Kwako Mh. Nchimbi,
Salaam! Natumaini umzima wa afya na unaendelea vema na shughuli zako za kuiongoza Wizara Nyeti ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo Jeshi la Polisi liko chini yake. Mheshimiwa, inawezekana kabisa kuwa Dr. Slaa, Mnyika na Lema wamezusha madai kuwa kuna mpango wa kuwadhuru ambao unasukwa na Vigogo wa vyombo vya usalama. Siwezi kusema ni kweli au la mpaka uchunguzi utakapokamilika.
Ila Mheshimiwa kwa kuwa tuhuma zimetolewa hadharani na wewe ukatoa kauli hadharani itakuwa vema uchunguzi ukikamilika taarifa nayo iwekwe hadharani.
Ningependa kukufahamisha kuwa wananchi walio wengi (mimi nikiwa mmoja wao) hawana imani na Jeshi la Polisi. Kuna viashiria vingi tu vya kukuonyesha kukosa imani kwa wananchi na chombo hiki muhimu ambacho kiesemwa na Katiba na sheria kuwa kina jukumu la kuwalinda raia na mali zao.
Moja ya viashiria Mheshimiwa ni kuongezeka kwa wimbi la kile kinachoitwa raia wenye hasira kali kutoa hukumu ya kipigo kikali na pengine hata kifo kwa watuhumiwa wa makosa ya udokozi na ukwapuaji wa mali za raia wenzao. Hujawahi kujiuliza kwanini raia wanapowakamata watuhumiwa huwa hawawapeleki Polisi na badala yake wanatoa hukumu wao wenyewe???
Kwa taarifa Mheshimiwa, wananchi walio wengi wanaona kupeleka mashauri yao polisi wakati mwingine ni sawa na kupoteza muda na hata fedha. Mara nyinigi utatakiwa kununua au kutoa fedha za jalada la kufungulia shauri lako na utatakiwa kutoa fedha au kununua karatasi za kuchukulia maelezo yako.
Hapo upelelezi haujaanza. Upelelezi ukianza utatakiwa kutoa fedha za usafiri kwa askari aliyepangiwa kufanya upelelezi wa shauri lako na wakati mwingine kuvunja shughuli zako na kuambatana nao wakati wa kile wanchokiita kumtafuta mtuhumiwa wako.
Wakati mwingine utatakiwa kutoa fedha za mawasiliano (kununulia muda wa maongezi) na posho ya kuwalipa watu wanoitwa informers wa Polisi ambao wengi wana record Mbaya katika jamii halafu upelelezi unaweza kuendelea milele hasa inapotokea mtuhumiwa naye anakuwa na uwezo wa kuwapooza wapelelezi.
Mheshimiwa, katika mazingira haya bado utasema kuwa mtu asiyeliamini Jeshi la Polisi kwa maana ya askari Polisi wanaotekeleza majukumu ya Ki-polisi ana matatizo? Ningekushauri ufanye uchunguzi uone ni mashauri mangapi yaliyofunguliwa polisi ambayo walalamikaji wameamua kumwachia Mungu matatizo yao baada ya kuona wamegeuzwa ngombe wa maziwa na wapelelezi wa polisi, kesi zilizotupiliwa mbali na mahakama baada ya wapelelezi kupeleka ushahidi wa kitoto kwa lengo la kutengeneza mazingira ya watuhumiwa kuachiwa huru na mahakama.
Nawasilisha hoja!