Na mimi nondo ninazo wala sihitaji nondo kutoka kwako mkuu, uzinzi upo ndani ya uasherati
zerominus10 ingawa umekataa kwamba hutaki nondo zangu, mimi nakupa tu ili kuitetea hoja yangu ile. Naomba usome kisha na wewe unipe nondo zako. You never know, labda za kwako zimeenda shule zaidi. Niko tyari kujifunza.
Mimi naamini hivi:
Mtu anaruhusiwa kumwacha mkewe kwa sababu ya uasherati tu. Biblia ya SUV inasema hivi katika Mathayo 5:32
"lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.”
Neno la Kigiriki lililotumika hapo kwenye uasherati ni “porneia” – sio “moicheia” (uzinzi). Kwa hiyo sio sahihi kusema
'kwa sababu ya uzinzi'
Andiko hilo la Mt 5, linafafanuliwa vizuri na habari ya Yusufu na Mariamu katika Mathayo 1:18-19. Chunguza vizuri habari hiyo utaona kuwa walikuwa wachumba, ingawa Yusufu aliitwa “mumewe”
"...Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri.”
Baadaye Malaika akamwambia Yusufu asimwache Mariamu “mkewe.” Hivyo hao waliitwa mume na mke kwa desturi za kiyahudi lakini walikuwa bado hawajaanza kuishi pamoja kikamilifu. Katika hali hiyo Yusufu alikuwa na haki ya kumwacha Mariamu kama angebaini amefanya “porneia” – uasherati.
Huo ndio mfano mzuri unaoonyesha uhalali wa kumwacha mke kwa sababu ya uasherati(porneia). Ndio sababu hata leo kuna msemo kwamba uchumba sio ndoa. In other words, mtu akitoa posa baadaye akagundua mwenzake amefanya uasherati, ni ruksa kabisa kumwacha au kuvunja huo uchumba.
Katika Mt 5:312 Yesu amepinga utoaji wa talaka. Angalia anavyosema:
"lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini."
Maandiko hayo maana yake ni kwamba ukimwacha mke wako kwa madai kwamba amefanya uzinzi, huyo mke atahesabiwa mzinzi maisha yake yote. Na mtu yeyote atakayemwoa, na yeye atahesabiwa mzinzi. Kwa hiyo kwa maneno mengine mwanaume aliyefunga ndoa halali hapaswi kumwacha mkewe.
Ndoa ikiishafungwa, wanandoa hawapaswi kutengana kwa sababu yoyote ile, hata uzinzi. Angalia Yesu anavyosema katika Mathayo 19:6
"Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.”
Soma 1 Wakorintho 7:10-11 uone pia jinsi Paulo alivyosisitiza tusiachane:
“Lakini wale waliokwisha kuoana nawaagiza; wala hapo si mimi, ila Bwana; mke asiachane na mumewe; lakini, ikiwa ameachana naye, na akae asiolewe, au apatane na mumewe; tena mume asimwache mkewe.”
Kwa hiyo, uzinzi sio sababu ya kuvunja ndoa. Kumbuka tena mafundisho ya Yesu kuhusu msamaha:
Mathayo 18:21-22
"Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.”
Je, kama tunawasamehe ndugu, marafiki na majirani, sembuse mwenzi wetu wa maisha?
Kumbuke tena yule mama aliyefumaniwa. Yesu alimwambia nini. Kumbuka yule mama msamaria aliyekuwa na waume watano, aliambiwa nini. Ni msamaha tu. Hata sisi tulipokuwa wenye dhambi, Yesu alitusamehe dhambi zote. Kwanini sisi tusisamehe?
Mt 6:14-15
Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
Haya, mimi nimemaliza. Weka hapa sasa na wewe nondo zako, zinazokuambia kwamba ni halali mume kumwacha mkewe kwa sababu ya uzinzi.