranet ambao unaruhusu utangazaji wa zabuni kwa uwazi na uwajibikaji.Marekani ina mfumo wa FedBizOpps unaoruhusu mawasiliano kati ya wafanyabiashara na serikali na kuwezesha utangazaji wa zabuni.

Mifumo ya Tehama pia iruhusu uratibu wa maoni ya wananchi na itoe nafasi ya upigaji kura juu ya mambo yanayowahusu wananchi moja kwa moja kuliko kuwaachia wachache wafanye maamuzi kwa niaba yao. Kuwa na mifumo imara ya Tehama ya namna hii itajenga Imani kwa wananchi na kujituma kwa ufanisi wa Taifa lao.

Mwisho kabisa tukumbuke maisha ni kuacha alama.Tuwajibike katika kujali Utu wetu na utu wa wengine pia. Kwa kujali Utu, hatutasita kujituma na kuwajibika ili kuacha alama njema kwenye maisha ya wengine.
 
Upvote 1
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…