Kutokana na experience, udumavu wa akili wakati mwingine tunautengeneza (create) wenyewe. Sijuwi kwa jirani zetu; Kenya, Uganda, na wengineo, lakini kwetu sisi Watanzania, mtu halijuwi jambo fulani, lakini anajifanya anajuwa.
Tabia hii imetamalaki sana miongoni mwetu, hasa vijana. Unakuta mtu hajuwi jambo fulani, na wakati huohuo yuko mtu anayelijuwa jambo hilo, badala ya kuuliza ili tujuwe, mtu anaona ataonekana mshamba na hivyo kuendelea kubaki nalo moyoni mwake na kutolijuwa jambo hilo.
Nimekaa katika vijiwe mbalimbali, mtu (mwerevu) akiuliza jambo fulani, vijana wa pale kijiweni wanaanza kimzomea na kumcheka huku wakisema 'hata hili hujuwi?'. Kwa mtindo huu, utakuta vijana wengi wanaingia woga wa kudadisi mambo, kwa kuogopa kuchekwa na kuzomewa.
Kwa wenzetu wenye akili zao, hakuna jambo dogo wala kubwa katika kuuliza; jambo lolote analotaka kujuwa anauliza ili apate maarifa. Kila siku tunasema kuuliza sio ujinga, lakini hatujuwi maana ya sentensi hii. Na kwa maana hii, hatutakuja kuerevuka kamwe, tutabaki na ujinga wetu mpaka kiama!