Kwahio hii mipango ni ya kumfurahisha nani ?
Mwisho wa siku, sifa na utukufu zinamrudia Mungu Mwenyewe, kwa sababu mambo yote hutendeka kwa manufaa ya wale wampendao Mungu.
Unapogusia matukio ya ulimwengu, kamwe usisahau picha pana ama chimbuko la hayo yote—dhambi.
Bwana Mungu mwenye hekima yote anashughulikia tatizo kuu la dhambi kwa namna ambayo wakati mwingine mwanadamu anaweza asielewe mantiki kamili ya utendaji huo.
Ila mwishowe kila nafsi itakiri kwamba matendo Yake ni makuu na ya ajabu na kwamba njia Zake ni za haki na za kweli (Ufunuo 15:3).
Unadhani Mungu hufurahishwa na mateso ya wanadamu? Kuruhusu wakati fulani tupitie taabu za dunia haina maana kwamba ndio mpango Wake. Wala kamwe hajapanga wengine wateseke na wengine wanufaike duniani.
Pia haina maana kwamba hana uwezo wa kutuepusha na masaibu hayo. Naamini kwamba Mungu ana kusudi fulani katika kila jambo analopitia mwanadamu.
Ni vyema tukajifunza kuuona utendaji wa Mungu wenye hekima na upendo hata katikati ya majanga na misiba.
Dhambi imemfanya mwanadamu kujijengea fikra kwamba kwa namna fulani yeye ni mungu wa maisha yake mwenyewe.
Lakini kadiri mwanadamu anavyoendelea katika mawazo potofu kama haya ndivyo anavyozidi kuzama zaidi katika janga la utumwa wa dhambi na matokeo husika ya dhiki.
Laiti tungekiri kwamba sie ni viumbe na kwamba yuko Muumbaji wetu, ingekuwa rahisi sana kusaidika. Mgonjwa asiyehitaji msaada akiamini kwamba hata tatizo, hatima yake ni mbaya zaidi.
Katika mazingira haya yote, Mungu lazima aoneshe kwamba Yeye ni Baba mwenye upendo na rehema, lakini pia ni Bwana aichukiaye dhambi—atangazaye kwamba mshahara wa dhambi ni mauti.
Mwisho, kuhusu falme mbalimbali kuinuka na kuanguka, zote hizo hutokea kwa sababu ya ukweli uleule kwamba Mungu ameruhusu hivyo.
Ndivyo maana viongozi na watawala wanakumbushwa daima kutenda haki wakitambua kwamba wako madarakani ili kutekeleza amana hiyo kwa niaba ya Mungu aliyewakasimu mamlaka hayo.
Taifa la Marekani ni muhimu sana katika unabii kama yalivyokuwa mataifa na falme za zamani kama vile Rumi, Misri, Babeli, Asiria, Siria, Uajemi na zinginezo.
Haiwezekani kuzungumzia matukio ya siku za mwisho bila kuizungumzia nchi ya Marekani, kama nilivyosema awali, kwa wema ama kwa ubaya.
Kidini na kihistoria, taifa hili limejiweka katika nafasi ya kuhusiana kwa ukaribu zaidi na utekelezaji wa mpango mkuu wa Mungu kuhusu ukombozi, hasa katika siku hizi za mwisho.